Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Ado: Rais Samia ameitoa gizani tasnia ya habari
Habari Mchanganyiko

Ado: Rais Samia ameitoa gizani tasnia ya habari

Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo
Spread the love

 

KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameitoa nchi gizani katika masuala ya uhuru wa habari na kujieleza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwanasiasa huyo ameyasema hayo leo tarehe 8 Machi 2023, ikiwa Tanzania na dunia kwa ujumla inaadhimisha siku ya wanawake duniani.

Ado amesema kuwa, Rais Samia ameweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke Tanzania, ambaye amefanikiwa kuitoa tasnia ya habari gizani, kwa kuruhusu uhuru wa kujieleza na hata kuagiza Serikali yake kuifanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Habari ya 2016, ili kuondoa vifungu vyake kandamizi.

“Unapozungumzia uongozi wa Rais Samia kama mwanamke, tunaweza kuona mifano mingi. Kipindi cha nyuma kidogo tulikuwa gizani mnajua nyinyi wenyewe hali ilikuwaje? Leo unapozungumzia mafanikio ya mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari, ndani yake unaona msukumo mkubwa wa Rais Samia. Na katika hili, historia yake ndani ya nchi hii itaandikwa,” amesema.

Akizungumzia mabadiliko ya sheria hiyo, Ado amesisitiza kwamba haoni sababu tasnia ya habari kuundiwa Baraza la Habari ambalo litasimamiwa na serikali, kwa kuwa ndani ya tasnia ya habari kuna watu wenye weledi mkubwa na wenye uwezo wa kujisimamia.

“Kuna mifano katika hili, nakumbuka katika zile vurugu za gesi Mtwara. Ni weledi wa wanahabari pekee waliomaliza vurugu bila kutumia mtutu wala vitisho, kutokana na weledi wao, walikubaliana na kuandika tahariri ambayo ilizima kabisa vurugu Mtwara.

“Angalia kilichofanyika mwaka jana kwenye Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani, Afrika nzima ilikuja Tanzania kusherehekea, wanahabari ndio waliopanga hili na matokeo yake Afrika nzima macho yao yalikuwa Tanzania. Acha wanahabari wajisimamie,” amesema Ado.

Mwanasiasa huyo kijana amesema, ikiwa waandishi wa Kenya wanalo baraza lao la habari lisiloingizwa mikono na serikali sawa na lile la Canada na hata Ghana, amehoji kwani Tanzania isichukue mkondo huo?

“Hoja ya kuwa na Baraza Huru la Habari inaungwa mkono hata na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma aliyewaambia waandishi wa habari, umuhimu wa kuwa na baraza lao la kitaaluma litakalosuluhisha kesi zote zinazohusiana na malalamiko kuhusu taaluma yao,” amesema.

Pia amesema, Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 18 na 19 zinatambua uhuru wa kujieleza, kutoa mawazo lakini hakuna sheria ya Bunge inayowapa nguvu waandishi kutambulika kisheria kama wanasheria, madaktari hivyo kukosa ulinzi kikatiba.

Anasema, waandishi wakitambulika kwa sheria ya Bunge, watasimamia masuala yao ya weledi na utendaji kazi na wanapokosea, kupeana adhabu kupitia kamati za maadili kama ilivyo wa tasnia nyingine nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!