August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Aliyoyasema Lipumba mbele ya wafuasi wake

Spread the love

BAADA ya kuingia Ofisi Kuu za Chama cha Wananchi (CUF), Buguruni jijini Dar es Salaam, mchana wa leo Profesa Ibrahim Lipumba amezungumza mambo mbalimbali kuhusiana na kurejeshwa kwake na Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama Vya siasa hapa nchini, anaandika Charles William.

Prof. Lipumba alikuwa mwenyekiti wa CUF kabla ya kuandika barua ya kujiuzulu tarehe 05 Agosti mwaka jana, lakini tarehe 08 Juni mwaka huu aliandika barua ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na kuzua mvutano ndani ya chama hicho.

Mapema baada ya kupata barua ya Jaji Mutungi inayoeleza kumtambua kama mwenyekiti halali wa CUF Lipumba aliwasili Ofisi Kuu za chama hicho na kusema yupo tayari kukitumikia tena chama hicho.

“Nimerejea tena na nitafanya kazi kwa ari, sikukutana na Maalim Seif barabarani. Nimekutana naye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1973. Tena tulikutana  msikitini,” amesema.

Akizungumza kuhusu kuomba kurejea baada ya kujiuzulu, Prof. Lipumba amesema, “wazee na viongozi wa dini waliniomba nirejee, nikawasikiliza, nikawambia nitarejea ila wazungumze kwanza na Katibu Mkuu. Wakaenda kwa Maalim, akawajibu; hana tatizo na mimi, wazee wakaniambia Maalim hana tatizo na wewe.”

Prof. Lipumba amesema, aliandika barua ya kurejea tarehe 08 Juni mwaka huu, akimtaarifu Maalim Seif kuwa, angeanza kazi ya uwenyekiti tarehe 10 Juni, na kwamba kazi yake ya kwanza ingekuwa kuchambua bajeti ya nchi.

“Tarehe 09/06 Katibu mkuuu akaniambia nisianze kwanza kazi mpaka ashauriane na wanasheria. Nikamjibu kuwa nazingatia ushauri wake lakini hakuna utata wa kisheria kwasababu Katiba inasema wazi kuwa, kujiuzulu ni mpaka ithibitishwe na mamlaka iliyokuchagua.

Baadaye nikasikia akisema kuwa maamuzi ya chama yatafanywa kwenye vikao. Kiukweli hata mimi sikupenda tufikie tulipofika. Hata hivyo kwa kuwa msajili katoa maelekezo ambayo ni lazima yafuatwe naomba sasa tusahau yaliyopita na tugange yajayo,” ameeleza.

Lipumba amesema anataka kujenga mtandao wa chama hicho ili chama kienee nchi nzima na kusisitiza kuwa atafanya kazi na viongozi wote waliochaguliwa kihalali lakini siyo wale walioteuliwa 28 Agosti mwaka huu na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.

“Katika mvutano huu, hakuna aliyeshinda. Iliyoshinda ni Katiba ya CUF na sisi lazima tukubaliane na ukweli huu. Ni aibu kwa chama cha haki sawa kwa wote kufanya mambo bila kuzingatia demokrasia,” amesema.

Lipumba pia ameeleza masikitiko yake kwa chama cha CUF kutoka kuwafukuza wabunge wa kuchaguliwa Magdalena Sakaya (Kaliua) na Maftah Nachuma (Mtwara).

“Haiwezekani ufukuze wabunge. Sakaya ni mwanamke pekee wa CUF aliyeshinda jimbo kwa upande wa Bara, jimbo lake la Kaliua ni kubwa kuliko hata Zanzibar lakini alipambana na kushinda, leo tunamfukuza ili tumpoteze kirahisi? Huyu ni kipenzi cha wananchi wa Kaliua.

Unamfukuza Maftah? Ukizungumzia watu ngangari kinoma ndani ya CUF huwezi kuacha kumtaja Maftah, alisimama katika uchaguzi mkuu mwaka jana na NCCR, Chadema na CCM lakini akawagaragaza, leo tunamfukuza. Tutaingiaje Kusini? Tutaingiaje Mtwara?” ameng’aka.

Lipumba amesema alisikitishwa na wanachama waliokuwa wakimshambulia kwa nyakati tofauti akiwemo Julius Mtatiro na Hamidu Bobali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi.

“Bobali anaendesha vikao vya kumfukuza Maftah na kunibeza mimi, huyu ni kijana niliyemlea na kumpeleka Ulaya mwaka 2014 lakini amekengeuka. Mtatiro nimemteua mimi kuwa Naibu Katibu Mkuu na baadaye Mjumbe wa mkutano mkuu lakini alikuwa akinishambulia, jambo hili linasikitisha sana,” amesema.

Prof. Lipumba amewataka viongozi wote waliowekwa madarakani na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho mwezi mmoja uliopita kukaa kando vinginevyo watajikuta wakifikishwa katika vyombo vya sheria.

“Msajili ameweka msisitizo kuwa mtu yoyote asijifanye kiongozi wakati si kionggozi vinginevyo atatozwa faini milioni moja au kufungwa miezi sita au vyote kwa pamoja.

Wakati CCM na Magufuli wakisema Hapa Kazi Tu sisi lazima tusimame katika falsafa ya Hapa Haki Tu,” Amehitimisha Prof. Lipumba.

error: Content is protected !!