WATU 4,060 wamepoteza maisha kwa ajali za barabarani na wengine 6,427 wakipata majeraha kutokana na ajali za barabarani kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Hayo yameelezwa leo Jumanne tarehe 14 Machi 2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizindua wiki ya Nenda kwa Uasalama Barabara, hafla iliyofanyikia kitaifa mkoani Mwanza.
Majaliwa amesema takwimu hizo ni zile ajali ambazo ziliripotiwa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo kwa kipindi hicho ziliripotiwa ajali 5,132 zilizosababishwa na vyombo mbalimbali vya usafiri.
“Nyote mtakubaliana nami kwamba ajali za barabarani zimekuwa ni chanzo cha maumivu na majonzi kwa familia nyingi, zimechangia sana wafanyabisahara na wafanyakazi wengine kupata ajali, kupotez maisha na kupoteza mali,” amesema Majaliwa.
Akielezea makundi ya ajali zilizosababisha vifo hivyo Majaliwa amesema vifo 1,582 ni vya abiria wa vyombo vya usafiri huku amjeruhi wakiwa 4,372.
Amesema katika kipindi hicho amesema watembea kwa miguu 959 walipitiwa na vyombo vya usafiri na kupoteza maisha na wengie 650 wakijeruhiwa.
“Tukitumia vyombo vya moto lazima tuzingatie watembea kwa miguu na watembea kwa miguu pembeni mwa barabara nao lazima wazingatie usalama wao,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wa wapanda pikipiki kundi ambalo linahusisha boda na za watu binafsi amesema zimesababisha vifo 797 na wengine 725 walijeruhiwa.
Aidha amesema waendesha baiskeli 196 wamepoteza maisha katika kipindi hicho na wenigne 82 wamejeruhiwa.
Majaliwa amesema kwa upande wa madereva wa vyombo vya moto 589 wamepoteza maisha na wengine 584 wamepata majeruhi na wajasiriamali na watembeza mikokoteni 17 wamepoteza maisha na 14 kupata madhara.
“Nimejaribu kuonesha kwa makundi ili mpate picha namna ya ajali zinavyoteketeza maisha katika maeneo mbalimbali…idadi hii ni kubwa sana kuitaja hivyo nawasihi watanzania tutafakari lakini tutafakari kwa kujua sheria zilizopo za usalama barabarani kwa kufanya hilo tutafanikiwa,” amesema Majaliwa.
Amesisitiza kuwa jukumu la usalama barabarani ni la kila mmoja wetu na wala sio jukumu la Serikali pekee.
“Tushirikiane na kuzuia ajali kwa kuelimishana kwanza lakini kwa kuonya na kutahadharisha pale sheria zinapovunjwa kila mmoja ashiriki kwa kuonya,” amesisitiza.
Leave a comment