January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askari wa Wanyamapori wadaiwa kuwapiga wafugaji Ngorongoro

Spread the love

MGOGORO mpya umeibuka Ngorongoro baada ya Askari wa Wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kudaiwa kuwapiga wafugaji wa kata za Endulen na Alaitole wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo. Anaandika Ferdinand Shayo, Ngorongoro … (endelea).

Vurugu hizo zimeibuka mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha wafugaji 27 kujeruhiwa huku wengine 22 kuwekwa kizuizini, pamoja upotevu wa mifugo 52 ambayo haijulikani ilipo.

Chanzo cha mgogoro huo kinaelezwa kusababishwa na baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo yao eneo la Mash ambalo hutumiwa kunywesha mifugo yao hasa kipindi cha kiangazi, ambapo askari walipowakuta walianza kuwashambulia kwa madai kuwa hawaruhusiwi kufuga mifugo yao katika eneo hilo.

Wafugaji hao wameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kiangazi ambacho wanakabiliwa na uhaba wa maji hasa kwa ajili ya mifugo yao na wamekuwa na utaratibu wa kutumia eneo hilo kwa makubaliano ya kila mwaka ila kwa mwaka huu imekua tofauti kwani wamefukuzwa pamoja na kupigwa na askari hao kinyume cha sheria.

Mzee wa mila jamii ya Wamasai, Kadogo Olduati amesema kuwa kwa kipindi kirefu wameishi katika ardhi mseto yenye mchanganyiko wa wanyamapori na mifugo pamoja na binadamu bila kusababisha athari zozote katika kwa mazingira na wanyama.

Olduati ameitaka Mamlaka ya Ngorongoro isiegemee upande wa wanyamapori na kuwasahau wafugaji ambao hutegemea ufugaji kuendesha maisha yao ya kila siku.

Katibu wa Baraza la Wafugaji, James Moringe ameiomba mamlaka ya Ngorongoro na Baraza la wafugaji kwa pamoja kuitisha kikao cha haraka ili kuepusha mgogoro huo ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuathiri uhifadhi na utalii kwa ujumla.

Mhifadhi wa Ngorongoro hakuweza kupatikana kuzungumzia tikio hilo kwa kuwa simu yake ya mkononi haikupatikana, lakini pia walinzi waliwazuia waandishi kuingia ofisini kwake mpaka watakapopata kibali maalum.

error: Content is protected !!