Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Alichiandika Lissu, kuadhimisha miaka mwili tangu kupigwa risasi
Habari za Siasa

Alichiandika Lissu, kuadhimisha miaka mwili tangu kupigwa risasi

Tundu Lissu, Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya
Spread the love

SEPTEMBA 7, 2017 – SEPTEMBA 7, 2019: MIAKA MIWILI YA MATESO, MATUMAINI

Tundu AM Lissu, MB

Ndugu na marafiki zangu popote mlipo,

Wananchi wenzangu,

Salaam,

Leo ni tarehe 7 Septemba, 2019. Majira ya mchana wa siku kama ya leo miaka miwili iliyopita, nilitoka kwenye Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, na kuelekea nyumbani kwangu Area D kwa ajili ya chakula na mapumziko ya mchana.

Kwenye maegesho ya magari nje ya nyumbani kwangu, watu wawili wenye bunduki za kivita waliruka ghafla kutoka kwenye gari iliyokuwa inatufuata kwa nyuma na kuanza kunishambulia kwa risasi nyingi. Kati ya risasi zaidi ya 30 zilizoipiga gari, 16 zilinipiga katika sehemu mbali mbali za mwili wangu. Nilijeruhiwa vibaya.

Ijapokuwa ilikuwa mchana kweupe katika mji wa kawaida wa Dodoma, katikati ya nchi yetu; na katikati ya vikao vya Bunge ambapo ulinzi huwa mkali, washambuliaji hao walikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Leo hii, miaka miwili baadae, Serikali yetu bado inawaita washambuliaji hao ‘watu wasiojulikana.’ Hadi sasa, Jeshi la Polisi linadai halina ‘taarifa za kiintelijensia’ au hata tetesi za waliohusika kwenye kitendo hiki cha kijinai. Hakuna anayeshukiwa; hakuna aliyekamatwa na, kwa hiyo, hakuna aliyewajibishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Hii sio kwa bahati mbaya. Septemba 7, 2017, ilikuwa iwe hitimisho la mimi kuandamwa na vyombo vya usalama vya Serikali ya Rais John Pombe Magufuli.

Kati ya tarehe 29 Juni, 2016, na 18 Agosti ya 2017, nilipotoa rai hadharani kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi kuacha kunifuatafuata kila nilipokuwa nakwenda, nilikamatwa, kuwekwa mahabusu na baadae kushtakiwa mara sita kwa makosa mbali mbali ya uchochezi.

Siku yenyewe ya shambulio, hali haikuwa ya kawaida. Masaa machache kabla, Rais Magufuli alihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, wakati akipokea taarifa ya uchunguzi ya Bunge kuhusu madini ya almasi na tanzanite. Katika hotuba yake, pamoja na mengine, Rais Magufuli alitamka kwamba wale “wanaosaliti nchi wakati ikiwa kwenye vita ya kiuchumi hawastahili kuishi.”

Muda mfupi baada ya maneno hayo, nilishambuliwa kwa risasi nyingi na kujeruhiwa vibaya. Hadi leo haijawahi kuelezwa Rais Magufuli alikuwa anawalenga watu gani ambao, kwa maneno yake, ‘hawastahili kuishi.’

Itakumbukwa kwamba, katika kipindi hicho, kulikuwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa uliotokana na Serikali ya Rais Magufuli kukamata na kuzuia usafirishaji nje wa makinikia (mchanga wa dhahabu) ya kampuni ya Acacia Mining, uliopelekea kuandaliwa kwa Ripoti za maProfesa Mruma na Osoro, na baadae mabadiliko makubwa katika sheria zinazohusu madini na rasilmali nyingine za asili. Mimi nilipinga vikali vitendo na sera hizo za Rais Magufuli.

