January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ajali ya basi na lori yaua 11, kujeruhi 26

Spread the love

WATU 11 wamefariki dunia, 26 wakiwa wamejeruhiwa huku wanne kati yao wakipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza, Tanga kutokana na ajali ya gari iliyotokea leo.

Ajali hiyo imetokea saa 1 asubuhi katika eneo la Tanga Mlima ambapo imehusisha basi la Kampuni ya Simba Mtoto lenye namba za usajili T 393 DBZ na lori aina ya Scania lenye namba T 738 CFE ambalo lilikuwa limebeba mchanga.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo,Mihayo Msikhela ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani humo, amesema, chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kusinzia.

Amesema, kusinzia kwa dereva huyo kumesababisha lori hilo kuacha njia na kwenda kugongana na basi hilo lililokuwa likitoka Tanga.

Kamanda Msikhela amesema, majeruhi hao kwa sasa wamepelekwa katika Hospitali ya Muheza na 24 kati yao wanaendelea vizuri.

Akitaja jinsia ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo, Kamanda Msikhela amesema wanaume ni wanane huku wanawake wakiwa ni watatu akiwemo mtoto wa miaka miwili na nusu wote wakiwa wa familia moja ambapo maiti sita kati yao tayari zimetambuliwa na ndugu zao.

error: Content is protected !!