AKAUNTI za Benki za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), zilizofungwa Agosti 2020, zimefunguliwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa ya kufunguliwa kwa akaunti hizo, imetolewa leo Jumatano tarehe 21 Aprili 2021, na Mwenyekiti wa Bodi ya THRDC, Vicky Ntetema.
Taarifa ya Ntetema imesema kuwa, akaunti hizo zimefunguliwa baada ya Serikali kuagiza zifunguliwe.
“Kufunguliwa kwa akaunti hizo kumetokana na maelekezo kutoka kwa mamlaka za serikali zilizoagiza kufungwa ili uchunguzi wa tuhuma zifanyike. Na kisha kutoa maelekezo kuwa zifunguliwe,” imesema taarifa ya Ntetema.
Awali, Serikali iliagiza akaunti hizo zifungwe ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizokuwa zinaukabili mtandao huo, ikiwemo kutowasilisha mikataba au makubaliano ya fedha za ufadhili katika Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s).

Pamoja na kutowasilisha nyaraka za usajili wa wanachama wake kwa ajili ya kusajiliwa na Serikali.
Kufuatia sakata hilo, THRDC ilitangaza kusitisha shughuli zake, lakini kwa sasa taarifa ya Ntetema imesema shughuli hizo zinaendelea kama kawaida.
“Hivyo basi, kwa taarifa hii mtabdao unaendelea na majukumu yake yote kwa mujibu wa mipango yake ya mwaka 2021. Tuendelee kushirikiana,” imesema taarifa ya Ntetema.
Aidha, THRDC imeshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo ya kufunguliwa kwa akaunti zake.
” Bodi ya THRDC inamshukuru Rais Samia kwa uongozi wake unaojali na kuzingatia haki za binadamu na utawala bora,” imesema taarifa ya Ntetema.
Leave a comment