January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Albino wazichapa Ikulu kabla kuteta na JK

Rais Jakaya Kikwete akiwakaribisha viongozi wa maalbino

Spread the love

KIKAO baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi viongozi  wa Chama Cha Watu Wenye Ulemavu wa ngozi (Albino), nusura kishindwe kufanyika baada ya Albino kuvurugana na viongozi wao katika lango kuu la Ikulu. Anaandika Mwandishi wetu … (endelea).

Sababu ya vurugu hizo ni wanachama kupinga uwakilishi wa viongozi wao, wakidai muda wa kuwa madarakani ulikoma tangu mwaka jana na hivyo kutaka waruhusiwe waingie wote kuonana na rais.

Wamesema kuwa wawakilishi hao wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi yao kila wanapopata fursa ya kukutana naviongozi wakuu badala ya kueleza matatizo ya wenzao.

Ilikuwa kama “sinema” kuona watu waliopata fursa ya pekee ya kuonana na rais kuzungumzia hoja zao kutokana na mauaji ya yanayoendelea nchini dhidi yao, badala yake wanageuka kuchapana makonde wenyewe kwa wenyewe.

Lakini heka heka iliyotokea katika eneo la mapokezi iliwalazimu maafisa wa Ikulu kuwatawanya walemavu hao.

Ni muda mfupi baada ya ukaguzi kuanza kufanyika katika moja ya lango la kuingilia Ikulu, kundi moja la walemavu hao waliokuwa katika moja ya chumba wakaanzisha malalamiko kwa sauti huku viongozi wao wakiwa wanajiandaa kuruhusiwa kuingia ndani.

Kelele hizo na mabishano hayo miongoni mwao kwa mbali ikaanza kuonekana ni dosari hasa baada ya kila mmoja kuanza kusema lake kupinga ushiriki wa viongozi hao.

Kutokana na vurugu hizo, maafisa wa Ikulu waliwatawanya na kutoka nje ya lango na hapo ikawa mwanzo wa sakata jipya baada ya kuanza kulumbana na viongozi wao na hatimaye kupigana.

Wateta na JK

Baada ya rabsha hizo kutulizwa, maafisa wa Ikulu waliwaongoza wawakilishi wa walemabu hao hadi kwa Rais Kikwete, ambaye katika mazungumzo yake amesema Serikali inasikitishwa na kufedheheshwa sana na mauaji dhidi yao na kwamba itafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji haya.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Kikwete amewaeleza viongozi hao  walioongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest Kimaya kuwa; “Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana”.

“Msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo,” amesema rais.

Katika kikao hicho viongozi hao, wamesoma risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja ambayo itajumuisha Serikali, viongozi wa Albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu katika suala hili ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini.

Rais Kikwete amesema mauaji hayo hayafanywi na serikali bali watu ambao wako katika jamii kwa kushirikiana na waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii hivyo na kwamba ni lazima yakomeshwe.

“Kwenye familia,  jamii na hatimaye  vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo jukumu kubwa ambalo serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa ushirikiano wa pamoja,” ameahidi.

Rais amesisitiza kuwa kamati hiyo ya pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya walemavu hao.

Pia, aliahidi kuwa serikali  itasaidia familia na wahanga wa vitendo vya mauaji kwa hali na mali  ili waweze kujimudu na pia kuwapa ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo hivyo kwani vinawaletea waathirika na watu wanaoishi nao mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii.

Katika kikao hicho, viongozi wametoa kilio chao kwa serikali kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua kuwa zinatetea haki za Albino nchini bado hazina mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.

Naye Ernest Kimaya-mwenyekiti wa walemavu hao, ameelezea masikitiko yake kwa rais kuhusu vurugu zilizojitokeza muda mfupi miongoni mwa kabla ya kikao hicho.

Kwa mujibu wa Kimaya, uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha na wamemuomba rais awasaidie kutimiza azma yao ya kuitisha mkutano na kuchagua viongozi wa chama chao.

Kimaya ameongeza kuwa wamepanga kufanya mkutano huo wa kuchagua viongozi katikati ya mwaka huu ambapo pia dunia itakua inaazimisha siku ya watu wenye Albino duniani.

error: Content is protected !!