BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeikopesha Serikali ya Tanzania Dola za Marekani 140 (Sh. 323.4 bilioni), kwa ajili ya utekelezaji mradi wa kufua umeme wa nguvu ya maji kwenye Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Mikataba ya mkopo huo wenye mashtari nafuu, imesainiwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi Mkuu wa AfDB Kanda ya Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo.
Akizungumza baada ya mikataba hiyo kusainiwa, Tutuba amesema mradi huo utagharimu dola 144.1 milioni, ambapo AfDB imetoa dola 140 milioni na Serikali ya Tanzania itachangia dola 4.14 milioni.
Tutuba amesema katika mradi huo, kitajengwa kituo kipya cha uzalishaji umeme wa gridi 49.5 megawati.
“Kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha wastani wa GWh 181 za umeme kwa mwaka, kitapunguza utegemeziu wa uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta mazito,” amesema Tutuba.
Pia, Tutuba amesema mradi huo utajumuisha ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme, upanuzi wa mtandao wa kusambaza umeme wa kilovoti 132 na ununuzi wa transfoma mpya 15, ili kuongeza uwezo wa kusambaza umeme kwa wananchi.
Tutuba amesema, mradi huo utaliwezesha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kusambaza vifaa vya kuunganisha wateja 4,250 kwenye wilaya za Kigoma, Kibondo na Kasulu.
Kwa upande wake Nwabufo, amesema mradi huo ni moja ya miradi sita iliyoidhinishwa na AfDB, katika kipindi cha miaka mitatu.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni, mradi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma, wenye thamani ya dola 180 milioni, Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato (dola 271 Mil.).
Barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu (dola 256 Mil.), Barabara ya Bagamoyo – Horohoro – Lunga – Malindi (dola 150 Mil.) na Mradi wa usambazaji umeme wa Nyakanazi – Kigoma (dola 123 Mil.).
Nwabufo amesema kuwa uwekezaji wa benki hiyo Tanzania, imefikia thamani ya dola 2.33 bilioni zilizowekezwa katika sekta za miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji na usafi wa mazingira, kilimo, utawala bora na fedha.
Leave a comment