Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Amani Karume: Asimulia Mapinduzi ya Zanzibar na kusema: Mzee Karume alikuwepo Zanzibar usiku wa Mapinduzi 
Makala & Uchambuzi

Amani Karume: Asimulia Mapinduzi ya Zanzibar na kusema: Mzee Karume alikuwepo Zanzibar usiku wa Mapinduzi 

Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love
MTOTO wa kwanza wa mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Sheikh Abeid Aman Karume amesema, baba yake, alikuwapo Zanzibar, usiku wa kuamkia siku ya Mapinduzi, Januari 12, mwaka 1964. Anaripoti Livingstone Luhere, Zanzibar….(endelea).

Dk. Aman Abeid Karume, aliyekuja kuwa rais wa sita wa Zanzibar, anaeleza kuwa kinyume na inavyoelezwa na baadhi ya watu, kuwa Sheikh Karume, hakuwapo Zanzibar siku ya Mapinduzi, ukweli ni kwamba mzazi wake huyo, alikuwapo Zanzibar na alishiriki Mapinduzi.

Anasema, “Mzee Karume, alishiriki Mapinduzi. Nakumbuka hilo vizuri, kwa kuwa mimi nimezaliwa mwaka 1948 na wakati Mapinduzi yanatokea, nilikuwapo Zanzibar.”

Rais Karume ametoa ufafanuzi huo, katika mahojiano yake na Raia Mwema, yaliyofanyika ofisini kwake, Unguja, hivi karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine, anaeleza alivyoshuhudia mapinduzi hayo na ushiriki wa baba yake katika tukio hilo la kihistoria.

Anasema, “alfajiri ya siku ya Mapinduzi, nilizisikia bunduki zikirindima kutokea sehemu za Ziwani, wakati tukiwa tumelala. Nilikuwa mimi, mama pamoja na mdogo wangu. Tulikuwa pale Kisima Majongoo, ambako tulikuwa tukiishi kwenye moja ya nyumba ya Mzee Karume.”

“Mimi mawazo yangu ya kwanza, ni kwamba milio hiyo ya risasi, inaashiria kuwa waanza kupiga kunguru, kwa kuwa kulikuwa na zoezi la aina hiyo. Nikasema, hawa wanapiga kunguru mbona mapema mno? Nilipochungulia dirishani, nikaona kuna kiza kinene. Niikajiuliza, hawa watawaona vipi kunguru na kiza hiki?

“Mara Mzee (Abeid Karume) huyo akagonga mlango. Akasema, amkeni, vaeni nguo sasa hivi. Tukamuuliza, kuna nini saa hizi? Akasema, “tayari sisi tumeshaanza vita, tunakomboa nchi yetu. Hiyo ilikuwa majira ya saa 10 alfajiri.

“Tukavaa suruali zetu, tukakaa pale, sasa kutajwa vita tukaona kazi ipo. Basi akatuambia sasa nyie msikae hapo ondoke, akatuchukua akatupeleka nyumba ya jirani.”

Alipoulizwa waliondokaje kwenye nyumba hiyo na kwenda kujihifadhi kwa jirani, wakati risasi zilikuwa bado zinarindima, Rais Karume anaeleza, “tuliondoka kupitia mlango wa nyuma kwa kuwa nyumba yetu ilikuwa na milango mitatu, mlango wa mbele, jikoni na mlango wa nyuma.

“Tuliondoka bila kuhoji kwa kuwa saa hizo unafuata maelekezo, amri moja. Tulielekea nyumbani kwa Mzee Ramadhani Mfua; tulikuwa mimi, mama na mdogo wangu. Baba akatupeleka kwa Mzee Ramadhani na akatuacha hapo. Yeye akarejea nyumbani.”

Alipoulizwa kuwa aliposikia risasi zinarindima na kuelezwa na baba yao kuwa waondoke katika eneo hilo, kwamba hawakuwa na hofu, Dk. Karume alijibu: “Alaah, sasa wewe bunduki zinapigwa kama hivyo, usiwe na hofu?

“Ni lazima uwe na hofu, kwa sababu Mzee katuambia tumeshaanzisha vita, tunapigana kuikomboa nchi yetu, na unajua kwenye vita kuna kushinda na kushindwa.”

Anasema, “tukakaa pale, nikamsikia Mzee akisema, kaeni hapa mimi narudi kule. Mzee akasema, kaeni hapa, mimi narudi kule. Mzee Ramadhani akasema, mimi Mzee siwezi kukuacha peke yako, naondoka na wewe. Akafuatana naye wakarudi nyumbani; sisi tukabaki nyumbani kwake na mke wake na watoto wake wadogo.