Itakumbukwa pia kwamba, katika kipindi hicho hicho, kulikuwa na mgogoro mkubwa uliotokana na mimi kutoa taarifa zilizokuwa zimefichwa na Serikali kuhusu kukamatwa nchini Canada kwa ndege ya Serikali kutokana na Serikali yetu kushindwa au kukataa kulipa deni la kesi iliyotokana na Serikali kuvunja mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Dar Es Salaam – Bagamoyo, kati yake na kampuni ya kimataifa ya ujenzi ya Sterling Construction & Engineering Ltd.

Ulinzi wote katika nyumba za Serikali nilikokuwa ninaishi uliondolewa siku hiyo ya shambulio. Kwa hiyo hao wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ walinifuata hadi ndani ya makazi ya viongozi wa umma, wakanishambulia kwa risasi na kisha kuondoka kwenye eneo hilo bila kizingiti chochote. Hadi leo, Jeshi la Polisi halijawahi kueleza ni nani aliyeamuru walinzi wote wa eneo hilo kuondolewa na sababu za kuondolewa kwao.

Lakini maajabu hayakuishia kwenye mazingira tata ya kabla na wakati wa shambulio. Siku tano baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilitangaza hadharani kupatikana kwa mkanda wa video uliochukuliwa na kamera ya ulinzi (CCTV) iliyokuwa imewekwa kwenye jengo la makazi yangu.

Hata hivyo, mwaka mmoja na nusu baadae, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alikanusha sio tu kuwepo kwa mkanda huo na kamera yake, bali pia kuwepo kwa ulinzi wowote katika majengo hayo ya viongozi wa umma mjini Dodoma.

Pengine maajabu makubwa zaidi yanahusu matibabu yangu. Mara baada ya jaribio la mauaji dhidi yangu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai, na viongozi wengine wa Bunge na Serikali, walitoa matamko mbali mbali hadharani kwamba Bunge na Serikali wangegharamia matibabu yangu.

Spika Ndugai aliwaandikia barua rasmi wawakilishi wa familia yangu, akiwaalika kwenye vikao pamoja naye kuhusu matibabu yangu. Vikao hivyo vilifanyika mara kadhaa katika Ofisi za Bunge Dar es Salaam na Dodoma. Kulikuwa na mabadilishano ya barua mbali mbali kati ya pande hizi mbili.

Hata hivyo, takriban miezi sita baada ya shambulio, Spika Ndugai alitangaza bungeni kwamba Bunge haliwezi kulipia gharama za matibabu yangu kwa sababu, pamoja na mengine, Rais Magufuli hakutoa ridhaa kwa fedha za Serikali kutumika kwa ajili ya matibabu yangu.

Ndio kusema kwamba yule aliyetangaza hadharani kwamba wale wanaopinga vita yake ya kiuchumi hawastahili kuishi, na nikashambuliwa kwa risasi muda mfupi baadae, ni yule yule aliyezuia mimi kutibiwa kwa gharama ya Bunge, kama inavyotakiwa na Sheria ya Uendeshaji wa Bunge.

Kuninyima gharama za matibabu haikutosha. Mwezi Disemba mwaka jana, nikiwa bado nasubiri operesheni tatu za mwisho, kulianza kujitokeza fununu kwamba kulikuwa na njama za kunifuta Ubunge kwa kisingizio cha utoro bungeni.

Ilipofika mwezi Februari ya mwaka huu, Spika Ndugai alitangaza rasmi bungeni kwamba Bunge litazuia malipo ya mshahara wangu na posho za kibunge kwa sababu yeye Spika alikuwa hajui niliko. Hivyo, kati ya Januari na Machi, Bunge lilizuia malipo ya mshahara na posho hizo hadi nilipotishia kupeleka shauri hilo mahakamani kudai haki zangu.

Hata hivyo, Spika Ndugai alitekeleza tishio lake la kunifuta Ubunge. Mnamo tarehe 29 Juni ya mwaka huu, Spika Ndugai alitangaza bungeni kwamba ameiandikia Tume ya Uchaguzi kuwa kiti cha ubunge cha Jimbo la Singida Mashariki kiko wazi kwa sababu ya mimi kutokuhudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge; na kutokujaza fomu za tamko la mali kama kiongozi wa umma.

