July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Gwajima: Viongozi wa Serikali wanamchonganisha Rais

Josephat Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe (CCM)

Spread the love

 

MBUNGE wa Kawe, Askofu Dk. Josephat Gwajima amesema baadhi ya viongozi wa serikali badala ya kutatua migogoro ya ardhi wanachochea migogoro hiyo na kuichonganisha na serikali na wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Gwajina ambaye ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ametoa kauli hiyo leo tarehe 27 Mei, 2022 jijini Dodoma wakati akichangia hotuba ya waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Dk. Angeline Mabula ambaye amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Amesema wilaya ya Kinondoni ni kinara wa migogoro ya ardhi nchini Tanzania na kutolea mfano kuwa katika jimbo lake la Kawe kuna migogoro mingi inayochochewa na viongozi wa Serikali.

“Mfano kuna eneo linalitwa Mbweni Mpiji, siku moja nimepigiwa simu na katibu wangu, kwamba kuna matrekta na mabuldoza yanabomoa nyumba za wananchi, nikakimbia kwenye kata hiyo ya Mbweni, nilikuta nyumba 103 kubwa zimeanguka chini, mbaya zaidi nikakuta kuna baadhi ya watoto wameachwa kwenye hizo nyumba.

“Polisi nao wanapiga mabomu, kina mama wanachapwa viboko, sikuamini hii ndio Tanzania ninayoijua,” amesema.

Amesema kilichomshangaza alipomuuliza Ofisa Upepelezi wa wilaya hiyo kama anayo ‘order’ ya mahakama inayomruhusu kubomoa nyumba hizo, alijibu kuwa hana.

“Nikafuata wananchi kama wana hati yoyote nao wakasema hawana… nikauliza sasa kwanini wanabomoa nyumba za wananchi?

“Wakaniambia eneo hili kwenye ramani limepangwa kuwa eneo la bustani ya miti ya wizara. Bustani yenyewe haijajengwa na wala haipo. Wananchi wamejenga nyumba zao wanaishi zaidi ya miaka mitano mtu anakwenda kuangusha chini nyumba za wananchi 103.

“Wananchi hao hao tulipita kuomba kura za Rais na Mbunge, huyu polisi anayetekeleza hili jambo hana vielelezo vyovyote,” amesema.

Amesema alimpigia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni naye akasema hajamuelekeza yeyote.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula

“Baadae wakasema wameelekezwa na wizara. Inashangaza kweli! viongozi wa kiserikali waliowekwa kwa ajili ya kutetea wananchi wanakuwa sehemu ya kugombanisha wananchi na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Ni vizuri kukubali, kiongozi yeyote wa kiserikali au wa kisiasa kupitia CCM, jukumu lake la kwanza ni kuhakikisha Rais amekaaa kwenye kiti salama na yuko salama kwenye shughuli zake.

“Inapotokea kiongozi wa kiserikali au wa kisiasa anayetokana na CCM hafanyi jukumu hilo, huyo anafanya hujumu juu ya Rais wetu na chama chetu,” amesema.

Amesema jimbo la Kawe lina migogoro ya ardhi mingi na hakuna anayeonekana kujali kusuluhisha migogoro hiyo.

Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na hatua walizochukua, Naibu waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete na Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Nape Nnauye ambao walifika jimboni Kawe katika mitaa ya Jogoo na Ndumbwi na kutatua mgogoro wa anuani za makazi.

Amesema wananchi hao walikuwa wamezuiwa kuwekewa anuani za makazi kwa sababu eneo hilo lenye nyumba ya zaidi 4,500 ni la viwanda.

“Hakuna kiwanda chochote, kesi yoyote wala hakuna anayewadai ila wananchi wamegomewa kuwekewa anuani za makazi. Nape na Ridhiwani walikaa ndani ya saa mbili, walitatua mgogoro ambao ulidumu miaka 30 iliyopita,” amesema.

Amesema ni afadhali kulaumiwa kwa kufanya maamuzi yasiyosahihi kuliko kutokuamua kabisa.

error: Content is protected !!