“Sasa hapo ndipo nilipoona mambo palipopambazuka, mara Mzee Ramadhani akarudi. Akaja kutupa taarifa kwamba zimekuja gari za watu ambao yeye hawafahamu, kuja kuripoti kwa mzee tena wamekuja kiume na bunduki na wamekuja na gari za polisi na kuzungumza na Mzee kuwa kazi wamemaliza.

“Wameshachukua Ziwani Polisi Station na Mtoni, ilikua vituo viwili. Mzee akawaambia chukueni silaha zote pelekeni Raha Leo ndio itakuwa head quater (makao makuu) zetu. Ndio ilivyokuwa, sasa akaja kutuambia wanangu tumeshinda, haya turudi kule.

“Kulipopambazuka, mara nikamuona jamaa mmoja akifuatana na mwenzie wamevaa kiraia, akiwa na mkoba na bunduki ya serikali, mwenzie amebeba panga wanapita, sijui wanakwenda wapi. Palepale nikajua hii kweli…kama raia wamepata bunduki kama hivi, nikajua tayari vita tumeshashinda.

“Hao watu wawili waliobeba silaha, wakiwa wamevalia kirai, walitia rangi nyeusi nyuso zao,” anasimulia.

Anaongeza: “Baadaye tena, akarudi Mzee Ramadhani akatuambia, sasa amekuja jamaa kumchukua Mzee wamekwenda Radio Station ya Rahaleo.

“Tukakaa pale mpaka ilipofika saa nne, ndio mzee akaja akatuchukua tukarudi nyumbani. Akasema, basi tumemaliza kila kitu, twendeni nyumbani. Akatuambia kwa sababu ninyi mnasafiri, basi twendeni, kwa kuwa tulikuwa na safari ya kwenda Dar es Salaam.

“Tukaingia ndani ya gari yetu na gari moja aliendesha jamaa mmoja wa Zanzibar anaitwa Selemani Kambangwa, tukaanza safari kuelekea Fumba. Njiani tukakuta watu fulani, wakatuambia njia hii msipite, kwa sababu kuna kituo kimoja kule gerezani Kilimani kilikuwa bado hakijachukuliwa.”

Akimnukuu mmoja wa wasamalia wema huyo, Dk. Amani anasema, “alimueleza Mzee huku hatujachukua bado na kuna mzungu anapiga risasi kama hana akili vizuri; na Yusuph Himid tayari amepigwa risasi.

Mzee akashtuka sana, na kuhoji “…eeeh yu hai? Wakamwambia alipigwa risasi ya mkono, lakini alishapelekwa hospitali.  Basi tukapita njia ya Ziwani hii ilikuwa ya mkato, mpaka njia ya Jang’ombe na Jang’ombe, lilikuwa jimbo lake.”

Anasema, walipofika mbele wakasimama ili kubadilisha gari, ambapo waliacha gari waliokuwa wakilitumia na kuondoka na gari ya Kambangwa, huku nyingine ikiwafuata kwa nyuma, moja kwa moja mpaka Fumba.

“Tulipofika Fumba, tukaingia kwenye ngalawa. Mzee akauliza, Jimy Miringo, yuko wapi? Tukaingia na sisi tukaanza safari ya kwenda Dar es Salaam. Tulitumia ngalawa ambayo inatumia Tanga. Safari yetu ilianza saa mchana.

“Safari ilikuwa ndefu, tulikuwa na njaa pia, hatujanywa chai, zamani ilikuwa tofauti kidogo, mitaani kule asubuhi unakwenda kununua mikate kwa jirani lakini zama zile hakuna mkate.

“Tumetoka na njaa, tumeshinda kutwa baharini, kwa hivyo pale bahari ilikuwa shwari tukaanza kupiga makasia, tukafika kijiji kimoja kule  kiilikuwa kinaitwa Mbweni, Dar es Salaam, ambako kulikuwa kuna station (kituo) moja ya uvuvi. Nakumbuka tumeshuka pale, jamaa wametuona kama wavuvi. Mzee akauliza, kuna mtu ana gari hapa?

“Akajibiwa kwamba iko gari moja tu ya mkuu wa kituo cha uvuvi. Tukaenda mpaka nyumbani kwake, karibu na pwani. Kufika pale, Mzee akajitambulisha, jamaa akamwambia Mzee karibu, nikusaidie nini?

“Mzee akamwambia unaweza kutupeleka nyumbani kwa Rashid Kawawa mjini Dar es Salaam? Akasema, nitakupelekeni sasa hivi. Akatutia ndani ya gari lake na kijana mmoja ambaye alikuwa kama mlinzi wake, tukaenda mpaka kwa Mzee Kawawa, walinzi wakatuzuia kwenye geti, saa hizo ilikuwa magharibi tena kiza kilikuwa kinaingia.