Sasa suala hili liko Mahakama Kuu ya Tanzania kwa uamuzi, hivyo sitalizungumzia zaidi ya haya.

Itoshe tu kusema kwamba kama lengo la hao wanaoitwa ‘watu wasiojulikana’ lilikuwa ni kuniondoa bungeni ili nafasi yangu ichukuliwe na wale niliowashinda kwa kura za wananchi mara mbili mfululizo, basi lengo hilo limefanikiwa, angalau kwa muda tu.

Lakini kama lengo lao lilikuwa ni kuninyamazisha ili niache kupigania maslahi ya nchi yetu na wananchi wake, yaani kutetea haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na utawala bora, basi lengo la ‘watu wasiojulikana’ limefeli vibaya. Hii ni kwa sababu, Mungu aliyeniepusha na mauti ya risasi 16 siku ya Septemba 7, ameendelea kunisimamia katika safari ndefu ya matibabu na uponyaji.

Baada ya matibabu ya miaka miwili, kwanza katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, na tangu Januari ya mwaka jana katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, nchini Ubelgiji, sasa ninaweza kutangaza hadharani kwamba, kwa kiasi kikubwa, nimepona.

Nimeacha kutumia magongo tangu tarehe 29 Juni; na pia sindano na dawa zote nilizokuwa natumia tangu tarehe 30 Julai. Na kufuatia vipimo nilivyofanyiwa tarehe 20 Agosti, madaktari bingwa ambao wamenitibu tangu Januari mwaka jana wamenijulisha kwamba mifupa iliyovunjwa vunjwa na risasi za Septemba 7 mwaka juzi imeunga na kupona vizuri.

Aidha, vipimo vya damu vinaonyesha kwamba sasa damu yangu ni safi na haina bacteria wowote. Kilichobaki ni marekebisho ya viatu maalum nilivyotengenezwa kwa ajili ya kusawazisha mguu wa kulia ambao umekuwa mfupi kuliko mwingine kutokana na majeraha makubwa ya risasi za Septemba 7. Baada viatu hivyo kukamilika, nitafanyiwa vipimo vya mwisho tarehe 1 Oktoba na tarehe 8 Oktoba nitakutana na madaktari wangu ili kupatiwa maelekezo ya mwisho kabla ya safari yangu ya kurudi nyumbani.

Hii ni habari njema sana. Ni majibu muafaka ya sala, maombi na misaada yenu ya hali na mali katika kipindi chote cha kuanzia Septemba 7, 2017, hadi sasa ninapowapa taarifa hii.

Sala na maombi yenu kwa Mwenyezi Mungu hayakuwa ya bure. Fedha mlizonichangia; damu mliyonitolea; chakula na vinywaji mlivyoniletea nikiwa hospitalini Nairobi na UZ Leuven; salamu za pole na faraja mlizonitumia kwa simu na kwa kuja wenyewe hospitalini Dodoma, Nairobi na UZ Leuven, pamoja na nyumbani kwangu Tienen, vilinipa nguvu na ari ya kupambania afya na uhai wangu.

Juu ya yote, kazi kubwa iliyofanywa na madaktari bingwa, wauguzi na wafanyakazi wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Nairobi na UZ Leuven; pamoja na wataalamu wa mazoezi ya viungo wa Hospitali ya Nairobi, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Pellenberg, na wa Motion Center mjini Tienen, imezaa matunda mema.

Mke wangu mpenzi Alicia, wanangu Agostino Lissu na Edward Bulali, ndugu zangu wa kuzaliwa na wa ukoo, jamaa na marafiki zangu, waliumia kwa namna ambayo haielezeki. Leo ni siku yao ya kutua mzigo mzito wa majonzi na wasi wasi juu ya afya na maisha yangu.

