September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ajali Mwanza yaua 13, yajeruhi 11

Spread the love

WATU 13 wamefariki dunia huku wengine 11 wakijeruhiwa katika ajali ya basi la kampuni ya Super Shem, ambalo limegongana uso kwa uso na daladala katika eneo la Nhungumalwa, wilayani Kwimba jijini Mwanza, anaandika Moses Mseti.

Ajali hiyo imetokea leo, saa 12 asubuhi  wakati basi hilo lenye namba T- 874 CEW lililokuwa likitoka Mbeya kuja Mwanza kugongana daladala Na. T368 CWQ iliyokuwa ikitoka barabara ndogo ya Shilima kuelekea Nyegezi.

Tukio hilo linakuja katika kipindi ambacho wimbi la ajali za barabarani linazidi kuongezeka hapa nchini, ikiwemo ajali mbaya iliyotokea mwanzoni mwa wiki hii mkoani Njombe na kusababisha watu 12 kupoteza maisha huku Rais John Magufuli akituma salamu za rambi rambi.

Chanzo cha ajali iliyotokea leo jijini Mwanza kinatajwa kuwa ni dereva wa daladala aliyekuwa akitoka barabara ndogo ya Shilima akielekea Nyegezi kuingia barabara kuu bila kuzingatia sheria.

Mtemi Simion, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, amesema kuwa majeruhi wa ajali hiyo pamoja na marehemu wapo katika hospitali ya Wilaya ya Kwimba- Ngundu.

“Baada kutokea ajali, majeruhi wote walikimbizwa hospitalini na wengine watatu walipelekwa hospitali ya Wilaya ya Misungwi kutokana na hali zao kuwa mbaya ambapo wawili kati yao walipoteza maisha wakati wakiwa njiani,” amesema Simion.

Bethod Mchemba, Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Kwimba-Ngundu, amekiri kupokea majeruhi na miili ya marehemu wakiwemo watoto wawili.

“Kati ya majeruhi tuliopokea, watatu  wanahali mbaya na tayari wamepelekwa hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibu zaidi ambapo wengi wao wana majeraha ya kuvunjika nyonga, miguu pamoja na kutikisika kwa ubongo,” amesema Mchemba.

Eliza Magambo, Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, amesema kuwa dereva wao hakuwa kwenye mwendo wa kasi na kwamba kosa lilifanywa na dereva wa daladala aliyeingia barabara kuu bila kuangalia kushoto na kulia.

Ahmed Msangi, Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, amedhibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akiwataka madereva kuwa makini pindi wanapokuwa wanatumia vyombo vya moto.

“Ajali hii ni ya kwanza tangu nihamishiwe hapa nikitokea Mbeya, imesababishwa na uzembe wa madereva ambao kila kukicha tunakemea suala la uzembe huu,” amesema Msangi.

Msangi ameongeza kuwa, ajali hiyo imetokea ikiwa ni wiki moja kabla ua kuanza kwa wiki ya nenda kwa usalama barabarani inayotarajiwa kuanza wiki ijayo na kusisitiza kuwa, wataendelea kutoa elimu juu ya kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

 

error: Content is protected !!