Tuesday , 27 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Askofu akerwa aina upigaji kura wa sasa
Habari za Siasa

Askofu akerwa aina upigaji kura wa sasa

Wapiga kura wakiwa katika foleni ya kupiga kura
Spread the love

MATOKEO ya uchaguzi wa udiwani katika kata 43 nchi nzima uliofanyika Jumapili yameleta taswira kwamba itafika wakati Watanzania wapige kura kwa kutamka mgombea wanayemtaka badala ya kupiga kura kwa kutumia karatasi vituoni, anaandika Jabir Idrissa.

Kauli hii imetolewa leo na Askofu William Mwamalanga wa Kanisa la Pentekoste nchini (PEC), akitathmini matokeo ya uchaguzi huo pamoja na matukio yaliyoandamana na upigaji kura.

Uchaguzi uligubikwa na matukio ya vurugu na ukamataji wa mawakala na viongozi wa vyama vya upinzani kwa visingizio vya kuhusika na vurugu. Hakuna hata kiongozi mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekamatwa.

Askofu Mwamalanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Viongozi wa Dini, amesema ripoti zinazotoka kwa watu katika maeneo mengi ambako uchaguzi ulifanyika, zinaonesha kulikuwa na mpango mahsusi wa kuvuruga uchaguzi kwa manufaa ya CCM.

“Ukisikiliza yanayosemwa na watu waliokuwa maeneo ya uchaguzi utajenga hisia kuwa palikuwa na kila dalili watawala walitaka kulazimisha matokeo wayatakayo wao na sio kulingana na matakwa ya wananchi ambao ndio hutoa ridhaa kwa viongozi wawatakao. Sasa tunapata malalamiko ya wananchi kwamba wanataka wasikilizwe na vyombo vya kisheria kuhusu namna ya kupata haki yao ya kuchagua.

“Watu wanatulalamikia sisi viongozi wa dini kuwa hatushughuliki kukemea mtindo huu wa kuminya haki za raia wakati wa uchaguzi hivyo kuonesha kama tunaridhika na mtindo huu. Ni kadhia inayoonesha utawala bora umo kwenye mtihani katika nchi yetu.

“Lakini kwa hakika tunasema mambo haya kila wakati kwamba si mazuri; lazima raia walindwe ikiwemo kuthaminiwa kwa kura zao wakati wa uchaguzi maana hii ni haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Si vizuri watu kulalamika kuwa wamemchagua mgombea fulani awe kiongozi wao lakini mwishoni mwa uchaguzi, anatangazwa mtu mwingine ambae wananchi wana uhakika amepata kura ndogo sana,” alisema katika mahojiano yake maalum na MwanaHALISI Online, yaliyofanyika leo kwa njia ya simu.

Amesema misingi ya demokrasia inapaswa kuenziwa kwani ina maana yake kubwa ikiwamo kuondoa taratibu za kupata viongozi kwa njia za asili kama wananchi kusimama nyuma ya mgombea ambaye mtu anamtaka au kutamka jina la mgombea anayemtaka.

Ameongeza kuwa inashangaza kuitarajia haki kwa mfano katika mazingira ambayo Jeshi la Polisi limekamata mawakala wote wa vyama vya upinzani kwenye kituo cha uchaguzi. “Ni nani atakayesimamia haki ya wagombea ambao mawakala wao wamekamatwa na kupelekwa vituoni,” alihoji.

Jeshi la Polisi kupitia makamanda wa mikoa mbalimbali walikaririwa wakisema kwamba walilazimika kukamata watu walioripotiwa kuwa wameshiriki vitendo vya fujo wakati wa uchaguzi. Hata hivyo, hakuna maelezo ya kuridhisha kuhusu wale waliokamatwa siku moja kabla ya Jumapili, siku ya uchaguzi.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa maeneo mbalimbali walikamatwa siku ya kabla ya uchaguzi na kuwekwa vituoni mwa polisi.

Katika uchaguzi huo, CCM imetangazwa kushinda Kata 42, zikiwemo kata tano za Arumeru mkoani Arusha ambako madiwani wake walijiuzulu kwa mkupuo katika kile kilichosadikika kuwa ni njama za CCM kuhodhi siasa za maeneo hayo na hivyo kutawala kimaamuzi kwenye halmashauri. Madiwani waliojiuzulu ni wale waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.

Chadema ilifanikiwa kukamata vielelezo vya kuonesha kuwa hatua hiyo ilikuwa ni mkakati wa CCM kwa kutumia viongozi wa kiserikali ambao waliwashawishi madiwani kwa ahadi ya fedha na vyeo.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!