August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Anayeiuza CUF ni Maalim Seif au Lipumba?

Maalim Seif na Lipumba

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimeingizwa kwenye mgogoro wa uongozi. Wenye nia mbaya wanasingizia eti Maalim Seif Shariff Hamad anataka kukiuza chama kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Profesa Ibrahim Lipumba, aliyevuliwa uanachama baada ya kuwa mwenyekiti kwa miaka 16, anaeneza fitna hiyo, anaandika Juma Duni Haji.

Profesa ni mtaalam wa uchumi na hesabu; na ndiyo silaha kubwa katika kufanya uchambuzi wa masuala ya kiuchumi akiikosoa serikali ya CCM. Kwa mtu kama mimi na wale tuliosoma naye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tunajitukanisha kukubali hoja hizi kutolewa na profesa.

Sasa nimeelewa kwa nini Babu wa Samunge, Ambilikile Mwasapila, alifanikiwa kuwahadaa Watanzania wakiwemo viongozi wakuu wa serikali, kwa kusema amepata dawa ya kila maradhi kwa kuwanywesha maji ya ‘mti wa ajabu.’ Sishangai vipi wananchi wenye tatizo la ualbino wamekuwa wakiuliwa, kwani baadhi ya watu wanaamini utajiri unapatikana kwa kuwaua albino. Sishangai pia kusikia baadhi ya watu wakikamatwa na kuchunwa ngozi kwa kudhani tu kwamba ngozi hiyo ikifanyiwa matambiko unapata utajiri.

Inasikitisha baada ya zaidi ya miaka 50 ya uhuru Tanganyika, bado watu wamefungwa akili, hawajazinduka, kujitambua wala kujikomboa. Angalia mafanikio ya CUF katika uchaguzi ili kupima kama chama kinauziwa Chadema.

Profesa akiwa ndiye mgombea urais wa CUF uchaguzi wa 2010, alipata kura 695,667; sawa na asilimia 8.28 na Dk. Willibrod Slaa wa Chadema alipata 2,271,491 sawa na asilimia 27.05. Hapakuwa na Ukawa wala vyama kushirikiana.

Mwaka 1995 na 2000 ambako Chadema hawakuweka mgombea urais, CUF ilipata kura 418,973 (1995), asilimia 6.43 na 1,329,077 (2000), sawa na asilimia 16.5. Miaka 10 hiyo tulikosa hoja ya msingi ili kupata kisingizio cha kuwalaumu Wazanzibari au Chadema. Muda wote kisingizio chetu ni dola ya CCM kuhujumu uchaguzi.

Mwaka 2005 CUF ilipata kura 1,327,125; sawa na asilimia 11.68; takriban sawa na 2000. Katika uchaguzi wa 2010 tulifanya vibaya zaidi kwa kushuka hadi kura 695,667; takriban sawa na zile za 1995.

Baada ya miaka 20 ya kushiriki uchaguzi chini ya uongozi wa miaka 15 wa Profesa Lipumba na mara zote akiwa ni mgombea wetu wa urais, tukipata kura chache. Uchaguzi huu wa 2010, pia hatukupata hoja ya kusingizia Wazanzibari kukiuza chama kwa Chadema.

Si mara moja wala mbili Profesa amesikika akisema misikitini kwamba kwa makusudi “waliamua” kumuachia Dk. Jakaya Kikwete wa CCM ili ashinde eti kwa sababu ni Muislam mwenzao wa Tanganyika. Mwisho wa Novemba, Sheikh Khalifa Khamis wa Msikiti wa Kwa Mtoro, Dar es Salaam, alilalamikia uonevu unaofanyiwa Waislamu na vile walivyokuwa wameendelea kukibeba chama hicho kila uchaguzi. Alisema bila wao, CCM ilikuwa ICU, yaani mahututi. Kama si fyokofyoko za Prof. Lipumba si ajabu kingeondoka madarakani 2015.

Badala ya kuuanika ukweli huo, Profesa anasingizia Ukawa ndio umekosesha ushindi CUF; kama vile amesahau alivyoanzisha Ukawa na kutoa jina hilo yeye binafsi tulipokutana kikao cha umoja wa wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, ukumbi wa Msekwa, mjini Dodoma. Ni Profesa akiwa mwenyekiti wa ushirikiano huo, aliyeweka saini makubaliano ya kuweka mgombea mmoja wa urais kwenye uchaguzi wa 2015. Alipojua mgombea hatokuwa yeye, akaanzisha fitna.

