March 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ahadi ya Rais Magufuli, nyumba za Magomeni yaota mbawa

Ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota ulipoanza. Picha ndogo Rais John Magufuli alipokuwa anatoa ahadi ya ujenzi huo

Spread the love

AGIZO  la Rais John Magufuli alilotoa mwaka jana la kujenga nyumba eneo la Magomeni Kota limegeuka kuwa ahadi hewa baada ya kazi hiyo kushindwa kufanyika badala yake kiwanja hicho kimegeuzwa kuwa maegesho ya magari, anaandika Mwandishi Wetu.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo Septemba 6  mwaka jana na kuagiza Wakala wa Majengo Nchini (TBA),  waanze kujenga nyumba 644 katika eneo hilo ndani ya miezi miwili.

Alitoa miezi miwili ya maandalizi na baada ya hapo waanze kujenga nyumba hizo na kuwapa mwaka mmoja ambao umeisha mwezi uliopita kuikamilisha ili waliokuwa wapangaji wa nyumba hizo kabla ya kubomolewa wapewe wakae bure kwa muda wa miaka mitano.

Alisema baada ya miaka mitano kupita ya kukaa bure wapangaji hao wauziwe nyumba hizo kwa bei nafuu huku akisisitiza kwamba hakuna mtu kutoka nje atakayeuziwa.

Tangu  Rais Magufuli atoe agizo hilo mbele ya wananchi hao, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, umepita zaidi ya mwaka sasa lakini hawajaanz hata kuchimba msingi.

“Nasema wakandarasi ndani ya miezi miwili waanze kujenga nyumba 644 kwa ajili ya wazee ambao wameteseka sana baada ya nyumba zao kuvunjwa, nitatoa fedha serikalini mwezi huu (wakati huo mwaka jana mwezi wa 9) kwa ajili ya kuanza kwa shughuli hiyo,” alisema Dkt. Magufuli.

Wakati huo alisema ujenzi huo anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi sita kama ulivyokuwa kwa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es  Salaam.

Rais Magufuli alisema angefurahi kama angepewa nafasi ya kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.

“Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,”alisema Magufuli.
Rais Magufuli alionyesha kukerwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kuwanyima haki wanyonge.

Alifafanua kuwa vitendo hivyo vya unyanyasaji viishe mara moja na Watanzania wakae kwenye nchi yao kwa amani.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi alimshukuru  Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge hasa kwa kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa Magomeni Kota.

“Mheshimiwa Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee hawa wa Magomeni, nami nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro huu hadi kupata ufumbuzi”, alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema wakati huo kuwa  mgogoro wa Magomeni ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo ameishughulikia na ataendelea kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu ardhi ziishe kama alivyoagizwa na Rais.

Nyumba zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi wakaahidiwa kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei nafuu. Lakini kwa takribani miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali ambayo iliwafanya wakazi hao waishi maisha ya kuangaika.

Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli alifuta hati zote za umiliki eneo la Magomeni Kota na kuondoa usimamizi wa Nyumba TAMISEMI na kuupeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuanza kusimamia ujenzi.

error: Content is protected !!