Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Arcado Ntangazwa afariki dunia
Habari za SiasaTangulizi

Arcado Ntangazwa afariki dunia

Arcado Ntagazwa
Spread the love

 

WAZIRI wa zamani katika serikali za awamu ya Kwanza, Pili na Tatu, Arcado Ntagazwa (75) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amefariki dunia. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam …. (endelea). 

Mwanasiasa huyo nguli nchini, amekutwa na mauti leo alfajiri, tarehe 10 Februari 2021, wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Mloganzila, iliyopo Kibamba, jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, kifo cha Ntagazwa kimetokana na matatizo ya kupumua.”

Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ndani ya chama hicho.

Alikuwa miongoni mwa walioshiriki kikao cha chama hicho kilichofanyika wiki mbili zilizopita, Visiwani Zanzibar.

Ntagazwa alipata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu. Aliwahi kuvuliwa uraia na baadaye kukata rufaa na kushinda kesi.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, aliyepata pia kuwa Mbunge wa Kibondo, mkoani Kigoma, alijiunga na Chadema, Agosti mwaka 2010, baada ya “mizengwe ya kura za maoni za ubunge katika jimbo la Kibondo, mkoani Kigoma.

Ntagazwa ameitumikia serikali ya awamu ya kwanza akiwa Naibu Waziri wa Fedha (1983-85) na baadaye akashika nafasi hiyo kwenye Wizara ya Mawasiliano, Uchukuzi na Ujenzi (1986-87).

Chini ya uongozi wa Ali Hassan Mwinyi alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii (1990-2000) na kuanzia mwaka 2000 alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) hadi mwaka 2005 alipoanguka kwenye ubunge.

Baada ya kujiunga na Chadema, kutokea Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ntagazwa aliteuliwa kugombea ubunge katika jimbo la Muhambwe, mkoani Kigoma.

“Tunashukuru kwa kumpata Ntagazwa ambaye ana uzoefu mkubwa katika serikali. Tunaamini atatusaidia wakati Chadema inapounda serikali yake,” alieleza Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Chadema (Bara), wakati akimpokea Ntagazwa kwenye chama chake.

Kwa sasa, Zitto ni Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo.

Arcado Dennis Ntagazwa, alizaliwa tarehe 4 Desemba 1946 na kuanza kupata elimu yake ya msingi mwaka 1955 hadi 1958, katika shule za msingi Kizazi na Kabangwa, zilizopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Alimaliza masomo yake hayo kwa kuhitimu darasa la nne na hivyo kujiunga na shule ya Seminali ya Ujiji kwa masomo ya darasa la tano na sita mwaka 1959 na 1960.

Baada ya kutoka Ujiji, Ntagazwa alijiunga na Seminari ya Mtakatifu Joseph Kaengesa, iliyopo  Sumbawanga, mkoani Rukwa kwa masomo ya darasa la saba hadi la 12.

Kutoka Kaengesa, Ntagazwa alipata masomo yake ya darasa la 13 na 14 katika shule ya Sekondari ya Saint Francis College – sasa Pugu Sekondari.

Alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa Mkuyu-Handeni, Tanga na Oljoro Arusha kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda, kwa ajili ya mafunzo ya shahada ya sheria.

Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu cha Makerere, Ntagazwa alirejea nchini na kuajiriwa Idara ya Usalama wa taifa. Alifanya kazi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu.

Wakati huo, Idara ya Usalama wa taifa, ilikuwa inaongozwa na Emilio Charles Mzena, ambaye sasa ni marehemu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!