Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Alibakwa, akaambukizwa Ukimwi, sasa shujaa
Makala & Uchambuzi

Alibakwa, akaambukizwa Ukimwi, sasa shujaa

Niqita Pieterse
Spread the love

NI binti anayetimiza miaka 28 mwaka huu. Alibakwa akiwa na miaka 10 na kuwa chanzo cha kuambukizwa ugonjwa wa ukimwi. Ameishi na virusi vya ugonjwa huo kwa miaka 18 na sasa anapigania ustawi wa watu wengine ili wasiupate na wale walioambukizwa; waishi bila hofu ya kifo.

Makala haya ya mahojiano na Niqita Pieterse anayeishi Durban, Afrika Kusini, yameandikwa na Simon Mkina wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tampa), yanaeleza zaidi … 

Swali: Mara nyingi umejitambulisha kuwa shujaa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwanini umeamua kujitangaza jemedari?

Jibu: Ama hakika mimi ni jemedari, unaona hata wewe umejua hilo! (anacheka). Vita nimevishinda, kwanza nikiwa peke yangu na sasa naendelea kukusanya jeshi kubwa ili ushindi uwe mkubwa zaidi na siku moja sote tufurahie ushindi kwa pamoja.

Najiita jemedari, lakini wengine wananiita Malkia wa Ukimwi, haya yote ni majina yangu kuonyesha namna jitihada zangu za kueneza elimu dhidi ya Ukimwi zinavyoshika kasi kila siku.

Swali: Unakusanyaje jeshi lako na kina nani wapiganaji wako?

Jibu: Ushindi dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi unahitaji nguvu ya pamoja, nimeamua kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuelimisha watu, siyo wa hapa Durban, au Afrika Kusini pekee, bali Afrika na dunia nzima.

Jeshi ninalozingumzia hapa ni wale watu walioathirika na kuathiriwa kwa VVU (Virusi Vinavyosababisha Ukimwi) na Ukimwi na wale ambao wana nia njema kuangamiza ugonjwa huu. Nashukuru nchi nyingi sasa, hasa za Afrika zinatambua juhudi zangu na napokea misaada mingi ya kunipa moyo ili juhudi za kuelimisha jamii ziendelee.

Swali: Ushindi upi unaozungumzia?

Jibu: Nazungumzia ushindi dhidi VVU vinavyoleta ugonjwa wa Ukimwi. Huu ni ugonjwa usiobagua, unatuathiri wote; matajiri kwa masikini, haujali rangi; unashambulia weusi na wazungu wala hauangalii kimo; uwe mrefu ama mfupi, unaweza kuambukizwa tu.

Inaeleweka sasa kwamba Ukimwi unasambazwa kwa njia nyingi, ingawa kubwa na ambayo inafahamika kwa wengi ni njia ya ngono zisizokuwa salama. Njia nyingine ni pamoja na kuchangia vitu vyenye ncha kali na mtu aliyeambukizwa tayari na hata kuongezwa damu ya muathirika.

Katika hilo la ngono zisizokuwa salama, wapo wanaobakwa na wale wanaoamua kutotumia kinga dhidi ya Ukimwi. Kinga salama zaidi ni kutumia kondomu.

Swali: Lipi lilikukuta mpaka ukaambukizwa Ukimwi?

Jibu: Mimi nilibakwa nikiwa na miaka 10, wakati huo nilikuwa binti mdogo kabisa, nikiwa bado nasoma elimu ya msingi. Nilifanyiwa ukatili huo na baba yangu mdogo ambaye alikuwa anaishi kwenye familia yetu. Ni mtu ambaye aliaminika na kuthaminiwa sana pale nyumbani, lakini kumbe alikuwa mtu mbaya sana asiyekuwa na maadili ya kijamii na kimila.

Pamoja na kuwa baba mdogo, lakini pia alikuwa rafiki yangu mkubwa, kila mara, baada ya masomo alikuwa akinifundisha hesabu na masomo mengine, siku za wikiendi alinichukua kwenda matembezi na kuninunulia vitu vidogo vidogo madukani.

Hakuwahi hata siku moja kuniambia kunitamani kwa mtazamo wa kingono. Nami sikuwa na mawazo mabaya juu yake. Lakini mwisho wa siku alinigeuka na kunibaka tukiwa ndani ya nyumba yetu. Ilikuwa siku ya Jumamosi ambapo hapakuwepo watu ndani, walienda matembezini. Yeye aliamua kubaki na kunishawishi kubaki naye tukiangalia vipindi vya televiseni.

