DONALD Njonjo, Meneja wa Maabara katika Tume ya Madini anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh Milioni 507.3, Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).
Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Kanda hiyo leo tarehe 11 Julai 2019 amewaambia waandishi wa habari kuwa walimkamata Njonjo baada ya kupata taarifa zake kutoka kwa Ally Sadick, Afisa Madini jijini Dar es Salaam.
Mambosasa amesema baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa hizo lilianza uchunguzi mara moja na kubaini kwamba Njonjo alianza kuiba madini hayo tangu mwezi Desemba 2018, ambapo hadi anakamatwa alikuwa ameshaiba madini zaidi ya Kg. 6.244.
“Jeshi la Polisi linamshikilia Njonjo (30) kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu mali ya serikali kilogram 6.244 yenye thamani ya Tsh 507,347,000,.Yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye Kasiki katika ofisi za wakala wa madini Masaki Jijini Dar es salaam,” amesema.
Ameeleza kuwa baada ya kumhoji Njonjo alikiri kuhusika na wizi huo na kwamba alikuwa anayaficha madini hayo kwenye chumba kilichomo katika jengo la ofisi za Tume ya Madini, zilizoko Masaki jijini Dar es Salaam.
“Mtuhumiwa alieleza kuwa madini hayo aliyauza katika duka la kuuzia vito vya dhahabu na kisha kuhifadhi madini bandia yenye uzito wa kilo 6.001 nyuma ya jengo la tume ya madini, ili kuyapeleka katika chumba walichoiba madini hayo halisi ili kuyabadilisha,” amesema.
Hata hivyo amesema kuwa Njonjo aliiba madini halisi ya dhahabu yaliyokamatwa mwaka 2017 maeneo ya Bandarini Zanzibar yakiwa yanasafirishwa kinyume cha sheria kisha kutafishwa na serikali na kuhifadhiwa katika ofisi za Tume ya Madini.
Aidha, Mambosasa amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linakamilisha upelelezi wa tukio hilo na liko kwenye hatua za mwisho kwa ajili ya kuandaa jalada na kulipeleka kwa mwanasheria wa serikali, kwa ajili ya kuandaa mashtaka ya kumpeleka mhusika mahakamani.
“Nitoe onyo kwa watu ambao wamepewa mamlaka, madaraka na wameaminiwa na serikali kupewa wadhifa wa kama bwana huyu njonjo na yeye anaibia serikali, watumishi wa namna hii hawana nafasi na kila mmoja ajionye kwenye nafasi yake kutenda mambo yanayoendana na serikali,” ameonya Kamanda Mambosasa.
Katika hatua nyingine Kamanda Mambosasa amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata watu saba wanaotuhumiwa kwa ujambazi na kuiba bajaji mbili za wizi na vifaa mbalimbali, maeneo ya Ukonga.
Kamanda Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Salum (27), Amo Kefas (30), Said Ahmad (38), Mohamed Musa (31),Mboke Samwel (26),Abdallah Kipaneli(25) na Mfaume Mussa (25).
“Mnamo tarehe 9 Julai 2019 majira ya saa nane usiku huko maeneo ya Kibeberu na Magole Ukonga watuhumiwa hao walivunja maduka matatu na kufanikiwa kuiba bidhaa mbalimbali, fedha pamoja na bajaji mbili zenye namba za usajili MC 312 CFB aina ya TVS na MC 540 CED aina ya TVS zote zikiwa na rangi ya bluu,” amesema Kamanda Mambosasa na kuongeza.
“Baada ya wizi huo, taarifa zilipokelewa katika kituo cha Polisi Stakishari na upelelezi ulianza maramoja ambapo mnamo tarehe 9 Julai 2019 watuhumiwa walikamatwa huko maeneo ya Hondogo Gogoni Kiluvya wilaya ya Ubungo,” amesema.
Leave a comment