September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Akopesha wananchi kisha awasulubu

Spread the love

NELSON Ndalu (67) anatuhumiwa kukopesha wananchi kwa riba kubwa na kisha kuwafilisi kwa kutaifisha mali zao kinyume cha sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani Dodoma, inamshikilia Ndalu maarufu kwa jina la Osama kwa madai ya kutumia vibaya mikopo hiyo kinyume na sheria na kusababisha hasara kwa wananchi.

Tuhuma zake zinaelezwa kwamba, amekuwa akikandamiza wakopaji, kisha kutumia fursa hiyo, kutaifisha mali zao ikiwemo mashamba, nyumba kwa wale wanaoshindwa kurejesha madeni yao.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano tarehe 3 Juni 2020 na Sosthenes Kibwengo, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Dodoma.

Kibwengo amedai kuwa, Osama amekuwa na tabia ya kudhulumu wateja wake wanaoshindwa kulipa madeni, kufuatia kuwawekea riba kubwa, inayoanzia asilimia 100.

“Osama ambaye anafanya biashara ya kukopesha fedha bila kufuata taratibu za ukopeshaji amekuwa akitoa mikopo kandamiza kwa wananchi wa Kata ya Chamkoroma, ambapo wananchi wengi walishindwa kurejesha mikopo hiyo yenye riba kuanzia asilimia mia moja, “ amesema Kibwengo na kuongeza:

“Katika utaratibu maarufu kama shilingi kwa shilingi, na hivyo wakapoteza mashamba na nyumba zao walizoweka dhamana.”

Kibwengo amesema TAKUKURU ilichukua hatua ya kumshikiliwa Osama, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi mmoja wa Kata ya Chamkoroma, ya kwamba amedhulumiwa na mkopeshaji huyo.

“Baada ya TAKUKURU wilayani Kongwa kupata malalamiko ya mwananchi mmoja mwezi Mei 2020,  ilifanya uchunguzi na kubaini kwamba ni kweli Osama amekuwa na tabia hiyo kwa muda mrefu, na baadae wakatokea wananchi wengine ambao nao walikuwa na malalamiko ya kudhulumiwa na hivyo kuifanya TAKUKURU kumshikiliwa mkopeshaji huyo,” amesema Kibwengo.

Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani Dodoma amesema, baada ya taasisi hiyo kumshikilia mtuhumiwa huyo, tarehe 27 Mei 2020, alikubali kurejesha mashamba yenye hekari 30, na nyumba mbili kwa wananchi 13, ambao anadaiwa kuwapora.

“Tarehe 27 Mei 2020 aliridhia kurejesha mashamba na nyumba mbili kwa wananchi hao 13, baada ya kulipwa fedha alizowakopesha,” amesema Kibwengo.

Wakati huo huo, Kibwengo amesema TAKUKURU mkoani humo imerejesha kiwanja namba 3 Kitalu Q, Iyumbu New Town Center kwa mkurugenzi wa jiji hilo.

Amesema TAKUKURU ilichukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba aliyekuwa mhasibu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), alimwezesha rafiki yake kupata kiwanja hicho kwa njia ya udanganyifu.

“ Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba malipo ya awamu tatu yenye jumla ya Sh. 43,613,600, yalionekana kufanywa kulipiwa kiwanja hicho kati ya Junu 2016 hadi Januari 2017, na kukatiwa stakabadhi za malipo ni batili kwani fedha hizo hazikupokelewa na risiti za mfumo wa Epicor ni za kughushi,” amesema Kibwengo.

error: Content is protected !!