June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Gwajima “achezeshwa danadana”

Askofu Josephat Gwajima

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (kushoto) akitoka kituo cha Kikuu cha Polisi mara baada ya kumaliza mahojiano, akiongozana na wachungaji wake wa kanisa lake.

Spread the love

JOSEPHAT Gwajima-Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amejikuta akihojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mara ya tatu pasipo kutambua kosa lake halisi. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Askofu Gwajima aliitwa kwa mara ya kwanza Machi 28, mwaka huu, akidaiwa kutoa kauli ya uchochezi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Katika ukanda wa video unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Gwajima anaonekana kumshambulia kwa maneno Kardinali Pengo akidai amewasaliti maaskofu wenzake waliotoa tamko la kuwataka waumini wao waipigie kura ya hapana katiba pendekezwa.

Hata hivyo, mahojiano yake na polisi hayakufika mwisho kutokana na hali ya Gwajima kubadilika ghafla na hivyo kulazimika kukimbizwa hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikolazwa kwa siku tatu.

Aprili mosi, Askofu Gwajima alitakiwa kufika kituo cha polisi Oysterbay kwa ajili ya mahojiano zaidi, lakini pia haikuwezekana kutokana na afya yake kutotengamaa, hatua iliyomfanya awekwe kiporo hadi leo.

Akisindikizwa na waumini wake, Gwajima aliwasilia kituo kikuu cha polisi saa 2:00 asubuhi, tayari kwa ajili ya mahojiano aliyodhani ni kuhusu kauli yake dhidi ya Askofu Pengo, ambaye hata hivyo alishatangaza kumsamehe, lakini hali ikawa tofauti.

Akizungumzia mahojiano hayo muda mfupi baada ya kutoka nje, wakili wa Gwajima, John Mallya, amesema, wanashangazwa na kitendo cha polisi kuuliza maswali ambayo hayahusiani na kosa tajwa.

Kwa mujibu wa Mallya, mahojiano ya leo yalijikita katika masuala binafsi ya mali na maisha ya Gwajima.

“Baada ya kumaliza mahojiano, wamemtaka Gwajima awasilishe vitu 10 na akishatimiza masharti hayo ndipo wataweza kumfungulia mashtaka mahakamani,” amesema.

Mallya ametaja vitu hivyo kuwa ni, hati ya usajili wa kanisa, bodi ya wazee wa kanisa, hati ya umiliki wa helikopta yake, mali za kanisa, nyumba zake, idadi ya makanisa yaliyo chini yake, wafadhili wa kanisa, idadi ya maaskofu wake na mpiga picha za video kanisani kwake.

“Hivyo vitu vyote vipo, hatuna wasi wasi juu ya hilo. Tumeambiwa tuje kuviwasilisha tarehe 16 mwezi huu, saa mbili asubuhi. Na kama kutakuwa na utofauti, labda kitu kimoja hakijapatikana, basi tutaacha sheria ichukue mkondo wake,” amesema Mallya.

“Baada ya kumalizika kwa mahojiano na kukamilisha masharti yao, tunatarajia kesi itapelekwa mahakamani, huko ndiko tutapata nafasi ya kuomba ufafanuzi juu ya kesi hii. Je, kesi ya matusi inahusikanaje na maisha binafsi na mali za mtuhumiwa? Amehoji Malya.

error: Content is protected !!