Ili aonekane aliyekerwa kwa Bunge Maalum la Katiba kuvurugwa, alitoa hotuba ya kushawishi wabunge wa upinzani watoke kwa msingi kuwa “tukishiriki, tutakuwa tunahalalisha katiba wanayoitaka CCM chini ya kivuli cha Bunge Maalum.”

Profesa Lipumba alipinga mjadala kutawaliwa na ubaguzi wa kidini na kikanda na asili za watu. Aliwafananisha CCM na Intarahamwe wa Rwanda kwa ubaguzi. Anayoyasema leo ni tafauti. Kumbe wakati akisema yale, alikuwa mbuzi aliyevaa ngozi ya kondoo? Kutushawishi kututoa ilikuwa ni agizo la CCM ili wapate nafasi kufanya watakavyo katika kupindua maoni ya wananchi yaliyoratibiwa na Tume ya Jaji Warioba. Nitaeleza mbele, amebadilikaje.

Hoja ya kuuzwa chama anayoitumia kukiua chama, inashangaza. Tulipokwenda mimi na Maalim Seif kumuona nyumbani kwake kabla ya kujiuzulu, alikuwa anakimbilia kwa James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ili wakamilishe mazungumzo ya kumleta Edward Lowassa upinzani. Ni yeye alipendekeza kwetu kuwa Lowassa ajiunge NCCR au Chadema; na “CUF tumuunge mkono.” Tulishawishika baada ya kutupa takwimu alizosema alipewa na “wazee” wa Chadema. “Akija Lowassa tutashinda kwa asilimia 60 au zaidi,” alitwambia.

Leo Profesa anapomlaumu Maalim Seif eti ni kisirani anayetaka kukiuza chama kwa Chadema, anajua anadanganya.

Mwaka 2010, CUF iliweka wagombea 132 wa majimbo Bara, yaliyokuwa na jumla ya kura 6,002,623. Tulipata kura za wabunge 639,402 sawa na asilimia 10.65 ya kura hizo.

Mwaka 2015, tuliweka wagombea 86 tu, mawili ya zamani na 50 tuliyopewa na Ukawa. Ziada ya majimbo 34 ni yale tuliyoweka wenyewe, yakiwemo 25 tuliyopambana na CCM pekee. Tulipata kura jumla 4,398,666 kwa majimbo hayo. Kati yake, CUF tulipata kura 1,112,246 sawa na 25.29.

Kwa majimbo machache chini ya ushirikiano, tumeongeza kura, kuliko majimbo mengine tulipokuwa peke yetu akiwepo Profesa. Wingi huu wa kura kutoka 695,667 hadi 1,112,246 hauwezi kutafsirika kuwa chama kimeuzwa, ukweli umetuongezea ruzuku kwa zaidi ya Sh. 11 milioni kuliko ilivyokuwa 2010 tuliposimama wenyewe.

Siamini na nitakuwa nahitaji kikombe cha Babu wa Samunge, kwamba kupata kura nyingi ni kukiuza chama. Ni hoja dhaifu maana kama chama ni kukiuza, basi alipotuacha wakati tukikaribia uchaguzi, palikuwa pabaya. Alituacha akiwapuuza wazee waliombembeleza. Je, alikiuza au kukiua chama?

Vipi chama kinasemwa kimeuzwa wakati chini ya Ukawa kimeongeza wabunge kutoka wawili Tanzania Bara hadi 10, na kupata madiwani 285 kutoka 152 tukiwa peke yetu, kutwaa Halmashauri tano, Naibu Meya watatu, ushindi tusiowahi kuupata popote tangu 1995 tukiwa naye.

Chini ya Ukawa tumeshinda urais Zanzibar, tumeongeza majimbo Unguja kufikia 10, kutoka mawili, hivyo kuisukuma CCM kwenye kona hadi kutumia majeshi kupindua ushindi fawahisha wa CUF.

Badala ya Profesa kushiriki kuhangaikia kuikamata serikali Zanzibar, radhi yake ni kutambuliwa Dk. Ali Mohamed Shein kuwa rais halali. Suala ni jee kweli Profesa alikuwa mwana-CUF katika maisha yake upinzani? Au aliingia kufanya kazi maalum ya CCM? Kupata majaribu akiwa kiongozi ndio tunamjua sasa. Maslahi yake yameguswa sasa ndio anachukia na kujiuzulu, akipuuzaInaende vilio vya kumsihi asubiri uchaguzi kwisha.

