August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Aibu tupu Serikali ya Rais Magufuli

Spread the love

NI aibu katika utawala wa Rais John Magufuli tangu aingie madarakani kwa kuwa, hali ya ukandamizaji inaelezwa kukithiri, anaandika Regina Mkonde.

Serikali ya Rais Magufuli imeelezwa kukithiri kwa ukiukwaji wa haki ya kuishi, uwakilishi bungeni, uhuru wa kujieleza, kutoa maoni, kupata habari pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, umekithiri katika kipindi cha nusu mwaka wa 2016.

Kauli hiyo imeelezwa leo na Helen Kijo Bisimba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) wakati akitoa ripoti ya haki za binadamu kwa kipindi cha nusu mwaka wa 2016 kuanzia Januari hadi Julai.

Bisimba amesema kuwa, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa na kituo hicho, ufuatiliaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na taarifa mbalimbali kutoka kwa waangalizi wa haki za binadamu na wadau wengine umebaini ukiukwaji wa hali ya juu katika kipindi cha nusu mwaka.

“Mauaji yanayotokana na imani za kishirikina pia yemeendelea kuwa chanzo cha mauaji na mateso hususan kwa vikongwe katika maeneo ya vijijini, ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka wa 2016 yameripotiwa mauaji ya watu 394.

“Hii inaonyesha ongezeko kubwa ukilinganisha na vifo vilivyotokea kwa kipindi kama hiki kwa mwaka 2015 ambapo ni vifo 57 tu ndivyo vilivyoripotiwa,” amesema.

Bisimba ameyataja maeneo yaliyo kinara kwa kukithiri kwa mauaji hayo ikiwemo Mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga.

“Taarifa za Jeshi la polisi zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji kwa watu kujichukulia sheria mikononi yamekuwa yakipungua, hii ni kulingana na taarifa za matukio haya kwa vipindi vya nusu mwaka kwa miaka minne iliyopita,” amesema na kuongeza;

“Kwa kipindi cha nusu mwaka wa 2016 taarifa kutoka jeshi la polisi zinaonyesha watu 135 waliuawa kutokana na watu kujichukulia sheria mikononi. Matukio ya vifo hivi ni pungufu ya kipindi cha mwaka 2015 ambapo viliripotiwa vifo 366.”

Kuhusu vifo vya watu mikononi mwa vyombo vya dola, amesema kuwa vyombo hivyo vinahusishwa na kusababisha mauaji ya watu mbalimbali wakiwa chini a ulinzi wa vyombo hivyo.

“Vyombo vya dola vimehusishwa na kusababisha mauaji ya watu mbalimbali wakiwa chini ya ulinzi wa vyombo hiyo,taarifa rasmi ya jeshi inaonyesha ni mtu mmoja pekee aliuawa akiwa mikononi mwa jeshi hilo, taarifa hii haikuanisha huyu mtu aliuawa wapi,” amesema.

Amesema hata hivyo kituo cha LHRC kina taarifa ya matukio ya watu wawili wanaosemekana walifia mikononi mwa vyombo vya dola, moja lilitokea mkoani Mtwara na jingine kutoka mkoani Shinyanga.

“Askari polisi nao wamekuwa wahanga wa mashambulizi mbalimbali hasa wanapokuwa kazini, matukio ya uvamizi yaliyozoeleka ni yale ya uvamizi wa vituo vya polisi yanayofanywa na watu wenye hasira kali ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka vituo 5 vya polisi vilivamiwa,” amesema na kuongeza.

“Taarifa zinaonyesha kuwa askari polisi 2 waliuawa huku 4 walivamiwa na kujeruhiwa katika matukio mengine.”

Kuhusu ukiukwaji wa uhuru wa haki za kisiasa, uhuru wa kutoa maoni pamoja na ugandamizwaji wa vyombo vya habari, Bisimba ameeleza kuwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa isimame kama chombo huru ambacho kinaweza kusimamia masilahi ya vyama vya siasa kwa kulinda haki ya vyama hivyokufanya kazi zao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.

“LHRC bado kinaamini kuwa sheria ya makosa ya mtandaoni ina makosa yanayominya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, pia imeshuhudiwa kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na upatikanaji wa habari, pamoja na kuzuiwa kwa baadhi ya mikutano ya kisiasa huku baadhi ya chama vikifanya mikutano ambayo mazingira yake yanafanana,” amesema.

Ametaja baadhi ya mikutano iliyozuiliwa ikiwa ni pamoja na ule wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kahama na pia ACT-Wazalendo.

error: Content is protected !!