Thursday , 18 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Ananilea Nkya: Tunasubiri muswada sheria ya habari utinge bungeni
Habari Mchanganyiko

Ananilea Nkya: Tunasubiri muswada sheria ya habari utinge bungeni

Ananilea Nkya
Spread the love

 

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Daktari Ananilea Nkya, amesema wadau wengi wanasubiri Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya 2016, utinge bungeni jijini Dodoma, ili wabaini kama vifungu vilivyolalamikiwa kukandamiza uhuru wa habari, vimeondolewa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Nkya ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 25 Novemba 2022, akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.

Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, kusema mapendekezo ya Serikali pamoja na wadau kuhusu marekebisho hayo, yatafikishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa ajili ya kuandaliwa muswada utakaofikishwa bungeni kupitishwa kuwa sheria.

Dk. Nkya amesema, kwa sasa wadau wa sekta ya habari wanapaswa kuendelea kupiga kelele ili muswada huo upelekwe bungeni huku ukiwa umebeba mapendekezo waliyotoa kwa ajili ya kuondoa vifungu kandamizi, ili vyombo vya habari vifanye kazi kwa uhuru.

“Kwa sasa hatuna jambo kubwa tunaweza sema kuhusu marekebisho hayo mpaka tuone Bunge linapitisha sheria ndiyo tunaweza kusema tuna matumaini gani. Sababu tumeona miaka kadhaa mtu anasema kitu kinakuwa kizuri halafu hakifanyiki,” amesema Nkya na kuongeza:

“Sina matumaini yoyote mpaka nione vifungu kandamizi vimeondolewa kisheria, vimepelekwa bungeni na kupatikana sheria bora itakayowezesha vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kwa sasa tuendelee kushinikiza muswada upelekwe bungeni kwa ajili ya kubadilisha vifungu vyote ambavyo vinalalamikiwa kukwamisha vyombo vya habari kufanya kazi yake inavyotakiwa.”

Hivi karibuni akizungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya habari cha mapitio ya mwisho kuhusu mapendekezo yaliyotolewa juu ya marekebisho ya sheria hiyo, Nape alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ina nia njema ya kurekebisha vifungu kandamizi kwa ajili ya kuimarisha uhuru wa habari.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema Serikali imeonesha nia ya kukubali pendekezo la wadau la kuondoa vifungu vya sheria vinavyofanya makosa ya habari kuwa madai badala ya jinai.

Pia, alisema Serikali imeonesha nia ya kukubali pendekezo la wadau la kuondoa utaratibu wa vyombo vya habari kukata leseni kila mwaka, badala yake vikate leseni kwa kipindi maalum kinachozidi muda wa mwaka mmoja.

Hali kadhalika, Balile alisema Serikali imeahidi wadau kuwa itakwenda kujadili pendekezo lao la kupunguza mamlaka ya Waziri na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), dhidi ya vyombo vya habari katika masuala ya usajili, utoaji maudhui na ugawaji matangazo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari Mchanganyiko

Mume auwa mke kwa kumchoma visu, ajisalimisha Polisi

Spread the loveJACKSON Kalamji (49), anashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mwanza,...

Habari Mchanganyiko

Serikali yatoa ajira watumishi 46,000, yatangaza utaratibu mpya kuajiri

Spread the loveSERIKALI imetangaza nafasi za ajira za watumishi wa umma 46,000...

error: Content is protected !!