“Basi mzee akawaambia walinzi mwambie Rashidi Kawawa, kwamba Abeid Karume yuko hapa. Mara tukamuona Mzee Kawawa anakuja mbio, anawaambia walinzi mfungulieni mzee mlango. Tukafunguliwa, tukapita akatupokea.

“Tukasalimiana tukapanda juu, ni pale karibu na Ikulu. Mzee Kawawa akamwambia mzee, haya karibuni hapa subirini sasa hivi nimpigie Mwalimu (Nyerere), akampigia. Mwalimu akasema, nakuja. Akaja palepale.

“Kabla Mwalimu hajaja, Mzee akamwambia Mzee Kawawa kwamba hawa vijana wana njaa, hebu watengenezeeni chai kidogo, na tulikuwa na njaa kweli kweli. Tukatenegenzewa chai ilikuwa na sandwich. Mara Mwalimu akaja, wakaanza kuzungumza.

“Ilikuwa mara ya kwanza kula sandwich, nikaanza kuuliza hiki nini baba? Mzee akatuambia nyie acheni ushamba, hii inaitwa sandwich kuleni tu ni nzuri.

“Mwalimu tulishawahi kukutana naye Zanzibar, na aliwahi kufikia kwenye nyumba yetu, sisi tulikuwa na nyumba nne, mzee wetu alikuwa landroad pale alikuwa anawekeza kwenye nyumba, ananunua nyumba mbovu anaitengeneza, kisha anakodisha.

Alioulizwa kipi walikiongea kati ya Mwalimu Nyerere na Mzee Karume, Dk. Aman anasema, “Baba alimwambia Mwalimu tayari sisi tumeshachukua nchi yetu. Yule Sultani tulishamtoa kule, Mwalimu akamwambia sawa.

“Nakumbuka mzee akamwambia Mwalimu, mjulishe Jomo Kenyatta, kwamba tumefanya sisi wenyewe kitu kama hivyo, akasema nitampa taarifa sasa hivi.

“Sababu mwaka 1961 Waingereza walileta askari hapa kutoka Kenya, hawakuamini askari wa Tanganyika, walisema askari wa Tanganyika wanajuana hao, tukiwaleta hapa itakuwa mashaka kidogo, wakaleta Wakenya.

“Sasa baada ya hapo wakawaleta pia askari kutoka Uingereza, kwa hivyo mzee akaogopa akasema, Kenyatta  asije akaleta hapa askari wake wakaja kutuvuruga. Hilo ndilo lililotokea.

“Tulipomaliza kunywa chai, Mzee akasema hawa nimewaleta wana safari kwenda Malawi shuleni, passport zao hizi wanazo. Nishawakabidhi hapa tiketi zao kila kitu, sasa hawa ikifika siku ya kwenda kule watayarishieni safari waende.

“Mwalimu akasema, basi vizuri. Hawa nitawachukua watakaa state house (Ikulu) na wenzao. Kina Makongoro (Makongoro Nyerere), walikuwa wadogo zangu sio wakubwa. Mzee akasema, hapana usiwaweke hapa. Wapeleke Magomeni kwa rafiki yangu pale mzee mmoja aliitwa Shaban Ferooz, alifanya kazi kampuni ya uchapishaji, asili yake ni mtu wa Zanzibar.

“Walikuwa marafiki sana na mzee, sasa wapeleke kule Magomeni Makuti, kule kwenye nyumba za kota maeneo ya Polisi Station.  Tulikopelekwa kule kumbe ilikuwa kheri yetu.

“Baada ya pale, nikamsikia mzee akimuuliza Mwalimu, kina Kasim Hanga na Abdulrahman Babu, wako wapi? Mwalimu akasema, tumewaweka Palm Beach hotel, Mzee akamwambia, unaweza kunikusanyia sasa hivi nataka kuondoka nao kurudi nao Zanzibar,” anaeleza.

Dk. Amani anasema, watu wengi hawajui histori hiyo. “Mwalimu akamwambia kwa nini hulali kesho asubuhi tutakutengenezea ndege utarudi? Mzee akamwambia, mimi sea man (baharia) nitachukua boti tu hapa, yuko rafiki yangu mmoja Muisrael akivua anaitwa Misha, mwambieni Misha anitayarishie boti nitawachukua hawa (Hanga na Babu) nitarudi nao.

