MBUNGE wa Same Magharibi, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), David Mathayo David, amehoji ni lini Serikali ya awamu ya tano inayongozwa na Rais John Magufuli, itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Pangani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akizungumza bungeni katika kipindi cha maswali na majibu leo Jumatano tarehe 10 Februari 2021, David amesema ujenzi wa daraja hilo ilikuwa ahadi ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
David amesema, ahadi hiyo ya Kikwete, aliyekuwa Rais kati ya mwaka 2005-2015, ililenga kuondoa adha ya usafiri kwa wakazi wa jimbo lake.
“Safari ya Kutoka Kilimanjaro kwenda Dodoma kupitia Same na Simanjiro, huweza kufupishwa kwa zaidi ya kilomita 180 na kupunguza usumbufu.
“Je, ile ahadi ya Rais wa awamu ya nne (Rais Kikwete) ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya ya Same na Simanjiro, utaanza lini?” amehoji David.
Rais Kikwete alimaliza muda wake wa uongozi wa vipindi viwili mfululizo (2005-2015), Novemba 2015, kisha alikabidhi kijiti kwa Rais Magufuli.
Ikijibu swali, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi imesema, serikali imepanga kutenga kiasi cha fedha katika bajeti ya mwaka 2021/2022, kwa ajili ya kufanya usanifu wa daraja hilo, kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura).
Wizara hiyo imeeleza, usanifu huo utafanyika katika eneo ambalo kutajengwa daraja pamoja na barabara itakayounganisha Wilaya za Same na Simanjiro.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Tarura imepanga kufanya usanifu wa daraja ikiwa ni pamoja na kipande cha barabara yenye urefu wa kilomita 34.2 kwa upande wa Same hadi kufikia eneo la Mto Pangani. Panapohitajika kujengwa daraja ili kuunganisha Wilaya za Same na Simanjiro,” imeeleza wizara.
Aidha, wizara hiyo imeeleza, Tarura imekuwa ikihudumia kipande cha barabara hiyo kwa kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi, ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 Sh. 48 Mil zilitumika kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 kiasi cha Sh.63 milioni, kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ambapo kwa sasa mkandarasi anaendelea na matengenezo ya kipande cha kilomita 7,” imelezwa.
Na kwamba, serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa daraja na miundombinu ya barabara muhimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
Leave a comment