July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ASASI za kiraia zalalama Z’bar

Spread the love

ASASI za kiraia za Zanzibar zimetoa tamko la kutaka dhana ya utawala bora iheshimiwe katika muendelezo wa vikao vya majadiliano vinavyofanyika miongoni mwa viongozi wakubwa Zanzibar. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Bwawani mjini hapa jana, wawakilishi wa asasi zipatazo 250 wamesema vikao vya majadiliano yanayohusu mgogoro wa kisiasa vinapaswa kutolewa taarifa kwa umma.

Wawakilishi wa asasi za kiraia wamesema umuhimu wa wananchi kufahamishwa kinachoendelea unapata nguvu kwa sababu kufuatia kufutwa kwa uchaguzi Oktoba 28, “nchi imeachwa katika ombwe kubwa la kisiasa, na hali ya taharuki na wasiwasi mkubwa. Hii ni kutokana na kuwapo ukimya wa muda mrefu tokea Mwenyekiti atoe tangazo hilo.”

“Hali hii ni kinyume na matakwa ya utawala bora yanayohimiza uwazi na ushirikishwaji wananchi katika mambo yanayowahusu,” wamesema wawakilishi wa asasi Zanzibar ikiwemo ANGOZA yenye mtandao wa asasi zipatazo 200.

Wamesema wakati wanaridhishwa na taasisi za ndani ya nchi na nje kwa namna zilivyotoa mchango wao katika kuhangaikia muafaka miongoni mwa wanasiasa Zanzibar, ni “wajibu wa wanasiasa wetu kudhihirisha ukomavu wao wa kisiasa katika kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hili linaloikabili nchi yetu.”

Huku wakitoa mapendekezo matatu ya kuzingatiwa, wawakilishi hao wa asasi wanawakumbusha viongozi wa kisiasa kuwa wananchi wanaathirika na hali ya sintofahamu kijamii na kiuchumi.

Kuiacha hali ya ukimya mrefu iendelee kunaweza kuhatarisha amani ya nchi na wananchi kuathirika zaidi ya ilivyo sasa wengi wamejiinamia kwa kutojua hatima itakuaje.

Mapendekezo ya asasi hizo ni (i) Viongozi wa kisiasa kuwa makini zaidi katika kumaliza mgogoro unaoendelea na kutatua kwa njia ya amani na kwa haraka;

(ii) Viongozi wa vyama vya siasa vinavyotofautiana kuhusu uchaguzi kutoendelea kuwagawa wananchi kutokana na kauli zao badala yake wakae pamoja na kutafuta muafaka kwa njia ya majadiliano; na

(iii) Wanasiasa wakuu waweke utaratibu wa kuwapa wananchi mrejesho wa vikao vyao vya ndani ili kuondosha hali ya wasiwasi iliyotanda kuhusiana na hatima ya Zanzibar kisiasa.

Mbali na ANGOZA, asasi nyingine zilizoshiriki kutoa tamko hilo ni Zanzibar Interfaith Centre, Mtandao wa Kidunia wa Dini kwa Watoto (GNRC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Chama cha Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA).

Tamko hilo linaongeza nguvu ya sauti ya asasi za Zanzibar iliyoanza kutolewa na Jumuiya ya Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) mara baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza ufichoni Oktoba 28 kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar.

Tangazo lake limeibua sokomoko kubwa kwa kuonekana limetokana na shinikizo la CCM baada ya kuona kimeshindwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

error: Content is protected !!