Swali: Alikushawishi kwa lipi?

Jibu: Tukiwa tumeketi tunaangalia televisheni, alianza kunishikashika, nami sikupenda na nilimwambia kuwa sipendi. Lakini aliendelea. Nilimwambia nitamsema kwa mama endapo akiendelea. Aliamua kutumia nguvu kuniingilia kimwili.

Swali: Je, ulipiga kelele ili kumtisha?

Jibu: Nilijaribu kupiga kelele lakini sikufanikiwa kwa vile alikuwa ameniziba mdomo kwa kiganja cha mkono wakati ananiingilia kwa nguvu. Hakika aliniumiza sana katika viungo vyangu vya kijinsi na baada ya tukio lile nilishindwa kutembea kwa sababu ya maumivu.

Swali: Baada ya wazazi kurejea, uliwaeleza kilichotokea?

Jibu: Ilibidi kuwaeleza wanafamilia. Kiliitishwa kikao cha ukoo. Baada ya kuona kikao kimeitishwa, baba mdogo aliamua kukimbia na kutokomea kusikojulikana.

Katika kikao kile, kulitokea minyukano na mtafaruku mkubwa kuhusu kwenda kuripoti kituo cha polisi, wapo waliotaka nikashtaki na wengine wakisema ni aibu kwa ukoo, lakini kwa kuwa tamaduni nyingi za Afrika zinakumbatia mfumo dume – unaoshabikia ukatili wa kijinsia, hatukuweza kwenda polisi kushtaki.

Nguvu ya mama na wengine waliokuwa wakitaka twende kushtaki ilishindwa na ile ya wanaume ambao wengi hawakutaka jambo hii haramu kisheria na kimaadili, kwenda mbele ya vyombo vya sheria.

Swali: Pole sana, lini sasa uligundua kuwa umeambukizwa VVU?

Jibu: Baada ya kutokea hayo, niliamua kutoroka nyumbani na kwenda kujihifadhi kwenye kituo cha kulea watoto yatima. Nilipokelewa na kuanza maisha mapya ambapo pia niliamua kuacha shule.

Niliendelea kukulia hapo. Lakini huko nako nilibakwa na mwanaume nisiyemjua. Alinivamia nje kidogo ya kituo chetu. Baada ya miaka saba tangu nibakwe nikaona afya yangu inaanza kutetereka polepole, nilikuwa naumwa homa mara kwa mara, kupungua uzito na kukohoa. Niliamua kwenda hospitali kupimwa na ikagundulika kuwa nimembukizwa tayari.

Swali: Matokeo ya vipimo uliyatarajia na je, ulifahamu kuwepo kwa ugonjwa huo?

Jibu: Kamwe sikuyatarajia, niliona kwa umri wangu mdogo, magonjwa kama Ukimwi hayanihusu. Nililia sana. Nilikata tamaa na kuona dunia yangu imefika mwisho.

Nilijawa na mawazo mengi, nikataka kujiua ili niondoke mapema duniani na nisije kuteseka kwa Ukimwi baada ya kuamini jamii itanikataa kwa unyanyapaa. Mawazo haya yaliendelea kwa muda wa miezi mitano, na kila siku uzito wangu ulipungua kwa sababu ya msongo wa mawazo.

Lakini siku moja, miaka 10 iliyopita, niliamua kwenda hospitali tena na kuanza dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, kwani natambua kwamba hakuna tiba kabisa.

Hospitalini walinifanyia uchunguzi na kubaini kwamba nahitaji kuanza kumeza ARVs, dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo. Tangu kipindi hicho hadi sasa, sijarudi nyuma na afya yangu inaimarika kila uchao, si unaona nakuwa mrembo zaidi! (anacheka).

Swali: Umesema una watoto watatu, wako salama, maana uliwapata wakati tayari umegundua kwamba umeambukizwa?

Jibu: Hawa watoto wote wako salama kabisa. Hawana maambukizi na vyeti vyao VVU hivi hapa kutoka hospitali mbili tofauti – (anaonyesha vyeti VVU hivyo).

