August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Anayedaiwa kumwita Magufuli bwege apewa dhamana

Spread the love

ISAAC Emily (40) Mkazi wa Arusha anayetuhumiwa kumwita Rais John Magufuli bwege kwenye Ukurasa wa Facebook, amepewa dhamana, anaandika Wolfram Mwalongo.

Emily anatuhumiwa kutenda kosa hilo tarehe 17 Machi mwaka huu kinyume cha sheria ya mitandao namba 16 kifungu namba 14 ya mwaka 2014.

Emily alisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Gaudencia Masanja mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile.

Awali Masanja aliiomba mahakama isitoe dhamana kwa mshitakiwa huyo kwa maeelezo kuwa, usalama wake utakuwa shakani kwani watu wengi wamekerwa na ujumbe huo pia akiwa nje anaweza kuvuruga ushahidi.

Emily hakukubaliana na madai ya Masanja na kusema, ana uhakika hataingilia upelelezi wa kesi hiyo kwa sababu simu zake zote zipo mikononi mwa polisi.

Hakimu Mfawidhi Rwezire leo amesema, mahakama baada ya kupitia hoja mbili zilizotolewa na upande wa mashtaka na mshtakiwa, imeridhia kutoa dhamana kama haki ya msingi ya mshtakiwa.

Dhamana aliyowekea mtuhumiwa huyo ni kuwa na wadhamini wawili waliotakiwa kuwa na jumla ya Sh. 5 milioni kila mmoja.

Mbele ya hakimu Mfawidhi wa Mahakama Masanja alidai kuwa, mtuhumiwa alisambaza ujumbe wa uongo katika mitandao ya kijamii wenye lengo la kumdharau, kumdhihaki na kumtolea maneno Rais Magufuli yenye lengo la kumdhalilisha.

Kwamjibu wa Masanja ujumbe huo ulisomeka “hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi bwana.’’ Hata hivyo mshtakiwa alikana kutenda kosa.

error: Content is protected !!