May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu Bagonza atoa ujumbe wa Krismasi, akumbusha machungu 2021

Dk. Benson Bagonza

Spread the love

 

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, mkoani Kagera, Dk. Benson Bagonza amesema, mwaka 2021 unaomalizika , umetawala habari mbaya za kutisha, kusikitisha na kuumiza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Karagwe … (endelea).

Askofu Bagonza amesema hayo katika salamu zake za Krisimasi na Mwaka mpya 2022, kwenda kwa waamini wa Dayosisi ya Karagwe.

“Mwaka unaoisha ulikuwa na habari nyingi mbaya, za kutisha na zisizoleta furaha,” amesema Askofu Bagonza

Kiongozi huyo wa kiroho amesema, “corona imeua wengi, mkuu wetu wa nchi alifariki, kukawa na ukame, mafuriko, kukosa maji, kukosa umeme, uvamizi wa kigaidi huku Kusini na majeraha mengi mioyoni mwa watu.”

Katika salamu zake, Askofu Bagonza amesema, “tunapofikia mwishoni mwa mwaka tukiwa hai, tunayo kila sababu kumshukuru Mungu kwa wema wake kwetu.”

Askofu Bagonza amesema, kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulitokea katika kipindi chenye changamoto nyingi kama tulizonazo sasa.

“Hapakuwa na furaha wala matumaini. Taifa teule la Israeli lilikuwa chini ya utawala mbaya na watu walikuwa wamekata tamaa.”

“Taifa lisilo na furaha ni mzigo mkubwa kuliongoza. Kwa hiyo tamko la Malaika lisemalo Msiogope, lilikuwa la maana sana, tamko lilisisitiza kuwa Malaika analeta habari njema za furaha kwa watu wote,” amesema

Askofu huyo amesema, “wapendwa furaha ni kitu muhimu sana. Unaweza kuwa na vitu vingine vyote kama fedha, afya, uzao, nafasi, mashamba, kazi nzuri na familia lakini kama huna furaha navyo havina maana yoyote.”

“Kwa hiyo malaika kuleta furaha kwa watu wote lilikuwa tangazo jema sana,” amesema

error: Content is protected !!