January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ajali yaua 14 Mwanza, wamo waandishi 6, Rais Samia awalilia

Spread the love

WATU 14 wamefariki dunia wakiwemo waandishi wa habari sita wa Mkoa wa Mwanza baada ya gari waliokuwa wakisafiri kwenda Ukerewe mkoani humo kugongana uso kwa uso na gari la abiria Toyota Hiace. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ajali hiyo imetoa asubuhi ya leo Jumanne, tarehe 11 Januari 2022, wakiwa njiani kwenda Ukerewe katika ziara ya mkuu wa mkoa huo, Robert Gabriel kukagua miradi ya maendeleo.

Baadhi ya waandishi waliofariki ni, Johari Shani wa Uhuru, Afisa Habari wa Mkoa huo, Abel Ngapemba, Husna Mlanzi na Antony Chuwa wote wa ITV.

Husna Mlanzi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametumia ukurasa wake wa Twitter kutuma salamu za rambirambi akisema, “nimeshtushwa na vifo vya watu 14 wakiwemo wanahabari sita vilivyotokea leo asubuhi baada ya gari lililokuwa katika msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kugonga na daladala.”

“Poleni wafiwa, wanahabari na jamaa wote. Mungu aziweke mahali pema roho za Marehemu na Majeruhi wapone haraka.”


Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika akaunti yake Twitter ameweka gari lililokuwa limebeba waandishi na kuandika, “nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya gari iliyosababisha vifo vya maafisa habari, waandishi wa habari wa Mwanza na wananchi.”

“Natoa pole kwa familia za marehemu, waandishi wa habari wote, ndugu, jamaa na marafiki. Mungu aziweke mahali pema roho za marehemu wote, Amina.”

error: Content is protected !!