August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ajali yaua wawili, yajeruhi 26 Singida

Basi la kampuni ya National Express lililokuwa linafanya safari zake kutoka Kiomboi kwenda Dar es Salaam limepata ajali katika kijii cha Tumuli, wilaya ya Mkalama, Singida

Spread the love

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya National Express lenye namba za usajili T.662 DEF baada ya kuacha barabara na kupinduka zaidi ya mara tatu katika eneo la kijiji cha Tumuli, Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida, anaandika Mwandishi wetu.

Waliopoteza maisha kwa ajali hiyo ni dereva wa basi hilo, Athumani Idd (47) mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam na Mwalimu wa shule ya msingi Malunga aliyefahamika kwa jina moja tu la Janeth (anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 29).

Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, ACP.Debora Daudi Magiligimba alibainisha kwamba watu hao walifariki dunia papo hapo na miili yao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Akizungumza kwenye eneo la tukio Basi hilo lilikuwa linatokea New Kiomboi,likielekea jijini Dar-es-salaa Kamanda huyo aliweka bayana kuwa ajali hiyo imetokea dec,30,mwaka huu saa 12:45 asubuhi katika eneo la Kijiji cha Tumuli,na kwamba ajali hiyo pia imesababisha majeruhi 26 ambao wamelazwa katika Hosipitali ya Mkoa wa Singida kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Kamanda Magiligimba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa ajali hiyo imesababishwa na mwendo kasi na uzembe.

“Eneo hili ilipotokea ajali hii kuna mteremko na kona kali,kutokana na mwendo kasi ndipo dereva alishindwa kulimudu na hivyo kuacha barabara na kuingia kwenye korongo la mto na kuruka juu na kisha kupinduka mara tatu”,alisisitiza Kamanda huyo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Singida,Dk.John Mwombeki alikiri kupokea miili ya watu wawili waliofariki dunia kwenye ajali ya basi la Kampuni ya National Express pamoja na majeruhi 26.

“Kati ya maejeruhi hawa mmoja ni dada Joyce tumempa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na sehemu yake ya chini ya mwili kutokufanya kazi na kwamba majeruhi 10 wao tunaendelea kuwafanyia uchunguzi,lakini hata hivyo kuna uwezekano wa kuwapa ruhusa leo hii”,alifafanua Dk.Mwombeki.

Hata hivyo mmoja wa majeruhi hao ambaye pia ni mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) jijini Dar-es-salaam, Victor Elia alisema pamoja na kupoteza kila kitu lakini anamshukuru Mungu kwa kupona kufa kwenye ajali hiyo mbaya.

“Kilichonisaidia ni kufunga mkanda….abiria wenzangu wote ambao hawakufunga mikanda ndio walioumia zaidi wakiwemo waliopoteza maisha na ajali hii kwa vye vyote vile imechangiwa na mwendo kasi”. alisema Victor ambaye ni Mtayarishaji na mtangazaji wa TBC.

Nicolaus Apolinari (23), kondakta wa basi hiyo mkazi wa jijini Dar-es-slaam alisema ajali hiyo imechangiwa na utelezi uliosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hilo.

error: Content is protected !!