Wananchi na wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki sio tu waliumiziwa Mbunge wao waliyemchagua kwa vipindi viwili mfululizo na kwa kura nyingi; bali wamemnyang’anywa kabisa na sasa wamepandikiziwa mtu ambaye hawakumpigia kura wala kumchagua. Kwao pia leo ni siku ya sherehe na ya ushindi. Nguvu za wema, nuru na maisha zimeshinda ubaya, giza na kifo.

Kwa viongozi wenzangu wa ngazi zote, wanachama, wafuasi na mashabiki wa chama changu cha CHADEMA na vyama vyote rafiki vya upinzani nchini kwetu, na kwa wapenda haki, uhuru na demokrasia katika nchi yetu, mpambanaji mwenzenu aliyejeruhiwa vibaya, sasa yuko tayari kurudi nyumbani kuchukua nafasi yake stahiki katika mapambano ya kuijenga Tanzania Mpya, yenye kujali haki, utu, uhuru na demokrasia kwa watoto wake wote.

Kwa mawakili na wanachama wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), ambao waliumiziwa na kunyang’anywa Rais wao miezi mitano tu baada ya kumchagua kwa kura nyingi kwenye uchaguzi wa kihistoria wa mwaka 2017, siku ya leo ni siku yenu muhimu kama mawakili na watetezi wa haki za wananchi wetu na utawala wa sheria katika nchi yetu.

Kwa Watanzania wote walioshtushwa, kusikitishwa na kufadhaishwa na tukio la kushambuliwa kwangu na yote yaliyofuatia tukio hilo hadi sasa, hii ni siku ya furaha kubwa na matumaini mapya.

Kama risasi 16 hazikuchukua maisha ya mtu mmoja, basi hakuna mauaji, utesaji, utekaji nyara, upotezaji watu na kesi za jinai za kutunga na kubambikiza wasio na hatia, vitakavyoua ari na madai halali ya watu wetu ya kuwa na nchi yenye kujali haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na utawala bora.

Kwa marafiki zetu na marafiki wa nchi yetu katika ukanda wetu wa Afrika na katika jumuiya ya kimataifa, ambao nao walishtushwa na kufadhaishwa na yaliyonitokea Septemba 7; na ambao wamesikitishwa na mwelekeo wa nchi yetu tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015, siku hii ni muhimu sana pia kwao na kwa nchi zao.

Ni siku ya kuwatia moyo marafiki wa nchi yetu kwamba pengine bado kuna matumaini ya kuiokoa nchi yetu isiingie katika mkondo hatari wa ilikoingia Zimbabwe na Burundi.

Sasa nirudi kwenye suala la kurudi kwangu nyumbani.

Nimeshauriana na ninaendelea kushauriana na viongozi wenzangu wa chama, pamoja na familia yangu kuhusu tarehe muafaka ya kurudi nyumbani. Nimezungumza pia na ninaendelea kuzungumza na viongozi mbali mbali wa kisiasa, kidini na wa taasisi za kijamii nchini kwetu.

Aidha, nimezungumza na ninaendelea kuzungumza na wawakilishi wa nchi marafiki wa Tanzania, mashirika na taasisi za kimataifa na za kikanda na mashirika ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu.

Mazungumzo na mashauriano haya yote yana lengo la kuhakikisha mazingira salama na muafaka ya kurudi kwangu nyumbani.

Kama mnavyofahamu, vitisho dhidi ya maisha yangu vimeendelea kutolewa hadharani kwenye mitandao ya kijamii na mtu ambaye – kwa maneno ya Mzee Abdulrahman Kinana na Mzee Yusufu Makamba – anaelekea kulindwa na kukingiwa kifua na mtu ambaye hawezi kuhojiwa na mtu au taasisi yoyote ya Serikali.

Baada ya mashauriano yote haya, tutakubaliana juu ya siku na utaratibu mzuri na salama zaidi wa kurudi kwangu nyumbani. Siku na utaratibu tutakaokubaliana utatoa muda wa kutosha kufanya maandalizi yote yanayohitajika, ndani na nje ya Tanzania. Siku na utaratibu huo utatangazwa kwa umma katika muda muafaka.

