May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

ANGUKO SOMO LA HISABATI; Serikali, wazazi wanasikitika, nani achukue hatua?

Spread the love

Kwa zaidi ya miaka kumi sasa somo la hisabati limekua changamoto kwa Taifa hususani kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kwani wastani wa ufaulu wa somo hilo kwa wanafunzi hao ni wa chini sana ukilinganisha na masomo mengine. Anaandika Patricia Kighono – TUDARCo … (endelea)

Vyanzo mbalimbali vinaonesha kuwa ufaulu wa somo hilo haujaweza kuvuka wastani wa asilimia 20 kwa muda wa zaidi ya muongo mmoja ilihali wastani huo unazidi kupungua kila kukicha.

Matokeo ya mwisho ya kidato cha nne ya mwaka 2021 yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) tarehe 15 January, 2022 yameonesha kuwa somo la hisabati ndilo pekee lililo chini ya wastani kwa kupata ufaulu wa asilimia 19.54

Licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika kukuza elimu nchini ikiwemo kujenga madarasa, kuongeza walimu pamoja na vifaa vya kufundishia bado somo la hisabati limekua na dosari kubwa.

UFAULU ULIVYO

Kwa mujibu wa matokeo ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yaliyotangazwa kwa miaka tofauti, ufaulu wa somo hilo umeongezeka kwa asilimia 2.1 pekee kati ya mwaka 2016 hadi 2020.

Hiyo ikiwa na maana kuwa mwaka 2016 ni asilimia 18.02 ya watahiniwa wote ndiyo walifaulu somo hilo kabla ya kuongezeka na kufika asilimia 20.12.

Tofauti na miaka mingine, mwaka 2017 ufaulu wa somo hilo ulikuwa asilimia 19.19, mwaka 2018 ufaulu ulikuwa asilimia 20.02 huku mwaka 2019 ufaulu ukiwa asilimia 20.03.

Aidha, wastani kwa mwaka 2021 umeshuka zaidi katika matokeo ya hivi karibuni baada ya ufaulu kuwa wa asilimia 19.54.

Maswali mengi yameibuka miongoni mwa Watanzania wakijiuliza ni nini hasa chanzo cha ufaulu mdogo wa somo la hisabati.

Kwamba ni uelewa mdogo wa wanafunzi? Au ni walimu wasio na weledi wa ufundishaji wa somo hilo? Ama pengine ni uhaba wa vitendea kazi na mazingira magumu ya kufundishia?

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya elimu wameeleza sababu mbalimbali ambazo zinapesababisha matokeo mabovu kwa somo la hisabati ambapo mmoja wa wataalamu hao ni Mhadhiri wa Kitivo cha Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. George Kahangwa.

Akizungumzia hali hiyo, Dk. Kahangwa anasema kwanza sababu kubwa ambayo uhaba wa walimu.

“Kwa maana ya kwamba idadi ya walimu wa hisabati ndani ya Taifa hili haiendani na idadi ya wanafunzi.

“Kuna upungufu mkubwa wa walimu wa hisabati… tunazifahamu shule nyingi ambazo hazina walimu na zinategemea kuchukua walimu kutoka shule za jirani.

“Kwahiyo hilo ni tatizo ambalo wahusika ambao ni serikali kupitia wizara ya elimu pamoja na TAMISEMI wangedhamiria tokea mwanzo kwamba sasa kwamba tunaajiri walimu wa hisabati wa kutosha, hili tatizo lisingekuwa kubwa kiasi hiki,” anasema.

Anasema hata walimu waliopo wakifuatiliwa kwa makini, wanaweza kuwa sio wenye uwezo wa kutosha kufundisha somo hilo.

Aidha, Dk. Kahangwa anasema walimu watakaoongezwa wapelekwe katika maeneo yote kwa usawa kwa sababu tunapozungumzia uhaba ni kwamba kuna maeneo yananufaika na mengine hali ni mbaya zaidi.

“Lakini pia tuna kazi kubwa ya kubadilisha mtazamo wa jamii, sisi watanzania tulishajiwekea kuwa somo la hisabati ni gumu na hii tumewaambia hata watoto ambao hawajaanza shule.

“Yaani mtoto mdogo anaanza kuusikia wimbi huo kwamba hisabati n somo gumu, kwahiyo wanaenda tayari wakiwa wameathiriwa kisaikolojia ya kwamba somo fulani ni baya,” anasema.

Anasema Taifa linaweza kubadilisha mtazamo huo na kufanikiwa kuonesha kuwa hisabati ni somo rahisi kama masomo mengine.

“Tena wapo watakaodiriki kusema hisabati ni rahisi kuliko masomo mengine, kwahiyo tukifanikiwa kuubadilisha huo mtazamo ukawa mzuri itakua sawasawa na jitihada zinazofanyika kuwaonesha mbinu mbadala walimu namna ya kufundisha somo hilo.

“Katika shule za msingi kungefanyika mpango kabambe katika mikoa yote kuinua somo la hisabatai. Kwa mfano kulikua na mradi unaitwa Equip ambao ulichagua mikoa kumi tu kujaribu kusaidia huo ufundishaji wa hisabati.

“Ingawa hatujui umeishia wapi lakini mikoa kumi haitoshi, kwahiyo miradi kama hiyo ingekua inasambaa nchi nzima tungeweza kuona jitihada hizi zikizaa matunda.,” anasema.

Anasema Serikali inatakiwa kusaidia miradi hii ili kuwe namna rafiki ya ufundishaji wa somo hilo la hisabati.

Anasema haitoshi Baraza la mitihani kutangazia umma kila mara kuwa wanafunzi wamefeli zaidi somo la hisabati huku serikali na wazazi wakisikitika, bali jitihada zianze sasa kuinua ufaulu wake.

“Tunapaswa kuchukua hatua ambazo wataalamu wanazijua hivyo wenye mamlaka wawape wataalamu nafasi ili tuweze kupata nafuu kwa miaka ijayo.

“Umefika wakati sasa kwa serikali kuchukua hatua stahiki katika kuongeza ufanisi wa ufundishaji wa somo la hisabati kwani ndilo msingi wa sayansi na teknolojia ambayo tunahitaji ili kuleta maendeleo ya nchi.

“Vilevile ili kufikia uchumi wa juu tunahitaji wataalamu katika sekta ya uchumi ambao msingi wa taaluma yao ni hesabu,” anasema.

Aidha, mmoja wa walimu waliozungumza na RAIA mwema, anasema wakati mwingine jitihada za walimu kuinua somo hilo hukwamishwa na wanafunzi wenyewe.

“Mwanafunzi kama amejijenga kuwa somo hili ni gumu hata ufanyaje huwezi kumshawishi, baadhi wanabadilika lakini si wote, hivyo tunafanya kazi mbili, mwanafunzi apende hesabu na kuielewa,” anasemaMwalimu huyo aliyejitambulisha kwa jina moja ya Modesta.

Anasema somo hilo linahitaji mwalimu na mwanafunzi wawe watulivu wakati wa ufundishaji na ufundishwaji, ili waelewane vizuri.

error: Content is protected !!