January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Airtel yaeleza miamala ya Mbowe mahakamani

Spread the love

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, imepokea taarifa za miamala na usajili wa simu, kutoka kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania PLC na barua ya Ofisi ya Uchunguzi wa Kisayansi ya Jeshi la Polisi, kama vielelezo vya Jamhuri. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Nyaraka hizo zimepokelewa mahakamani hapo leo Alhamisi, tarehe 13 Januari 2022, mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya Meneja wa Kitengo cha Sheria cha Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania (PLC), Gladys Fimbari, kuiomba izipokee kama vielelezo vya Jamhuri.

Jaji Tiganga aliipokea barua ya Kampuni ya Airtell kwenda kwa Kamishna wa Uchunguzi wa Kisayansi wa Jeshi la Polisi, kama kielelezo namba 15, barua ya Ofisi ya Uchunguzi huo kwenda kwa Airtell ilipokelewa kama kielelezo namba 16, ripoti ya usajili wa 0784779944 (17).

Taarifa ya usajili ya 0782237913 (18), taarifa ya usajili wa 0787555200 (19) na taarifa ya miamala ya 0784779944 (20).

Fimbari alitoa maombi hayo baada ya kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janetreza Kitali, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ni katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Adam Kasekwa, Mhoamed Ling’wenya na Halfan Bwire waliowahi kuwa makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Fimbari ambaye ni shahidi wa tisa wa Jamhuri, amesema taarifa hizo ni za miamala na usajili wa namba za simu za 0782237913, 0787555200 na 0784779944, iliyofanyika kati ya tarehe 1 Juni hadi 31 Julai 2020, zilizoombwa na Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Jeshi la Polisi.

Fimbari amedai nyaraka hizo alizifanyia kazi na kuziandaa tarehe 2 Julai 2021, baada ya kampuni hiyo kupokea barua ya maombi ya uchunguzi kutoka kwa Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Fimbari, namba 0784779944, inadaiwa kumilikiwa na Freeman Aikael Mbowe, 0782237913 inamilikiwa na Halfan Bwire Hassan na 0787555200 ni ya Denis Urio ambaye ni ofisi wa JWTZ.

Katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi, Mbowe anadaiwa kutoa fedha zaidi ya Sh. 600,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kulipua vituo vya mafuta, kukata miti barabarani na kufanya vurugu kwenye mikusanyiko ya watu.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Kitali shahidi huyo amedai tarehe 2 Julai 2021, akiwa ofisi za Airtel Moroco, jijini Dar es Salaam akiendelea na majukumu yake, kuu wake wa idara ya sheria alimpangia kushughulikia maombi ya taarifa kutoka Ofisi za Uchunguzi wa Kisayansi za Jeshi la Polisi

Amedai maombi hayo yalikuwa yakitaka taarifa za miamala ya fedha ya namba 0782237913, namba nyingine ilikuwa 0787555200 ya tatu 0784779944. Pia iliomba taarifa za usajili wa namba hizo

Shahidi huyo amedai, alihakiki barua kujua ilitoka kwenye mamlaka husika za ofisi za uchunguzi wa kisayansi, ambapo “niliangalia ile barua ilikuwa inaongelea uchunguzi. Niliangalia taarifa gani ambazo zinaombwa kwa muda gani, pia nilihakikisha kwamba ilikuwa imesainiwa pamoja na mhuri wa chombo husika.”

Amedai baada ya kujiridhisha “niliingia kwenye kifaa changu cha kazi ambacho ni kompyuta kisha nikaingia kwenye mfumo kupitia mfumo huu ulikuwa ukifanya kazi vizuri, nikaingiza namba moja ya simu ambayo imeombewa taarifa na kisha nikaitolea taarifa baada ya kuchakata.”

Shahidi huyo amesema, mialama iliyofanyika ni ya tarehe 31 Julai 2021 wa Sh. 80,000 kutoka namba 0784779944 inayodaiwa kuya ya Freeman Mbowe kwenda 0782237913.

Amedai, salio lilikuwa ni Sh.104,284, baada ya kutuma alibakiwa na Sh. 23,684 na muamala ulifanikiwa kufanyika vizuri.

Mbali na muamala huo wa Mbowe, shahidi huyo amesoma mumala wa fedha unaodaiwa kufanyika tarehe 20 Julai 2020 katika namba inayodaiwa kuwa ya Dennis Urio 0787555200 iliyopokea Sh.500,000 kutoka kwa namba 0780900174. Kwa mujibu wa usajili wa namba hii, imesajiliwa jina la ‘Tigo Pesa Tigo Pesa.’

Fimbari alidai kuwa, tarehe 20 Julai 2020, ulifanyika muamala kutoka 0787555200 iliyosajiliwa kwa jina la Dennis Urio kwenda kwenye namba 0785191954, iliyosajiliwa jina la Augustino Hilary Msacky kiasi cha Sh.300,000, ambapo mhusika alikuwa na Sh.549,646 kisha baada ya kutuma alibakiwa na 243,646.

Akiendelea kuongozwa na Wakili Kitali, Fimbari alisoma muamala uliofanyika tarehe 22 Julai 2020, unaodaiwa kufanywa wa Sh.199,000 kutoka namba 0780900244 ambayo imesajiliwa kwa jina la VodacomDisb Tanzania kwenda 0787555200 iliyosajiliwa kwa jina la Dennis Urio.

error: Content is protected !!