Naomba niweke jambo moja wazi. Hili ni kuhusu uwazi wa tarehe ya kurudi kwangu nyumbani. Baadhi ya watu, kwa kuelewa kuwa watu waliotumwa kuja kuniua bado wanaitwa ‘watu wasiojulikana’, wamenishauri kwamba tarehe ya kurudi nyumbani iwekwe siri mpaka siku yenyewe ya safari ya kurudi nyumbani.

Watu hawa wenye nia njema wanaamini kwamba, siku ya kurudi nyumbani ikiwa siri, basi ‘watu wasiojulikana’ na wale wanaowatuma hawatafahamu kuhusu ujio wangu, na kwa hiyo nitakuwa salama.

Pamoja na nia njema yake, siafikiani na ushauri huu. Mimi sio mhalifu, kwa hiyo siwezi kurudi nyumbani kwetu kwa kificho. Badala yake, nirarudi nyumbani kwetu mchana kweupe mbele ya macho ya Watanzania na ya dunia nzima.

Aidha, licha ya vitisho vya mauaji vilivyotolewa na Cyprian Musiba na wale wanaomtuma na kumkingia kifua, Serikali ya Rais Magufuli ndiyo yenye wajibu wa kisheria wa kuhakikisha ulinzi na usalama wangu nitakaporudi nyumbani. Kwa sababu hiyo, hatuwezi, na haitakuwa busara, kuifanya tarehe ya kurudi kwangu siri.

Vile vile, Watanzania wengi ambao wameniombea au kunichangia fedha na rasilmali zilizoniwezesha kuishi na kupatiwa matibabu Kenya na Ubelgiji, wangependa kuja kwa wingi kunipokea uwanja wa ndege siku hiyo.

Mimi mwenyewe ningependa kupokelewa na watu wengi iwezekanavyo, baada ya yote ambayo nimepitia, na ambayo nchi yetu imepitia, tangu Septemba 7, 2017.

Zaidi ya hayo, vyombo vya habari vya ndani na vya kimataifa, pamoja na marafiki wa Tanzania katika jumuiya ya kimataifa wangependa kujua siku na tarehe ya kurudi kwangu, ili waweze kufuatilia tukio hili muhimu kwa ukaribu zaidi.

Katika hali ya kipekee, kuna wawakilishi wa taasisi za kidini na kijamii, ndani na nje ya nchi yetu; wanadiplomasia kutoka nchi rafiki na mashirika ya kimataifa, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kimataifa, ambao wameonyesha nia ya kunisindikiza katika safari yangu ya kurudi nyumbani.

Katika mazingira haya, kurudi kwangu nyumbani hakuwezi kufanywa siri. Ni muhimu, kwa hiyo, tarehe ya kurudi kwangu nyumbani ijulikane wazi kwa kila mtu.

Kwa vyovyote vile, lazima tusiwape kisingizio walio na wajibu wa kisheria wa kuhakikisha ulinzi na usalama wangu, cha kuja kusema hawakujua siku na tarehe ya kurudi kwangu kwa sababu tuliwaficha.

Naomba kumalizia kwa kusema yafuatayo. Leo ni siku ya kumbu kumbu muhimu katika historia ya nchi yetu. Ni kumbu kumbu ya huzuni kwa yote yaliyotokea siku hiyo, na ambayo yametokea tangu siku hiyo.

Lakini ni kumbu kumbu ya furaha pia. Waliyoyapanga waovu siku hiyo, Mungu aliye mwema aliyazuia kwa mkono wake. Ibilisi wa kifo alishindwa na Malaika Mlinzi wa maisha yetu.

Nawaombeni wote, kila mmoja kwa imani yake, muiadhimishe siku hii kwa misa za shukrani, sala na maombi na kumbu kumbu za aina nyingine mbali mbali.

Nawashukuru sana na Mungu awabariki.

Eindhoven, Uholanzi
Septemba 7, 2019.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

error: Content is protected !!