January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Dk. Bagonza: TLS imara ni Hoseah

Dk. Edward Hoseah mgombea urais chama cha wanasheria Tanganyika (TLS)

Spread the love

 

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kutafuta kiongozi mahiri atakayeweza kukivusha chama chao. Anaripoti Regina Mkonde, Arusha … (endelea). 

Amesema, ni muhimu TLS ikaongozwa na Rais mahiri mwenye upeo wa kimataifa (Cross cultural exposure and experience), kwa kuwa uimara wa taasisi hiyo, ni uimara wa taifa.

Katika andishi lake alilolisambaza kupitia vyombo vya habari, Dk. Bagonza anaeleza, “uchaguzi wa TLS, utakaoendana na kupatikana kiongozi imara, ni muhimu kwa mustakabali wa wanasheria na taifa.”

Chama cha mawakili nchini – Tanganyika Law Society (TLS), kinatarajia kufanya uchaguzi wake wa viongozi, Ijumaa wiki hii, tarehe 14 Aprili 2021, jijini Arusha na hivi ndivyo alivyosema:

“Kwa miaka 5 mfululizo, chaguzi za TLS zimekuwa zinavuta hisia kali nchini. Sababu ni nyingi, lakini moja si ya kupuuza.

Askofu Benson Kagonza, KKKT Dayosisi ya Karagwe

Kwamba, haja ya kuwa taasisi huru na imara katika taifa letu, haikupewa kipaumbele. Badala yake, taifa lilizama katika kushabikia watu binafsi wenye nguvu kuliko taasisi wanazoziongoza.

Mtindo huu umeenea nchini kote katika sekta za umma na binafsi. Neno liitwalo “HURU” limegeuka kuwa adui katika taifa.

Haishangazi hivi sasa kwenye mitandao ya kijamii, makundi yenye neno “HURU” ndiyo yanavutia washiriki. Uhuru wetu kama Taifa na Uhuru wa watu binafsi, umeingiliwa sana.

Awamu ya sita ina jukumu ya kukuza Uhuru wa watu wetu. Taasisi kama TLS ina dhamana ya kuongoza jitihada za kuongeza na kutetea uhuru katika taifa.

Ili kutekeleza dhamana hiyo, sharti TLS yenyewe iwe huru na imara. Uimara wa taasisi hii, unajengwa katika mambo makuu matatu muhimu kati ya mengi.

Dk. Rugemeleza Nshala, Rais wa TLS

Moja, ni uongozi wenye upeo wa kuikosoa na kukosoa. Pili, ni wanachama wenye wivu na TLS kuliko ukereketwa wao katika mambo mengine.

Tatu, ni msimamo thabiti wa kutetea haki na Uhuru wa watu hata kwa wale wasioitakia mema TLS.

Katika dhima ya kuongoza mchakato wa kitaifa wa kuthamini taasisi imara kuliko watu imara, TLS inamuhitaji Rais mahiri mwenye upeo wa kimataifa (cross cultural exposure and experience).

Waliogombea nafasi ya urais wanafaa lakini Dk. Edward Hoseah, anafaa zaidi zamu hii. Ni maoni yangu binafsi na sababu ninazo nyingi, nitaje moja:

Haogopi. Amewahi kunionya bila kujali nafasi yangu. Nawaheshimu sana wanaonionya kuliko wanaonishangilia na kunitukuza.

Kila la heri Wanasheria Wasomi wetu.

error: Content is protected !!