Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wakili Alute: Hakuna kikwazo Lissu kugombea urais akiwa ughaibuni
Habari za SiasaTangulizi

Wakili Alute: Hakuna kikwazo Lissu kugombea urais akiwa ughaibuni

Alute Mungwai
Spread the love

TUNDU Antipas Lissu, makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aweza kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, “hata kama bado yuko ughaibuni.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Alute Mughwai, kaka wa mwanasiasa huyo machachari nchini amesema, Lissu aweza kugombea urais kupitia Chadema, hata kama hajarejea nchini.

Mughwai ambaye ni wakili wa mahakama kuu, ametoa ufafanuzi huo jana Jumapili, 28 Juni 2020, kufuatia moja ya magazeti ya kila siku nchini Tanzania, kuelezea utata uliyogubika nafasi ya Lissu kupenya katika katika kinyang’anyiro hicho.

Katika andishi lake alilolisambaza kupitia  mitandao ya kijamii, Alute – mmoja wa wanasheria wenye weledi mkubwa nchini – anasema, “suala la Lissu kugombea urais, wakati akiwa nje ya nchi yake, halina shida yoyote kisheria.”

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Amesema, “kwa mujibu wa Kanuni ya 26 ya Kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge na madiwani za mwaka 2015, kama zilivyochapishwa kwenye tangazo la Serikali Na. 307 la mwaka 2015, fomu za uteuzi kwa mgombea urais au ubunge, zinaweza kuchukuliwa na mgombea mwenyewe au na mpiga kura kwa niaba yake.”

Ameongeza, “kwa hiyo, suala la uchukuaji fomu ya uteuzi halina utata hata kidogo.”

Lissu, ni miongoni mwa wanachama 11 wa Chadema waliotia nia ya kuomba ridhaa ya kupitishwa na chama hicho, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Utata ulioelezwa na gazeti hilo, umetokana na hatua ya Lissu kuwa nje ya nchi na michakato hiyo ya urais inafanyika nchini, jambo ambalo linamuweka katika mazingira magumu yeye kuteuliwa na Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), kugombea nafasi hiyo.

          Soma zaidi:-

Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu 7 Septemba 2017, aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma. Alikuwa akirejea nyumbani, kutokea kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Wakati huo, Lissu alikuwa mbunge wa Chadema katika jimbo la Singinda Mshariki.

Mara baada ya shambulio hilo ambalo lilimjeruhi vibaya mwanasiasa huyo ambaye wakati huo, alikuwa pia Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisafirishwa hadi nchini Kenya kwa matibabu zaidi.

Lissu alipata matibabu yake katika hospitali ya Nairobi kuanzia tarehe 7 Septemba 2017 hadi tarehe 6 Januari 2018, alipohamishiwa nchini Ubelgiji.

Dk. Maryrose Majinge, kada wa Chadema aliyetangaza nia ya kuwania Urais kupitia chama hicho

Tangu wakati huo, hajaweza kurejea nyumbani, pamoja na kuelezwa na madaktari wake, kwamba amemaliza matibabu yake.

Taarifa zinasema, Lissu ameshindwa kurejea nyumbani Tanzania, kutokana na kuhofia usalama wake. Mara kadhaa, amekuwa akitoa wito kwa serikali, kumhakikishia usalama wake.

Hata hivyo, pamoja na kuwa ughaibuni, Lissu aliweza shiriki uchaguzi mkuu wa ndani ya chama chake, Desemba mwaka jana, ambapo alichaguliwa kwa kura nyingi kuwa makamu mwenyekiti.

Aliomba kura kwa wajumbe wa mkutano huo kwa njia ya ‘video call’ na amekuwa akishiriki baadhi ya vikao vya chama hicho, kwa njia hiyo.

Hata alipotangaza kutia nia ya kugombea urais kupitia chama hicho kikuu cha upinzania nchini Tanzania, Lissu alitoa hotuba yake na kurushwa moja kwa moja na mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa Alute, changamoto itakayoweza kujitokeza, “ni endapo Lissu atakuwa ameteuliwa na chama chake kugombea urais na baada ya kuteuliwa akashindwa kurudi nyumbani.”

Anasema, “kuna mambo mengi atakayopaswa kuyafanya yeye mwenyewe kuanzia tarehe ya uteuzi wa chama chake na tarehe ya uteuzi wa NEC.”

Lazaro Nyalandu

Akizungumzia suala la usalama wake, Alute anasema, katibu mkuu wa Chadema ameripotiwa akilalamika kuwa mkuu wa jeshi la polisi (IGP), kutaka hakikisho la usalama wa Lissu pindi atakaporejea nchini, lakini mpaka sasa hawajajibiwa barua walizoziwasilisha.

Kama ni hivyo, Alute anasema, uongozi wa Chadema unapaswa kufuatilia majibu ya barua hizo kwa kwenda kumwona mkuu huyo wa jeshi la polisi ana kwa ana.

Anasema, “katika mazingira yaliyopo mawasiliano ya barua pekeyake yanaweza yasitoshe.”

Kuhusu haki ya Lissu ya kupatiwa ulinzi, Alute anasema, sheria iko wazi, kwamba ni jukumu la Jeshi la Polisi kulinda usalama wa raia na mali zao nchini.

“Lissu ni mmoja wa raia hao wanaopaswa kulindwa usalama wao, hasa ikizingatiwa kuwa lilifanyika jaribio la kumuua mnamo tarehe 7 Septemba 2017,” anaeleza.

Anasema, “kwa mujibu wa kfungu cha 29 cha Sheria ya gharama za uchaguzi No. 6 ya 2010, ni wajibu wa Jeshi la Polisi kutoa ulinzi na usalama wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea.

“Mahali ambapo mchakato huo unafanywa na chama cha kisiasa kitakachoshiriki kwenye uchaguzi husika.”

Kwa wagombea urais, Alute anasema, “maana yake ni kuwa wagombea urais wote, kuanzia tarehe ya mchakato wa uteuzi wa wagombea hao ndani ya vyama, kabla na baada ya uteuzi wa wagombea na tume ya uchaguzi watakuwa na haki ya kulindwa usalama wao na jeshi la Polisi.”

Anasema, “hoja hiyo inaungwa mkono na tafsiri ya maneno “mgombea” (Candidate), “mchakato wa uteuzi” (Nomination Process) na “uchaguzi” (Election) kwenye Sheria tajwa hapo juu.”

Anasema, “neno Mgombea ni mtu aliyejitokeza kwa ajili ya kuchaguliwa nafasi ya Rais. Kwamba, watia nia wote wa urais wanaingia humo. Na neno uchaguzi, limetafsiriwa ni pamoja na mchakato wa uteuzi.

“Na maneno mchakato wa uteuzi yametafsiriwa ni utaratibu ambapo chama cha kisiasa kinawakaribisha watu wanaopenda kupendekezwa na chama hicho kusimama kama wagombea kwenye  uchaguzi.

Alute anasema, “natumaini kuwa ufafanuzi huo wa kisheria utaweza kuondoa hicho kinachoitwa utata.”

Baadhi ya watia nia wengine wa urais ndani ya Chadema, ni Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Maryrose Majinge ambaye ni mwanamke pekee kwenye mbio hizo na mwenyeviti wa Chadema, Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu.

Wengine katika orodha hiyo, ni mbunge wa Iringa Mjini na mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mchungaji Peter Msigwa; aliyekuwa meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!