August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Afande Sele naye akimbia ACT Wazalendo

Selemani Msindi 'Afande Sele' alipokuwa katika kampeni za ACT-Wazalendo

Spread the love

SELEMANI Msindi maarufu kwa jina la “Afande Sele” ambaye ni msanii mkongwe wa muziki wa Hip hop hapa nchini na aliyekuwa mgombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, ametangaza kujivua rasmi uanachama wa chama hicho, anaandika Charles William.

Uamuzi wa Afande Sele unakuja ikiwa ni wiki moja tu tangu Habib Mchange, mmoja kati ya waasisi wa chama hicho na aliyekuwa Katibu wa Kamati ya Mipango atangaze kujivua uanachama wa chama hicho na kuahidi kubaki kama mtanzania asiye na chama.

Katika taarifa yake ya kujivua uanachama Afande Sele aliyoitoa leo, Afande Sele amesema “Leo natangaza rasmi kujivua uanachama wa chama cha ACT-Wazalendo na sitakua mfuasi wa chama chochote cha siasa bali nitabaki kuwa raia wa kawaida ndani ya nchi yetu nikiendelea na majukumu mengine ya kimaisha mpaka nitakavyoamua vinginevyo.”

Hivi karibuni Afande Sele ambaye amekuwa akieleza kutoridhishwa na viongozi wa ACT, akidai wamekuwa vigeugeu kiasi cha kumfanya ashindwe kujua iwapo msimamo wa chama hicho ni kuunga mkono upinzani au chama tawala (CCM).

Amekuwa akimlaumu Zitto Kabwe, kiongozi wa ACT na viongozi wengine wa chama hicho kwa kukifanya chama kuwa “vuguvugu” – kisicho baridi wala moto na kusababisha wanachama wakose pa kusimamia.

Taarifa ya Afande Sele ya leo imehitimisha kwa kusema “naomba kila mmoja aheshimu uamuzi wangu kama mimi ninavyoheshimu maamuzi ya watu wengine kwa mujibu wa Katiba ya nchi.”

Hapo awali, Afande Sele alikuwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kabla ya kutimkia ACT- Wazalendo mnamo mwaka 2015, akimfuata “swahiba wake” Zitto Kabwe aliyejiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa na Chadema kwa madai ya usaliti.

error: Content is protected !!