December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askofu akemea watu kupenda kulalamika

Mji wa Dodoma

Spread the love

WATANZANIA wametakiwa kuachana na tabia ya kulalamika na badala yake wafanye kazi huku wakiwa mstari wa mbele kupinga unyanyasaji na ukandamizwaji, anandika Dany Tibason.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Askofu Mkuu wa Church of God in Tanzania, Timoth Lutoloola alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa kongamano la watumishi lililofanyika Chang’ombe mjini Dodoma.

Kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa ili kuwepo maendeleo ya mtu binafsi, kikundi au taasisi pamoja na taifa kwa ujumla ni wajibu wa kila mmoja akafanya kazi kwa bidii huku akiwa anatambua haki zake.

“Watanzania ni lazima tukafanya kazi kwa bidii na tukaachana na malalamiko mbali na kufanya kazi ni lazima kutambua wajibu wetu sambamba na kusimamia haki na pale haki inapovunjwa ni vyema tukasema ukweli bila kuwa na woga.

“Hakuna maendeleo ambayo yanaweza kuja kutokana na malalamiko na manung’uniko bali maendeleo yanatokana na juhudi za kazi ikiwa ni pamoja na kusimamia haki pasipokuwa na uoga” amesema Makamu Askofu Mkuu.

Katika hatua nyingine amewataka viongozi wa dhehebu hilo kuhakikisha wanajihusisha katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo badala ya kutegemea sadaka au ufadhili.

Hata hivyo, amesema viongozi hao wanatakaiwa kuzitunza vyema familia zao huku wakiwajali hata watu ambao wanauhitaji wa mambo mbalimbali kwa kutambua kuwa viongozi wa dini ni viongozi wa kiroho na kimwili.

Akizungumzia juu ya amani amewataka viongozi wote kwa maana wale wa dini, siasa na serikali, kusimamia haki ili kujiepusha na uvunjifu wa amani.

error: Content is protected !!