December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ajali bodaboda pasua kichwa, 445 hufariki kila mwaka

Spread the love

 

RAIS Samia ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kutoa kipaumbele cha elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda kwa kuwa ndio wanaoongoza kwa matukio ya ajali za barabarani. Anaripoti Mwandishi Wetu (endelea)

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo tarehe 23 Novemba, 2021 wakati akihutubia katika maadhimisho ya Wiki nenda kwa usalama barabarani yaliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kauli mbiu ya ‘Jali maisha yako na ya wengine barabarani.’

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita jumla ya wapanda pikipiki 2,220 wamepoteza maisha kutokana na ajali barabarani na majeruhi 4,202.

“Hii ina maana kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja, tumepoteza vijana 445 kwa mwaka wanaoendesha bodaboda peke yao, mahospitali yetu yalikuwa na vijana 850 kila mwaka wanaotokana na ajali za bodaboda, wao kugonga wengine au kusababisha gari liue.

“Kwa hiyo watoto wangu na Watanzania mnaoendesha bodaboda kuwa kinara katika takwimu hizi sio zifa njema, niombe Jeshi la polisi mnapoendesha elimu ya usalama barabarani mara nyingi bakini na waendesha bodaboda tena kila mkoa waelewe nini wanapaswa kufanya barabarani,” amesema.

Amesema wachangiaji wengine wakubwa wa ajali za barabarani katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka huu, ni madereva wa magari binafsi ambao wamesababisha ajali 535, matroli ya trela 209, mabasi ya abiria ajali 148 na daladala ajali 142.

Amesema licha ya kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu kujitosheleza, jukumu la usalama barabarani ni la kila mmoja.

“Ni jambo la kusikitisha kuona ajali za barabarani zimekuwa zikigharimu maisha ya watanzania wengi mbali na juhudi za serikali kuwekeza kwenye miundombinu bora ya barabara, vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa wamekuwa wahanga wakubwa wa ajali hizi.

“Ingawa kuna dalili za kupungua kwa ajali hizi bado takwimu zilizosomwa hazitoi taswira nzuri kwa nchi yetu. Takwimu ukizitazama zinaonesha zaidi ya asilimia 90 za ajali husababishwa na makosa ya kibinadamu kama vile mwendo kasi, uendeshaji wa hatari, kuovertake katika maeneo yasiyoruhusiwa, kutovaa mikanda, au helmet, uzembe wa dereva na watembea kwa miguu,” amesema.

Awali Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Wilbroad Mutafungwa amesema matukio ya ajali yalikuwa 1,388 mwaka 2020, mwaka 2021 yalikuwa 1,187 yamepungua matukio 201 sawa na asilimia 14.5.

“Vifo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020 vilikuwa 949, Januari hadi Septemba mwaka huu ni vifo 900, hivyo tumepunguza vifo 49 sawa na asilimia 5.2.

“Majeruhi mwaka 2020 walikuwa 1,672, mwaka 2021 katika kipindi hicho walikuwa 1,405 hivyo tumefanikiwa kupunguza majeruhi 267 sawa na asilimia 16.0,” amesema.

error: Content is protected !!