RAIS Samia Suluhu Hassan amewaasa Watanzania kuwa watulivu wakati zoezi la uokoaji linaendelea katika na ajali ya ndege namba PW 494 ya Kampuni ya Precision Air iliyotokea leo tarehe 6 Novemba, 2022 wilayani Bukoba mkoani Kagera. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bukoba … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa leo kupitia mtandao wa Twitter, Rais Samia ameandika, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera.
“Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii. Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie.”
Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya ndege ya Shirika la Precision katika Ziwa Victoria, mkoani Kagera. Natuma salamu za pole kwa wote walioathirika na ajali hii. Tuendelee kuwa watulivu wakati huu zoezi la uokoaji likiendelea huku tukimuomba Mwenyezi Mungu atusaidie.
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) November 6, 2022
Ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam, kuelekea Bukoba, imepata hitilafu na kulazimika kutua majini mjini Bukoba ikiwa ni umbali unaokadiriwa kuwa mita 100 kutoka ulipo uwanja wa ndege Bukoba.
Taarifa zilizothibitishwa na mmoja wa wafanyakazi wa ndege hiyo zinasema, hitilafu hiyo, ilitokana na ndege hiyo, kushindwa kutoa matairi wakati wa kutua katika uwanja wa Ndege wa Bukoba, majira ya saa tatu asubuhi ya leo Jumapili, 6 Novemba 2022.
Leave a comment