CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema, kimewapeleka wanachama wake wanne bungeni ili wakasimamie ajenda tano za chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Ado amezitaja ajenda hizo kuwa ni Katiba Mpya inayotokana Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, Masheikh wa Uamsho Zanzibar, Muungano, Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu na hali ya maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne tarehe 9 Februari 2021, na Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo wakati akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu.
Wabunge hao wanne walioapishwa na Spika Job Ndugai tarehe 15 Desemba 2020, bungeni jijini Dodoma ni Khatib Said Haji (Konde), Salum Mohamed Shafi (Chonga), Omar Ali Omar (Wete) na Khalifa Mohamed Issa (Mtambwe).
“Na ndio maana wabunge wetu wanne tumeruhusu waende bungeni wakapeleke ajenda zetu. Tuna vipaumbele vitano, ambavyo ni Katiba Mpya inayotokana na mchakato uliosimamiwa iliyokuwa tume ya Jaji Joseph Warioba, Masheikh wa Uamsho, mikopo ya wanafunzi, muungano na hali ya kimaisha ya Watanzania,” amesema Ado.
Awali , ACT-Wazalendo kiliungana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutopeleka wawakilishi wake bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020, kwa madai kwamba mchakato wake haukuwa huru na haki.

Hivyo, Bunge la 12 lilifunguliwa na Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli tarehe 12 Novemba 2020 bila kuwa na wabunge wa upinzani.
Lakini baadaye ACT-Wazalendo kilipeleka wabunge wake, ambao waliapishwa na Spika Ndugai tarehe 15 Desemba mwaka jana.
Katibu huyo wa ACT-Wazalendo amesema, kipaumbele cha kwanza cha chama hicho bungeni ni Katiba Mpya, na kwamba wabunge wake wameanza kuwasilisha michango ya chama hicho.
“Tumehakikisha kwamba wanakwenda ndani ya bunge na ajenda maalumu, na ajenda ya kipaumbele ni Katiba Mpya, na tunashukuru wabunge wanaendelea kuitendea haki ajenda hiyo ndani ya bunge katika michango yao ili kuweza kutoa mchango wa chama katika msukumo wa katiba mpya,” amesema Ado.
Hivi karibuni mbunge wa Chonga visiwani Zanzibar (ACT-Wazalendo), Salum Mohamed Shafi, aliibua mjadala wa Katiba Mpya na sakata la Masheikh wa Uamsho bungeni, akiitaka serikali kufanyia kazi masuala hayo.
“Ajenda ya pili Masheikh wa Uamsho, sababu tunaona imetosha, masheikh wamekaa miaka minane ndani. Kama kuna ushahidi ndani yao wapelekwe mahakamani ili wahukumiwe, kama hakuna ushahidi miaka minane inatoisha kukaa ndani.
“Ni muhimu waachiwe huru. Hilo limekwisha zungumzwa ndani ya bunge, tunasubiri serikali itoe majibu,” amesema Ado.
Mwanasiasa huyo amesema, ACT-Wazalendo kimewatuma wabunge wake kuwasilisha bungeni ajenda ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu wa juu.
“Ajenda nyingine ni kuhusu mikopo ya wanafunzi, tumewaagiza wabunge wetu wakaisimamie bungeni na tunashukuru wanaisimamia vizuri,” amesema Ado.
Ado amesema, kuhusu ajenda ya muungano, ACT-Wazalendo kimewatuma wabunge wake kuhakikisha wanatoa michango yao bungeni itakayosaidia kutatua changamoto za muungano ambazo hajifanyiwa kazi muda mrefu.
“Ajenda nyingine ni muungano, rais katika hotuba yake ya ufunguzi bunge alizungumza kudumisha amani na muungano, lakini tumeagiza wabunge wetu wakasisitize kwamba muungano tunaohitaji ni wa haki na kuhesimiana,” amesema.
Amesema, ajenda ya mwisho ni kuhusu hali ya uchumi wa Watanzania, ambapo wabunge wake watatumia muhimili huo kuwasilisha changamoto za maisha ya makundi mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima.
“La mwisho ni hali ya kimaisha, hali ya maisha kwa makundi mbalimbali ya kijamii, wakulima, wafanyakazi, wana kero nyingi.
“Wafanyabishara ambao tunataka wabunge wetu wakasimamie, na hivi ndio vipaumbele vyetu vitano tulivyowatuma wakashughulikie,” amesema Ado.
Aidha, Ado amesema ACT-Wazalendo kitatuma ajenda zake bungeni kupitia wanachama wake hao, kulingana na mijadala itakayokuwa inaendelea.
“Ajenda zitakuwa zinatofautiana kutokana na ajenda mama ya bunge kwa wakati husika, inategemea bunge limeitishwa kwa ajenda gani. Kama limeitishwa kwa bajeti tutakuwa na vipaumbele vyetu katika bajeti.
“Kama kwa ajili ya sheria maalumu tutakuwa na maoni katika sheria hiyo, lakini kwa sasa inafahamika ajenda mama ni kujadili hotuba ya ufunguzi wa bunge ya rais,” amesema na kuongeza:
“Kwa kweli kwa kila bunge tutakwenda kwa vipaumbele, wabunge wetu watakapa ushirikiano wetu kutoka katika chama, kila bunge tutahakikisha kuna ajenda maalumu na wabunge wetu watasimama.”
Leave a comment