“Akatayarishiwa boti, sisi tukatiwa ndani ya gari tukaenda Magomeni, yaliyotokea huko nyuma hatuyajui. Sasa usiku uleule mzee akaingia ndani ya boti na kina Babu na Hanga akaja nao hapa wakateremkia Kizimkazi.

“Sasa kuna watu wengi wanaharibu stori hiyo wanasema, Mzee siku ya Mapinduzi hakuwepo, siyo kweli. Mzee alikuwapo, kisha ndio akaenda Dar es Salaam na alirejea kupitia Kizimkazi siku ya tarehe 13 Januari.

Tulivyokwenda Magomeni, baadaye kidogo ikatokea purukushani ya jeshi ya mwaka 1964. Mimi nilikuwa Dar es Salaam na dhahama yote hiyo nimo, sasa fikiria tungekuwa Ikulu si ingekuwa balaa?

Alipoulizwa kwanini Hanga na Babu hawakuwapo Dar es Salaam, Karume amesema, “waliogopa kukamatwa.”

Ameongeza: “Babu alikimbia kukamatwa kwa sababu serikali ya ZMP walilifunga gazeti lake, lililokuwa likiitwa The News. Wakafunga na chama chake cha Umma Party na kisha naye wakataka kumkamata.

“Lakini askari waliopewa kazi hiyo, wakawamwambia watu wa ASP, kwamba jamani tunakwenda kumshika yule, ndipo wakamkimbiza kumpeleka Dar es Salaam. Huo ndio ukweli wenyewe. Anayetaka kupinga aje ashindane na mimi kwa kuwa nilikuwapo.

Akizungumzia kama Mzee Karume alijua kutatokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi kwa upande wa Tanganyika, Dk. Aman anasema, “hapana. Hakujua.”

Anahoji: “Aatajuaje? Lakini ndio hivyo tena, unajua wazee wa zamani walikuwa wameshibana wale, Mzee Ferooz angesikia watoto wako hapo na yeye yuko mjini angetaharuki. Angesema, sasa mimi yule ndugu yangu, imekuaje tena. Ule ndio ulikuwa wokozi wetu.

“Na wale vijana wakaja palepale nyumbani kwetu, sababu nyumba ya pili au ya tatu kulikuwa na jamaa mmoja akiitwa Simba. Walikuja kumtafuta. Sisi tulikuwa hatujui, lakini Mzee Ferooz akasema tukubaliane, mkiulizwa semeni hamumjui.

“Wakaja wakatuuliza, sisi tulikuwa wageni na kiswahili chetu wakajua kwamba hawa wametoka Unguja. Ilikuja Landrover moja na askari watatu wakashuka kumtafuta Simba. Hayo tumeyaona, tulikuwepo hapo. Inshaalah siku moja nitaandika historia hiyo katika kitabu.

Dk. Aman Karume, ambaye sehemu ya elimu yake, aliipata nchini Malawi anaeleza kuwa alifika huko, kutokana na uhusiano mzuri wa kirafiki na kindugu, unaotokana na harakati za kisiasa na kuwa pamoja kwa muda mrefu, kati ya baba yake mzazi na aliyepata kuwa rais wa Malawi, Dk. Hasting Kamuzu Banda.

Anasema, hakuna uhusiano mwingine wowote uliokuwapo kati ya viongozi hao wawili.

Anasema, “mahusiano kati ya Mzee Karume na Dk. Banda, yalianzia mbali sana. Banda aliishi Uingereza na  Jomo Kenyatta kaishi huko pia, Mzee pia aliishi Uingereza wakati wa shughuli zake za kikazi. Sasa walionana huko wakajuana, lakini usisahau kwamba vuguvugu za kuikomboa nchi za Afrika lilikuwa limeanza.

Makala haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la kila wiki la Raia Mwema la Jumatano iliyopita, tarehe 13 Januari 2021 – Mhariri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Ruth Zaipuna: Sekta ya kibenki imeimarika maradufu miaka miwili ya Dk. Samia

Spread the loveTarehe 19 ya mwezi Machi, ni siku muhimu sana kwa...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Miaka miwili ya Rais Samia, TMA yaimarika, yatoa utabiri kwa usahihi

Spread the loveMACHI 19, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan anatamiza miaka miwili...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Zanzibar inahitaji sheria kumaliza udhalilishaji na ukatili wa kijinsia

Spread the love  DAKTARI Sikujua Omar Hamdan anaamini Zanzibar inahitaji “sheria za...

Makala & Uchambuzi

Uthubutu, uwezeshaji kielimu unavyopaisha wanawake GGML

Spread the loveMTU anapojitambulisha kuwa anafanya kazi mgodini, watu wengi hudhani kuwa...

error: Content is protected !!