Tuesday , 26 September 2023
Home Kitengo Biashara Airpay yapata leseni ya BoT kutoa huduma za malipo kidigitali
Biashara

Airpay yapata leseni ya BoT kutoa huduma za malipo kidigitali

Kunal Jhunjhunwala
Spread the love

KAMPUNI ya Airpay Tanzania imezidi kupanua wigo wake wa kuhakikisha wananchi kuttoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar wanapata huduma za uhakika za malipo ya fedha kwa njia ya kidigitali, baada ya kutambuliwa na kupewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa huduma hiyo hapa nchini. Anaripoti Mwandishi wetu …(endelea).

Kwa mujibu wa Airpay yenye makao makuu yake nchini India huku upande wa Tanzania ikiwa na ofisi kuu Visiwani Zanzibar, imeahidi kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi na kulinda kila taarifa ya mtumiaji wake.

Akizungumza mjini Zanzibar, Mwanzilishi wa Kampuni hiyo Kunal Jhunjhunwala alisema wanafuraha kupokea leseni hiyo ya huduma za malipo kutoka BoT na kwamba hiyo inaashiria kujitolea kwao katika kupanua huduma za kifedha kidijitali barani Afrika, huku Tanzania ikitumika kama lango lake kwa bara la Afrika.

Alisema mafanikio hayo yanaashiria hatua kubwa kwa Airpay Payment Services Private Limited ambayo ilianza safari yake Februari 2023 na tangu wakati huo wamefanya mikutano ya mashauriano na wadau mbalimbali wa Zanzibar na Bara.

Jhunjunwala alisema Airpay iliishirikisha Kampuni ya Ushauri ya Twigalpha Limited yenye makao yake makuu nchini Tanzania kwa kengo la kutoa mwongozo wa kimkakati wa upanuzi wake barani Afrika.

“Ushirikiano huu ulileta majadiliano na warsha ya wiki nzima juu ya jinsi gani Airpay itakavyotoa mwongozo wa njia kuelekea Zanzibar ya Kidigitali Kwanza,” alisema

Aidha, alisema zaidi ya uzuri wa Tanzania wa asili na vivutio vya kuvutia vya utalii, kuna fursa ya kweli kwa Airpay kuchukua sehemu muhimu katika safari ya kidijitali nchini ya kujenga jamii na uchumi usiotegemea mzunguko wa pesa taslimu.

“Binafsi nimejizatiti kufanya niwezavyo kuisaidia Tanzania kufikia malengo haya wakati kampuni yetu inapoanza safari yake kama mtoa huduma za malipo za Omnichannel hapa nchini, naamini sana katika ushirikiano na kuendeleza mfumo ikolojia unaowezesha kwa wote. ” alisema Jhunjhunwala.

Kwa upande wake Mwanzilishi Mwenza wa Airpay Tanzania, Yasmin Chali alisema kampuni hiyo bado imejitolea kutoa suluhu za malipo za kiubunifu, salama na zinazoweza kufikiwa kwa biashara na watumiaji barani Afrika huku zikiunganisha huduma za kifedha ndani na nje ya bara hilo.

Alisema leseni hiyo ya huduma za malipo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inasisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo kufuata mahitaji ya udhibiti wakati wa kutoa huduma za malipo ya kisasa.

“Nyuma ya teknolojia ni mwananchi ambaye anahitaji kuwa na uwezo wa kuamini huduma za kifedha za kidigitali ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku, sio kutuma na kupokea pesa tu. Tulikubali kufanya kazi na Airpay kwa sababu miongoni mwa watu wengi wanaotakia mema nchi, sisi kama waongozaji wa teknolojia ya Kiafrika na wafuatiliaji wa kufuatilia, tuliona imani na uaminifu ambao shirika hili lilikuwa nao.

“Twigalpha inachagua aina ya wateja tunaowachukua kwani tunaelewa kuwa tuna wajibu wa kimaadili wa kuhakikisha kwamba tunaleta aina sahihi ya mwekezaji na mshirika, na Airpay inalingana vizuri na kile tunachoona kinahitaji kutokea nchini Tanzania katika nyanja ya kidigitali,” anasema Chali

Naye Makamu Rais na Meneja Mikakati wa kampuni hiyo, Mihayo Wilmore alisema leseni hiyo mpya inaipa kampuni uwezo wa kufanya kazi ndani ya mfumo ikolojia wa fedha wa Tanzania, na hivyo kuimarisha uwepo wake barani Afrika.

Alisema Airpay inajenga Makao Makuu ya Afrika yenye hadhi ya kimataifa visiwani Zanzibar, sambamba na Mpango wa Silicon Zanzibar. Kutoka katika kisiwa hicho cha paradiso, Airpay inalenga kufikia kila kona ya Afrika kupitia ushirikiano wa thamani.

“Safari hii haikuanza Februari, imekuwa na mchakato wa subira na machungu kwa miaka 30 iliyopita. Hakika tulikatishwa tamaa na hata kutaka kutupa taulo na kutoka nje ya ulingo. Airpay inaleta msisimko na hari mpya katika mfumo wa ikolojia wa kidijitali nchini Tanzania.

“Tulikuwa tumedumaa kama tasnia na kukimbilia kulalamika. Tunaishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mtazamo wake wa dira na kuweka vipaumbele vya kidigitali. Ninatazamia sana kufanya kazi na washirika wapya na wa zamani. Milango yetu iko wazi kwa ushiriki na ushirikiano,” alisema Wilmore

Alisisitiza kuwa huduma za malipo za Airpay zimejitolea kudumisha viwango vya juu vya usalama na uzingatiaji nchini Tanzania.

“Kampuni itashirikiana kwa karibu na mamlaka ya Tanzania, wabia na wadau ili kuhakikisha matumizi ya uhakika na salama kwa watumiaji wote wa jukwaa la huduma zake za malipo,” alisema.

Aidha, inaelezwa kuwa Airpay ni kampuni ya kwanza ya kutoa huduma za fedha ya India iliyojumuisha huduma za kifedha za aina mbalimbali inayowawezesha watumiaji, wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo katika mkondo wa mwisho wa huduma, na hivyo kupelekea ujumuishaji wa kweli wa kifedha.

Mtazamo wao wa utoaji huduma katika mkondo wa mwisho umewezesha uwepo wa watumiaji wadogowadogo katika vijiji zaidi ya 5900 nchini India, unaojumuisha wilaya 558 na majimbo 37 na wajasiriamali wadogo zaidi ya 500,000 wanaoitwa “airpay vyaapaaris,” alisema.

Wana ushirikiano na taasisi za kifedha zaidi ya 200, na washirika wa kifedha zaidi ya 1000. Kimataifa Airpay inamtazamo wa kutanua nyayo zake katika Afrika na Mashariki ya Kati.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

NBC kuchochea ustawi biashara kati ya Tanzania na Afrika kusini.

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza kuhusu dhamira yake...

Biashara

NMB yazindua hati fungani mpya ya trilioni 1

Spread the loveBENKI ya NMB imezindua rasmi programu mpya yenye hati fungani...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kununua mitambo 15 ya kuchoronga miamba

Spread the loveSerikali kupitia Wizara ya Madini imepanga kununua mitambo 15 ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Mtanzania aweka rekodi kimataifa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu

Spread the loveIMEELEZWA kuwa Kiwanda cha Kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery...

error: Content is protected !!