April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

AFCON 2019; Wasiotarajiwa watengeneza hesabu

Wachezaji wa Madagascar wakishangilia baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya AFCON

Spread the love

JANA usiku vigogo wa soka Afrika, timu ya taifa ya Aljeria iliungana na Madagasca na Afrika Kusini kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kandanda kwa mataifa ya Afrika, AFCON, inayofanyika nchini Misri. Anaandika Yusuf Aboud … (endelea).

Mataifa mengine yaliyotangulia robo fainali ni Nigeria, Benin na Senegal. Leo usiku itachezwa michezo miwili, kupata washindi wawili watakaokamilisha idadi ya timu nane za robo fainali.

Vigogo wengine wa soka la Afrika Magharibi, Ghana watavaana na Tunisia, huku Mali watapapatuana na Ivory Coast. 

Mpaka sasa michuano hii imeshatuonyesha utamu halisi wa soka na maajabu yake.

Kwanza; Wanafainali wote wa msimu uliopita, Camerron na Misri wameshafurushwa kwenye hatua ya mtoano, kabla hata kufika robo fainali. Ikumbukwe Camerron ndio walikuwa mabingwa watetezi na Misri ndio makamo bingwa wa michuano hii.

Misri baada ya kuondoshwa na Afrika Kusini, kocha wake, Javier Aguirre amejiuzuru, huku akisema lawama zote atupiwe yeye na sio wachezaji.

Rais wa Shirikisho la Soka Misri, Abu Reida naye akasema anahusika na lawama na hivyo akafungasha virango na kuachia ofisi bila kulazimishwa.

Kama hiyo haitoshi, wajumbe wote wa Bodi ya shirikisho la soka Misri, nao wakajiona wanapwaya kwenye nafasi zao wameamua kuachia viti.

Huku hayo yakiendelea, kocha wa Uganda, Sebastiane Desebre ameachia ngazi na kuwapa nafasi Shirikisho la soka Uganda, FUFA kutafuta kocha mwingine wa kujaza nafasi.

Desebre, raia wa Ufarasa, ameiacha Uganda baada ya kupata kandarasi ya kuinoa timu ya Al-Ahly ya Misri.

Kocha wa Morocco, Mfaransa Herve Renard amekubali kubeba lawama zote baada ya timu yake kuondoshwa katika hatua ya mtoano na Benin.

Pili; Walioingia kwenye hatua ya mtoano kwa bahati mbaya (Best Looser), Benin na Afrika Kusini tayari wamekata tiketi ya kuingia robo fainali.

Benin na Afrika Kusini zote ziliingia hatua ya mtoano kila moja ikivuna point tatu kwenye hatua ya makundi, ‘wamezitengua udhu’ Morocco na Misri, ambazo kila moja ilikusanya point tisa kwa kushinda michezo yote mitatu katika hatua ya makundi.

Tatu; Utamu unazidi zaidi pale Best Looser, Afrika Kusini kumuondoa Makamu Bingwa, ambaye ndiye mwenyeji Misri na aliyeshika nafasi ya kwanza kwenye kundi A kwa kushinda michezo yote mitatu ya hatua ya makundi.

Wakati michuano hii inaanza, wachambuzi wengi wa soka Afrika na Dunia, waliipa nafasi kubwa Misri ya kutwaa ubingwa.

Lakini pia, Best Looser mwingine, Benin imethibitisha maajabu mengine katika soka kwa kuiondoa miongoni mwa timu nyingine iliyopewa nafasi ya kutwaa ubingwa, Morocco.

Nne; Madagascar inashiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hii, tayari imeshatangulia robo fainali kwa kuiondosha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika hatua ya mtoano.

Hapa maajabu hayapo katika Kongo kutolewa, bali timu iliyoshiriki kwa mara ya kwanza kuiondoa timu iliyoshiriki kwa mara ya 18.

Ingawa hatuwezi kuifananisha Madagascar na Tanzania pamoja na Burundi ambazo nazo unaweza kusema zimeshiriki kwa mara ya kwanza, lakini hatuwezi kuufuta ukweli wa ugeni wa mashindano na udogo wa taifa la Madagascar.

Hatuwezi kuifananisha Madagascar na wageni wengine, kwa sababu katika kikosi cha Madagascar kimejaza wachezaji wazoefu wengi wanaocheza barani Ulaya.

Katika kikosi chao cha wachezaji 23, ni wachezaji watatu tu ndio wanaocheza Afrika, ambao mmoja kipa anayecheza Ligi ya Madagascar, mwingine anacheza JS Aljers ya Aljeria na mwingine anacheza Keizer Chief ya Afrika Kusini.

Alichokifanya kocha wa Madagascar raia ya Ufaransa ni kuwashawishi raia wa Madagascar waliozaliwa Ufaransa, wenye uraia pacha kurudi Madagascar kuitumikia timu ya taifa na akafanikiwa.

Mchezo wa soka haujawahi kuacha kutuonyesha maajabu, na ndiomaana mchezo huu unaongoza kuwa na mashabiki wengi zaidi duniani.

Michezo ya leo usiku kati ya Ghana na Tunisia na ule wa Mali na Ivory Coast, ni wazi utawaondoa vigogo wengine wawili katika hatua hii ya mtoano.

error: Content is protected !!