Swali: Umesema una mume, je, ana maambukizi kama wewe?

Jibu: Kama walivyo watoto wangu, na baba yao pia hana maambukizi. Hajaambukizwa na sitarajii apate mambukizi kutoka kwangu, kwa kuwa wote nawalinda.

Swali: Unawalindaje?

Jibu: Nawalinda kwa kutumia ARVs kila siku. Unajua unapotumia vidonge vya kufubaza VVU, mara nyingi, virusi vinakosa nguvu, vinashindwa kuongezeka, hivyo kunakosekana mwanya wa kuambukiza wengine. Hatimaye unakuwa na msongamano mdogo wa VVU kwenye damu (low viral load count), kiasi kwamba huwezi kumwambukiza mtu.

Mume wangu na watoto wangu wamekuwa msaada mkubwa kwangu. Huwa wananikumbusha kumeza dawa kila unapofika muda. Watoto wangu, hasa huyu mkubwa—mwenye miaka 8—ananiletea dawa. Baba yao naye kila akitoka kazini lazima anikumbushe. Sasa dawa zimekuwa sehemu ya maisha yangu. Nimezoea kabisa.

Swali: Wakati unaanza uhusiano a mume alijua hali yako ya VVU?

Jibu: Hapana, hakujua, nami sikutaka kuwa na papara kumwambia kwani nilikuwa natafuta muda muafaka wa kufanya hivyo.

Siku moja alikuja kunichukua nilipokuwa naishi – kwani baada ya kutoka kwenye kituo cha watoto yatima, nilipanga chumba. Tulitoka na kwenda matembezini, na huko ndiyo nilimweleza kuhusu hali yangu ya kuwa na VVU.

Alikosa nguvu baada ya kusikia kwamba nina maambukizi, aliinama kwa muda, lakini baadaye aliinua kichwa chake na kuonekana machozi yakimlengalenga. Nilimfahamisha kuwa nilikuwa na uhakika kuwa nitamlinda hata kama tukifanya ngono siwezi kumdhuru. Hatimaye akatamka… “usijali, nitaendelea kuwa nawe.” Baada ya hapo nilianza kumwelezea kilichotokea.

Lakini hatukuwa tumefanya ngono kabla kabla ya hapo, kwani nilitaka awe na uamuzi ulio huru kabisa kabla ya kuanza uhusiano wa kimapenzi na mtu mwenye VVU.

Aliikubali hali yangu na tuliendelea hadi leo ambapo tuna watoto watatu na familia bora yenye furaha tele. Yeye na watoto wako salama.

Swali: Afrika ina watu milioni 37 wenye mambukizi na milioni nane wako Afrika Kusini, nchini mwako, unawafikiaje hawa?

Jibu: Kama nilivyokueleza, vita dhidi ya Ukimwi naipigana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Lakini pia natumika zaidi kutoa elimu kupitia matamasha mbalimbali, huko nakutana na vijana, kila nikisimama, wao wanaelimika na kujiepusha na maambukizi na wale walioambukizwa tayari, nawatia moyo na kuwasisitiza kuwa kupata Ukimwi siyo mwisho wa dunia. Kwamba maisha yapo tu hata baada ya kuambukizwa, kikubwa ni kujitunza na kufuata masharti ya wataalamu wa afya.

Swali: Vipi kuhusu tatizo la unyanyapaa?

Jibu: Hapo awali baada ya watu kugundua kwamba nina maambukizi ya VVU walianza kunitenga. Unajua niliamua kuweka wazi mwenyewe kwenye mitandao ya kijamii. Lakini, baadaye nimezoeleka na nina marafiki dunia nzima. Kuna wachache wananinyanyapaa, lakini wengi wananiona shujaa. Hata wewe ni rafiki yangu kutoka Tanzania. Karibu!

Swali: Nini falsafa yako katika mapambano haya?

Jibu: Virusi viko ndani yangu, havinipi chakula, havilipi kodi, siviogopi. Mimi ndiye naviongoza. Havinitishi kamwe.

Naomba waathirika wengine wote waibebe hii falsafa. Na kama bado mtu hajaambukizwa, basi ajilinde ama kwa kujizuia, au kwa kufanya ngono salama kwa kutumia kondomu kila wakati, au kujenga mahusiano na mpenzi mmoja asiye na maambukizi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!