January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ahadi ya elimu bure yamuinua Lowassa

Spread the love

AHADI ya kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya vidudu hadi chuo kikuu anayoitoa mgombea urais anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa leo ilipokewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa jimbo la Ubungo, ambako mgombea huyo alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Lowassa ambaye anapeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema wananchi wa Ubungo pamoja na Watanzania wengine kote nchini wasisumbuke kumuuliza atapata wapi fedha za kugharamia elimu kwa watoto wa Tanzania.

“Usiniulize hela nitapata wapi? Za kutoa elimu bure Tanzania pesa nyingi zipo serikalini. Kama waliopo madarakani sasa wana uwezo wa kuwanunulia wanawake na ndugu zao nyumba za kuishi kwanini tukose za kutolea elimu bure?”

Lowassa amesema ili kufanikisha mpango huo uliomo kwenye ilani inayounganisha Chadema pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) vinavyounda UKAWA, akishaingia madarakani serikali atakayounda itaunda tume kuchunguza sababu za watu kuichukia elimu.

Mkutano huo ulifanyika uwanja wa TP Sinza ambako pia mgombea ubunge wa UKAWA, Saed Kubenea, alihutubia akijiombea kura binafsi, na pia kuwaomba wananchi wampigie kura Lowassa za kumpa ridhaa ya kuwa rais wa Tanzania.

Lowassa amesema atakapoingia Ikulu wananchi watashuhudia utendaji wa kasi kwani serikali yake ataipeleka kwa spidi zote ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kufuta umasinini miongoni mwa Watanzania.

“Mimi nauchukia sana umaskini na ndio maana ninagombea urais, nataka niivunje ile hali ya kupata mlo mmoja kwa siku, niwaongoze Watanzania katika kuukimbia umaskini. Serikali yangu itakuwa na usawa kwa wote, hata marafiki zangu bodaboda, mama ntilie na wamachinga wanufaike,” amesema.

Lowassa anafuatana na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ambaye amekuwa akimuunga mkono tangu naye alipoamua kujitenga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa mwezi Agosti.

Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka miwili tu kwa kujiuzulu, aliondoka CCM Agosti 24 mwaka huu, baada ya kulalamika alikatwa jina kihujuma katika kutaka uteuzi wa chama hicho agombee urais.

Sumaye alimuombea kura Lowassa akisema anamuamini ana uwezo na dhamira nzuri ya kuwaondoa Watanzania katika tatizo kubwa la umasikini, na kwamba akichaguliwa, ataunda serikali makini kusimamia ndoto yake hiyo.

Akizungumzia mgombea ubunge jimbo la Ubungo, Sumaye alihimiza wananchi wamchague Kubenea aliyesema ni kijana muadilifu na mchapa kazi hodari. Alisema ni kosa kubwa kumachagua Didas Masaburi, kwa kuwa amesema ana matendo mengi ya ufisadi yanayomnufaisha yeye binafsi na CCM kinachomlinda asishitakiwe.

Amewaambia wananchi hao kuwa CCM imempendekeza Masaburi kugombea jimbo hilo ikiwa ni kama zawadi.

“Tumetoka CCM na kuja CHADEMA ili tuwasaidie Watanzania wenzetu kuondokana na umaskini na kuwaangusha mafisadi waliojaa CCM. Nawashangaa wanasema wataukomesha ufisadi, labda aanze viongozi wake wa juu,” anasema Sumaye akimaanisha Dk. John Magufuli, mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Akihutubia wananchi na kuwaomba kura, Kubenea ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), aliahidi atakapokuwa mbunge, kupigania kubadilisha sheria zote kandamizi ndani ya jimbo hilo zilizowekwa na uongozi wa Masaburi ambaye ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

“Nalijua vizuri Bunge kabla sijaanza kugombea na sheria nazifahamu vizuri, itakuwa rahisi kwangu kuyashughulika matatizo yote tofauti na Masaburi ambaye hata bunge halijui zaidi ya kufika Halmashauri tu,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema tatizo la ukosefu wa maji jimboni atalitafutia ufumbuzi wa kudumu. “Mkishapiga kura na endapo nikipita kwa sababu najua matokeo yatatoka saa nane mchana (Oktoba 26) asubuhi yake saa tatu naanza kupiga kazi,” amesema.

error: Content is protected !!