Hulka ya binaadam unaiona pale anaposhika uongozi. Atajidhihirisha alivyo. Sio kwamba amebadilika. Profesa amedhihirisha rangi yake halisi. Alipoachia uenyekiti karibu na kampeni, aliamini CUF itakufa na angetusuta kushindwa uchaguzi. Muungu ametulinda kwa kuzijua nia zetu.

Chama hakikufa. Amerudi akiue. Tangu lini akawa rafiki na Polisi? Walewale waliomvunja mkono Mbagala Zakhem mwaka 2005 na kumdhalilisha Mtoni Kwa Aziz Ali mwaka jana. Anatumia propaganda zilezile za CCM, ikiwemo kulindwa na dola, kugombanisha wana-CUF, bado anasema anakijenga chama.

Matokeo ya uchochezi kwa kulindwa na dola, ukagawa chama pande mbili; hapo unakijenga sio? Kule kukataa kubaki hakukuwa bure. Wapi duniani penye mfano wa kiongozi anayeacha uongozi kwa hiari yake, na akalazimisha kurudi baada ya mwaka mzima kuwa nje ya ofisi? Hutokea kwa aliyetibiwa na Babu wa Samunge.

CUF ilipaswa kusubiri kwa muda gani kuamini Profesa ameacha kiti? Miaka minne, au mitatu, au mwaka kabla ya uchaguzi wa 2020? Ilitarajiwa badala ya kuwa mahakamani tukigombana, CUF tujiimarishe zaidi ili kuongeza mafanikio utakapokuja uchaguzi wa serikali za mitaa. CCM inayochochea, inafurahia tulipo.

Nasihi Watanganyika wajitambue. Wanasafari ndefu ya kujikomboa, akili zao zimefinyangwa kwa miaka 50 kama unga wa chapati, hadi kuamini shida zao ndiyo raha ya maisha yao. Na ufakhari wa kijana wa Tanganyika ni ubabe na matusi, kama walivyo viongozi wa CCM na vijana wao. Badala ya kuona aibu kwa tabia hizo, Profesa nae anaona hiyo ni sifa. Takwimu zinazungumza.

Nimepitia matokeo ya uchaguzi tangu 1995 na kuangalia vipi vyama vya upinzani vilivyofanikiwa. Katika kipindi chote hicho, mafanikio yao wakiwa mmoja mmoja na kwa pamoja hayajafikia asilimia 30 ya ushindi wa CCM.

Uchaguzi wa 2015 tulipojiunga vyama vinne katika mazingira magumu ya mfumo uliopo, tumepata asilimia 40 ya kura za urais, sawa na asilimia 68.3 ya kura za urais za CCM. Ni dalili njema. Pia vyama viwili hivi vimefanikiwa kupata asilimia 44.5 ya viti vya CCM.

Ni takwimu zinazoshawishi kuwa kama tunalenga kuiondoa CCM madarakani, tutalifikia lengo 2020 tukiwa tumeungana, hata pakitumika nguvu gani za dola.

Ndiyo moja ya sababu kubwa za kutumiwa profesa kuua CUF, ili kuua ukawa. Hivyo hashikilii kurudi akajenge CUF, ameridhia kuua kila kitu. Lazima akamilishe kazi kabla ya Oktoba 2020. Profesa wa uchumi amejinadi.

Anazuga watu kutafute mchawi na kumpaka Maalim Seif matope yasiyo mvua. Tangu awali akitumung’unya ndani kwa ndani kama dumuzi kwenye gunia la mahindi. Muda wote dalili zikionesha kwa wepesi wake ndani ya chama.

Amejidhihirisha kwa kupoteza imani ya wanachama. Haitarudi. Nani ataamini kuwa akiongoza tena hatakimbia unapokaribia uchaguzi 2020? CCM si wajinga wa kumjenga kwa matumaini kwamba amuachie serikali ya CCM. Ndoto za alinacha. Profesa akishaua CUF, ataachwa huru, kama walivyoachwa wale waliotumika kabla yake ndani ya CUF.

Mwandishi ni msomaji wa MwanaHALISI, kiongozi mwandamizi CUF aliyefikia ngazi ya makamu mwenyekiti, na mgombea mwenza wa Edward Lowassa katika uchaguzi mkuu uliopita.

simu Na. 0778 028182.

error: Content is protected !!