Sunday , 5 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Aliyeshindwa ubunge Mkuranga, arudi kushukuru
Habari za SiasaTangulizi

Aliyeshindwa ubunge Mkuranga, arudi kushukuru

Spread the love

ALIYEKUWA mgombea Ubunge wa Mkuranga (ACT-Wazalendo), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Mohamed Mtambo, amerejea jimboni kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano waliompa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Katika uchaguzi huo uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, Mhandisi Mtambo alishindwa huku Abdallah Ulega wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akitangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Jumapili ya tarehe 29 Agosti 2021, Mhandisi Mtambo alikwenda kuwatembelea wazee wa Kata ya Tambani na kuwapa zawadi mbalimbali ambapo pamoja na kuzungumza nao, walimweleza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo daraja linalounganisha eneo la Churwi na Charambe.

“Nilipita hapa mwaka jana kuwaomba ridhaa ili niwatumikie kama mbunge wa Mkuranga na sababu zangu ni za kizalendo kama chama changu cha ACT-Wazalendo. Ukishakuwa na sababu za kizalendo, hakuna sababu za kukukatisha tamaa hata kama nilishindwa,” amesema Mhandisi Mtambo

“Mimi ni zao lenu ninyi wana Mkuranga na hali ya jimbo letu si sawa na majimbo mengine. Hali tuliyonayo labda kaka tuliyemtuma kajisahau na mimi najua mlinichagua kwa wingi lakini haikuwezekana, kila mtu anajua kilichotokea,” amesema

Mhandisi Mtambo amewaomba wazee hao kuungana naye kwa kumshirikisha kwenye matukio ya furaha na huzuni kwani msije kusema “ulikuja ukataka tukupe chakula lakini ukaamua kukimbia baada ya kukikosa, hapana nimeamua kurudi kwa wazee wangu na nitakwenda kata kwa kata na kijiji kwa kijiji na mimi nataka nikaitetea Mkuranga yangu.”

“Si lazima wawe walinipa ubunge, nimerudi kwa wazee na tukiwa na msiba, hitima, kuna kumkosha maji mwajuma nijuzeni tushirikiane kwa pamoja. Nataka niitetea Mkuranga yetu,” amesema

“Naomba muniambie tatizo lolote likitokea, nieleze ili tujumuike kwa pamoja kabla hata hatujawa wabunge tushirikiane kwa kuwa pamoja. Ubunge ni miaka mitano tu, lakini nimeamua kurudi kuwashukuru kwa kunipa kura za kutosha hata kama sijaenda bungeni,” amesema Mhandisi Mtambo

Wakizungumza katika kikao hicho kilichofanyikia eneo la Churwi, Fatuma Ngelela amesema, tangu “nimefika hii Churwi ni pori, tumepambana sana kuhusu maendeleo na kilio kikubwa ni barabara na daraja linalounganisha eneo letu na Charambe, kila mara tumekuwa tunapiga kelele lakini tatizo halitatuliwi.”

Naye Juma Chikota, Mkongwe wa siasa za Churwi aliyekuwa CUF na baadaye kuhamia ACT-Wazalendo amesema “sisi hatuchagui mtathimini tunachagua mhandisi na lile daraja ni mfano tosha kuwa kila siku anakuja mtathimini (mbunge wao) anakagua na kuondoka huku tatizo linabaki palepale.”

Kwa upande wake, Khadija Omari amewaomba wazee wenzake kuwa “kijana wetu tumemwona, tumpokee kwa roho moja. Kijana kaongea vizuri sana na naomba wazee wenzangu.”

Khadija amesema, mbali ya tatizo la daraja ambalo Mhandisi Mtambo ameahidi kuendelea kupaza sauti hadi likamilike, ni umeme ambao umefikishwa kwao kimafungu fungu na kuiomba serikali kufikisha kwa wananchi wote.

Awali, Mwenyekiti Ngome ya Wazee Kata ya Tambani, Salum Ally Kundaukile amesema, “Huyu ni mbunge wetu. Licha ya kushindwa lakini ameona aje kuwashukuru kwa kumpa ushirikiano. Kushindwa kwake ameona ni busara arudi kuwashukuru.”

“Amesema hata kama hakushinda, ameona bora arudi. Wale ambao hawakufanikiwa kumwona wakati wa kampeni, tumemleta hapa ili tuweze kumwona,” amesema

Kwa upande wake, Katibu Mwenezi Jimbo la Mkuranga wa chama hicho, Hassan Msati amesema, watapita jimbo lote kutoa shukuran kwa makundi mbalimbali huku Katibu wa Ngome ya Wazee wa Mkuranga, Hamza Mnyonge akimpongeza Mhandisi Mtambo kwa kushukuru licha ya kushindwa.

“Licha ya kutoshinda lakini tumshukuru sana kijana wetu kwa kuja kutushukuru. Huu ndiyo uungwana sasa,” amesema

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Prof. Muhongo aungana na wananchi ujenzi maabara za sekondari

Spread the loveMBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, kwa kushirikiana na...

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa majina 12 ya familia moja waliofariki kwenye ajali Tanga

Spread the love  MAJINA 12 kati ya 17 ya waliofariki dunia katika...

Habari za Siasa

CCM apiga marufuku wazazi kuwatumia watoto wa kike kwenye mambo ya kimila

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo...

Habari za Siasa

Ofisi za mabalozi wa mashina zitumike kuwale vijana kimaadili – Chongolo

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameagiza...

error: Content is protected !!