August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu ampa mtihani Rais Magufuli

Spread the love

WAKATI Rais John Magufuli akiwa kwenye hatarakati ya kujenga nidhamu kwa watumishi wa umma, pia ametakiwa kurejesha Azimio la Arusha, anaandika Dany Tibason.

Kauli hiyo imetolewa leo na Joseph Bundara, Askofu wa Jimbo la Dodoma, Kanisa la Methodisti Tanzania wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Kanisa hilo mkoani humo ambapo ameeleza, azimio hilo litarejesha Ujamaa na Kujitegemea.

Amesema, kitendo cha kutokuwepo kwa Azimio la Arusha kitaendelea kusababisha kuwepo kwa matabaka kati ya walionacho na wasiokuwa nacho hali inayosababishwa na kutokuwepo kwa usawa.

“Nataka kuliambia taifa kwamba, kama Serikali ya Awamu ya Tano haitaweza kurejesha Azimio la Arusha, kamwe nchi haitaweza kuwa na watu ambao wapo sawa.

“Kwa sasa kuna matabaka mengi na makubwa kati ya wenye nacho na wasio nacho na kutokana na hali hiyo, imepelekea watu wengi kuumizana iwe kwa mapigano au kudhulumiana.

“Na kama hali hii itaendelea hata utumbuaji wa majipu hautakuwa na maana yoyote kwani wenye nacho wataendelea kuwa nacho” amesema Askofu Bundara.

Hata hivyo amesema, katika muda wake wa uaskofu wa jimbo kwa miaka mitano, atahakikisha washirika wa kanisa hilo wanafanya kazi kwa ujamaa.

Amesema, hata kanisa pamoja na miradi mbalimbali ambayo wanatakiwa kuifanya lazima waifanye kwa ujamaa na wajenge tabia ya kutotegemea misaada kutoka katika mataifa mbalimbali.

“Waumini mnatakiwa kutambua kuwa, wafadhili ni nyie wenyewe hivyo hakuna mtu ambaye atawapatia misaada isipokuwa misaada ikitokea ni wazi itokee kwa nguvu ya Mungu na wala siyo ya kuwekewa masharti,” amesema Askofu.

error: Content is protected !!