July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Askofu aungana na Ukawa

Spread the love

ASKOFU Mkuu wa Kanaisa la The Word Ministries Tanzania, Damas Thadei ameungana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) dhidi ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge, anaandika Dany Tibason.

Askofu Thadei ameshauri Serikali ya Rais John Magufuli kuachana na mpango wa kuliingiza taifa gizani kwa kutojua kinachoendelea bungeni, badala yake iruhusu vipindi hivyo kurushwa moja kwa moja.

Kauli ya kusitisha matangazo ya moja kwa moja ilitolewa na Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamatuni, Sanaa na Michezo, Januari mwaka huu na kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani, taasisi na watu wa kada mbalimbali.

Jumamosi wiki iliyopita, Freeman Mbowe wakati akisoma hotuba kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika Ofisi Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/17 alisema, hatua hiyo inanyima fursa wananchi kuangalia nini wabunge wanafanya kwa ajili yao.

“Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi, na wananchi wana haki ya kujua Bunge lao linavyofanya kazi ili wawe na uwezo wa kuwawajibisha wawakilishi wao iwapo hawafanyi kazi inavyostahili.

“Katika hali isiyo ya kawaida, serikali na uongozi wa Bunge, imewapoka wananchi haki yao ya kupata habari za Bunge kwa kuzuia mijadala Bungeni kurushwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa na vyombo vingine vya habari vya kujitegemea,” amesema Mbowe.

Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), alikosoa mpango huo na kudai, serikali inajihami kwa wananchi kutokana na madudu ndani ya utawala wa CCM.

Askofu Thadei amesema, serikali inapaswa kuacha kufanya kazi kwa woga na badala yake ijiamini na kutoa haki kwa Watanzania wanazostahili kuzipata na si vinginevyo.

Amesema, kitendo cha serikali kutoonesha matangazo ya moja kwa moja ya bunge ni dalili ya uoga na kuzuia wananchi kuona madudu yanayofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali.

“Kitendo cha serikali kuficha yanayoendelea bungeni ni kuminya uhuru wa wananchi kupata habari jambo ambalo ni viashiria vya kuvunja Katiba ya nchi,” amesema.

Amesema, hata kama serikali itaficha ukweli, upo uwezekano mkubwa kwa wananchi kujua nini kinaendelea.

Amesema, watumishi wa Mungu na watumishi wa serikali kazi yao ni moja ambapo ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki zao.

“Viongozi wa serikali wanahakikisha wanakusanya mapato kwa ajili ya kuwapatia watu wake maendeleo, wananchi kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanaisimamia serikali.

“Viongozi wa Dini kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanatunza roho za waumini wao ili kuondokana na tabia mbaya ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Hivyo kwa kutambua kwamba, kila mmoja anawajibu wake. Ni vyema mambo hayo yakatimizwa ili asiwepo mtu yeyote wa kulalamiwa,” ameeleza Askofu Thadei.

Hata hivyo amesema, staili ya Rais John Magufuli kutumbua majipu inapaswa kufuatwa sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Amesema, “haya yote ya wizi, ufisadi na ubinafsi unatokana na watu kutokuwa na hofu ya Mungu, kama watu watakuwa na hofu ya Mungu mambo yote ambayo yanalisumbua taifa yatakwisha.”

error: Content is protected !!