September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Aliyetumbuliwa na Rais Magufuli afariki

Spread the love

WILSON Kabwe, aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam amefariki dunia usiku wa kumakia leo jijini Dar es Salaam, anaandika Pendo Omary.

Kabwe amefikwa na mauti akiwa kwenye matibabu na taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Isaya Mwita, Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa, Kabwe amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Mama Tuangoma, Mwenge ambapo Mwanahalisi Online halijathibitisha kama amefia hapo.

Mtandao huu unaendelea kufuatilia ili kujiridhisha na chanzo cha kifo chake, hospitali aliyofia na mazishi yake.

Kabwe alisimamishwa kazi na Rais John Magufuli tarehe 19 Aprili mwaka huu wakati wa ufunguzi wa Daraja la Mwalim Nyerere (Kigamboni) baada ya Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kumchongea kwa rais huyo.

Kabwe alisimamishwa kazi kwa madai ya ufisadi katika utekelezaji wa mikataba inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato katika Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani (Ubungo Terminal) na kodi ya uegeshaji magari katika Jiji la Dar es Salaam hivyo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. 3 Bilioni.

Hata hivyo, Stali ya Rais Magufuli kutimua watumishi wa umma kwa ‘munkari’ imekuwa ikiwavuruga wanasiasa, wanaharakati pamoja na viongozi wa dini nchini.

Miongoni mwao ni Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Wengine ni Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu Mkuu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislam Tanzania na Helen Kijo Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Wote hao wamekuwa wakimtaka Rais Magufuli kufuata sheria za utumishi wa umma katika kuwawajibisha watumishi wanaotuhumiwa kufanya makosa.

error: Content is protected !!