October 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Apigwa risasi akiamulia ugomvi wa mke na mume

Spread the love

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mfanyabiashara Issack Ngowi (29), kwa tuhuma za kumjeruhi kwa risasi Bakari Stambuli (40), aliyekuwa anaamua ugomvi kati yake na mkewe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumapili, tarehe 2 Januari 2022 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kilimanjaro, ACP Simon Marwa Maigwa, akitoa taarifa ya hali ya usalama ya mkoa huo, katika kipindi cha siku kuu ya mwaka mpya.

Taarifa ya Kamanda Maigwa imesema kuwa, tukio hilo lilitokea usiku wa tarehe 31 Desemba mwaka jana, maeneo ya Mjorohoroni, Moshi Manispaa mkoani humo, ambapo mtuhumiwa alimpiga risasi mhanga eneo la bega la mkono wa kushoto.

“Eneo la tukio kumepatikana ganda moja la risasi na bastola, mtuhumiwa anamiliki risasi hiyo kihalali.  Baada ya tukio alikimbia na kuacha silaha,  tayari amekamatwa.Chanzo cha tukio hilo ni mgogoro ulioibuka kati ya mtuhumiwa na mke wake, uliopelekea mhanga kuingilia kati kwa lengo la kuamulia,” imesema taarifa ya Kamanda Maigwa.

Taarifa ya Kamanda Maigwa imesema, mhanga wa tukio hilo ametibiwa katika Hospitali ya Mawezi, mkoani Kilimanjaro na kuruhusiwa, kwa  sasa anaendelea na matibabu akiwa nyumbani.

“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika. Jeshi la Polisi Kilimanjaro linatoa rai kwa wananchi wanaomiliki silaha kihalali,  halitasita kuwanyang’anya wale wote wanaotumia silaha hizo kinyume na taratibu na matakwa ya kisheria,” imesema taarifa ya Kamanda Maigwa.

error: Content is protected !!