August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Askari JWTZ kortini kwa mauaji

Spread the love

ASKARI tisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutoka kikosi cha 823 Msange, mkoani Tabora wamefikishwa kortini, wakituhumiwa kuwashambulia wananchi na hatimaye kusababisha kifo cha mtu mmoja, anaandika Charles William.

Samson Kabigi, Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi, akiwasomea mashitaka hayo mbele ya Agatha Chigulu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo tarehe 10 Septemba mwaka huu, saa tisa mchana katika kata ya Chemchemi.

Kabigi amedai kuwa askari hao, waliwapiga wananchi na hatimaye kumuua mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Omary Zuberi Shaaban ambaye ni mkazi wa kata hiyo.

Miongoni mwa askari walioshitakiwa kwa kesi hiyo ya mauaji ni pamoja na Private Yustin Mwingira (24), Private Shomary Hemed Mbaruku (24), Private Rajab Mbasa (24) na Private Said Rashid.

Wengine ni Koplo Msafiri Kitwima (26), Private Thobias Salum (30), Private Rogasian Shayo (24) na wengine wawili.

Agatha Chingulu, Hakimu wa mahakama hiyo, aliwataka washitakiwa hao kutojibu chochote mahakamani hapo kwani mahakama hiyo, haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo bali Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 5 Oktoba, mwaka huu ambapo itatajwa tena. Askari hao wote tisa wamerudishwa rumande.

Kesi hii inakuja ikiwa ni kipindi kisichozidi wiki moja tangu Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam imuhukumu adhabu ya kunyongwa mpaka kufa SP Christopher Bageni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni kwa kuhusika na mauaji ya watu wanne wakiwemo wafanyabiashara watatu na dereva teksi.

 

error: Content is protected !!