June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Asasi za kiraia zaachwa “njia ya panda”

Spread the love

UTOAJI wa elimu kwa mpiga kura kuhusu Katiba Mpya upo “njia panda”. Mpaka sasa haijulikani ni lini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Asasi za Kiraia zitatoa elimu hiyo kwa umma.

Sheria ya Kura ya Maoni inaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa elimu kuhusu katiba inayopendekezwa kwa mpiga kura. Au ikizidiwa inaweza kuzialika Asasi za Kiraia kutoa elimu hiyo.

Kifungu cha tano cha Sheria ya Kura ya Maoni, kinataka elimu kwa mpiga kura itolewe kwa muda wa siku 60. Pia sheria hiyo inataka muda wa siku 30 kuachwa ili kufanyika kwa kamapeni ya kura ya ndiyo au hapana kuhusu katiba inayopendekezwa.

Kwa kuwa Rais alitangaza kura ya maoni kufanyika 30 Aprili mwaka huu, tangazo lililopaswa kutolewa na NEC. Hivyo basi, kwa kuzingatia sheria, ilimu ya mpiga kura ilipaswa kuanza 28 Januari na kumalizika 28 Machi mwaka huu, ili kutoa nafasi ya siku 30 za kupiga kampeni ya ndiyo au hapana.

Aidha, kazi ya kutoa elimu hiyo ni jukumu la NEC, kama NEC iliona haitaweza kutimiza jukumu hilo, basi ingezialika Asasi za kiraia na si kuziomba kutuma maombi katika tangazo lake la 4 Januari mwaka huu.

Mpaka kufikia leo, bado siku 59 ili kura ya maoni ipigwe. Elimu kwa mpiga kura haijatolewa. Asasi za kiraia zilizotuma maombi ili ziruhusiwe na NEC kutoa elimu hazijapewa majibu ya kuruhusiwa kufanya au kutofanya kazi hiyo.

Akizungumza na MwanaHALISI online, mwishoni mwa wiki, Deusi Kimbamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania amesema, NEC imevunja Sheria ya Kura ya Maoni.

“Kitendo cha kuchelewesha Asasi za Kiraia kutoa elimu kwa mpiga kura sio tu kuvunja Sheria bali pia ni kuwakosea haki watanzania ambao wana haki ya kikatiba kupata elimu hii ili waweze kufanya maamuzi sahihi ifikapo tarehe 30 Aprili mwaka huu,” Kimbamba amesema.

“Kwa namna yoyote, NEC haitaweza kutimiza matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni. Elimu kwa mpiga kura inahitaji siku 60. Kampeni ya kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa inahitaji siku 30. Jumla tunahitaji siku 90 kabla ya 30 April. Mpaka kufika leo tumebakiwa na siku 59. Hivyo mchakato umekwama,” Kimbamba amefafanua.

Katika ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Humphrey Polepole, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ameandika mwishoni mwa wiki hii kuwa; “Asasi za Kiraia hazitaweza kabisa kutoa elimu kwa muda uliopangwa na kwa ufanisi katika mazingira haya…

“Ninayasema haya nikiwa na uhakika wa namna mazingira magumu katika kupanga (planning) yanaweza kuathiri ubora wa elimu ya umma ya uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa,” anasema Polepole.

Aidha, kuchelewa kwa NEC kuziruhusu Asasi za Kiraia, kufanya kazi ya kutoa elimu, pia kumechangia asasi hizo kukosa uhakika wa kupata fedha toka kwa wahisani mbalimbali ili kufanikisha zoezi hilo.

“Ni vema mkafahamu kwamba ili taasisi itoe fedha kwa asasi mpya inapaswa kwanza mambo kadhaa yazingatiwe, ikiwemo taasisi itoayo fedha kujiridhisha kwamba asasi inayoomba fedha ina uwezo wa kusimamia kwa uadilifu na kwa malengo husika fedha itakayotolewa” anaandika Polepole.

Aidha, Polepole ameandika kuwa taasisi itoayo fedha pia hupenda kujiridhisha kama taasisi inayoomba imepata kukubalika na mamlaka ya nchi kufanya kazi hiyo.

Hivyo, kulingana na hali ilivyo kwa sasa, hakuna mfadhili ambaye atatoa fedha bila kupata nakala ya kibali kutoka NEC kwenda kwa asasi ya kiraia husika.

“Muda muafaka kwa mfadhili kutoa fedha mpya kwa asasi ya kiraia ambayo ana uhusiano nao huwa si chini ya wiki mbili ukijumlisha uidhinishwaji wa ruzuku, kusaini makubaliano pamoja mchakato wa kibenki,” ameandika Polepole.

Aidha amesema, kama uhusiano huo ni mpya kwa wengine ni miezi mitatu hadi mwaka mmoja, na kama kuna mazingira maalum basi si chini ya mwezi mmoja na hapo ni kama asasi ya kiraia iko vema katika uadilifu wa kimfumo, kiuongozi na taswira yake.

error: Content is protected !!