May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu awapa somo viongozi, agusia suala la machinga

Spread the love

 

MAKAMU Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kushuka chini kwa wananchi kujua matatizo yao badala ya kutoa maagizo wakiwa maofisini. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Dk. Chilongani ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma ametoa ushauri huo leo tarehe 25 Desemba 2021 kwenye ibada ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Amesema viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kukaa maofisini na kutoa maagizo badala ya kushuka kwa watu wanao waongoza na kujua matatizo yao.

“Viongozi wamekuwa wakikaa kwenye viti vyao vya enzi na kutoa maagizo lakini hawashuki kwa watu wa chini ili kuweza kujua matatizo yao.”

“Kiongozi yoyote kwa ngazi yoyote anatakiwa kuelewa matatizo ya watu anaowaongoza na siyo kukaa ofisini na kusuribi kuletewa taarifa ambayo wakati mwingine inaweza kuwa haina uhakika,” amesema Dk. Chilongani.

Aidha, amezungumzia suala la wafanya biashara ndogondogo maarufu machinga kuwa wamekuwa wakiondolewa katika maeneo yao bila kupewa utaratibu wa kufuata.

Amesema wanapowataka machinga kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni lazima kuwepo na utaratibu mzuri ambao hautakuwa na usumbufu.

Katika hatua nyingine amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tafadhali juu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa korona (Uviko-19), kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa Afya.

“Kwa sasa mnajua lipo wimbi la nne la kirusi cha Uviko-19, hivyo kuweni makini na kuchukua hatua za kujikinga na wimbi hilo kwa kufuata misingi na maagizo ya wataalamu wa Afya,” amesema Askofu Chilongani.

error: Content is protected !!