Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Anguko sekta ya utalii: Nape aibana wizara bungeni
Habari za Siasa

Anguko sekta ya utalii: Nape aibana wizara bungeni

Spread the love

 

MBUNGE wa Mtama mkoani Lindi (CCM), Nape Nnauye, ameonya anguko la sekta ya uwindaji wa kitalii, endapo Serikali haitachukua hatua madhubuti, kukabiliana na anguko hilo. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).

Nape ametoa onyo hilo leo Ijumaa, tarehe 4 Juni 2021, akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, bungeni jijini Dodoma.

Mwanasiasa huyo amesema, sekta hiyo ilianza kuanguka tangu 2013, baada ya Serikali kubadili mfumo wa ugawaji vitalu vya uwindaji.

“Kamati wamegusia jambo la sekta ndogo ya uwindaji kitalii, kamati wamekiri sekta hii imetikisika, imeyumba. Takwimu huwa hazidanganyi, ukiangalia namna zinavoonesha liko tatizo na bahati nzuri jambo hili tulianza kuzumgumzia miaka minne iliyopita,” amesema Nape.

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

Nape amesema “ tukatoa mashaka yetu mnakokwenda mtapata matatizo, leo tukiangalia takwimu zinakabiliana na ripoti ya kamati kwamba sekta hii tusipochukua hatua, inakwenda kufa.”

Mbunge huyo wa Mtama amesema, takwimu za kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, zinaonesha Sekta ya Uwindaji wa kitalii imeshuka kutoka vitalu 1,550 mwaka 2013, hadi 473 mwaka 2019.

“Na hapa nipitie takwimu chache , 2013 ilikuwa na wawindaji wa kitalii 1,550, leo ukichukua takwimu z a 2018/2019, wameshuka mpaka wamefika 473, tusipochukua hatua tunakwenda pabaya,” amesema Nape.

Mbali na anguko hilo, Nape amesema, mapato ya Serikali yatokanayo na uwindaji wa kitalii, yameshuka kutoka Dola za Marekani 27 milioni (2013), hadi 8 milioni (2019), pamoja na kampuni za utalii huo kupungua kutoka 60 hadi 40, katika kipindi hicho.

“Katika mapato ya Serikali 2013, ilikuwa inapata mpaka dola 27 milioni, leo tumeshuka hadi dola 8 milioni. Hili anguko kubwa sababu mapato ya jumla ukikusanya na tozo, tulikuwa tunakwenda mpaka dola 100 milioni, leo ni dola 25 milioni, maana yake tunaanguka,” amesema Nape.

Kufuatia anguko hilo, Nape ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, iboreshe mfumo wa ugawaji vitalu vya uwindaji, ili kuvutia kampuni zilizokimbia na wawekezaji wapya.

“Kuna maamuzi Serikali tulifanya, kubadilisha mfumo wa ugawaji vitalu, nia ni njema. Lengo ilikuwa kuondoa rushwa lakini mfumo iliyowekwa ina mapungufu, ndiyo maama vitalu mnapeleka mnadani vinakosa wateja,” amesema Nape.

Mwanasiasa huyo amesema “kapitieni upya mfumo ulioanzishwa, mpunguze matatizo yaliyomo ikiwemo kuongeza uwazi. Hivyo mlivyoweka haitoshi, bado una mapungufu mengi ndiyo maana minada inakwama, minada inafanyika mnapeleka vitalu vingi mnauza vichache.”

Pia, Nape ameishauri Serikali ifanyie kazi ushauri unaotolewa na watu mbalimbali, juu ya namna ya kuboresha sekta ya utalii nchini, ili kukuza mapato ya nchi.

“Nataka kuiomba Serikali ondokeni katika kuona kwamba, kuamua jambo hata kama linafanya vibaya mnatakiwa kuendelea nalo. Nadhani sio sawasawa. Kila mara tunaonyesha takwimu na muelekeo ulivyo, lakini sababu Serikali mmeshaamua mnaendelea hivyohivyo hata kama tunakwenda kuanguka,” amesema Nape na kuongeza:

“Mkiendelea hivi maana yake mnahujumu sekta hii na mkihujumu sekta hii, mnahujumu mapato ya nchi. Kama mapato yameanguka kiasi hiki na bado hatuchukui hatua, liko tataizo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!