May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ado: Khatib amekufa na kilio cha Masheikh Uamsho

Spread the love

 

KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, amesema aliyekuwa Mbunge wa Konde kupitia chama hicho, Hayati Khatib Haji, ameondoka duniani na kilio cha sakata la Masheikh wa Uamsho, visiwani Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Khatib alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, tarehe 20 Mei 2021, alikokuwa anapatiwa matibabu, na mwili wake kuzikwa nyumbani kwao Pemba, Zanzibar, siku hiyo hiyo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, kwa simu , leo Jumapili tarehe 23 Mei 2021, Ado amesema kabla Khatibu hajafariki dunia, alimuandikia ujumbe, akisema kwamba, atakwenda bungeni kuzungumzia sakata hilo, hata kama afya yake haitamruhusu.

“Khatibu alikuwa mbunge wa kipekee sana, kwa wanaofuatilia takribani miezi sita ya uwepo wake bungeni amechangia mara nyingi hoja mbalimbali juu ya katiba mpya, tume huru uya uchaguzi na haki za binadamu bila kusahau masheikh wa uamsho,” amesema Ado.

Katibu Mkuu huyo wa ACT-Wazalendo amesema, “hata wakati anaumwa Khatib aliniandikia ujumbe akisema katibu mkuu naumwa, lakini nitakwenda bungeni kuna jambo la msingi lazima niseme kisha nitarudi hospitali. Amekufa na ajenda ya masheikh wa uamsho.”

Marehemu Khatib Said Haji

Ado amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie kati suala hilo ili kumuenzi Khatib, kwa kuhakikisha kesi inayowakabili masheikh hao inafika mwisho.

Kabla ya kufikwa na mauti, tarehe 14 Aprili 2021, akiwa bungeni jijini Dodoma, Khatib aliiomba Serikali kupitia mamlaka za uchunguzi pamoja na mahakama, ziharakishe uendeshwaji wa kesi hiyo, ili masheikh hao wapate haki yao.

“Naibu Spika (Dk. Tulia Ackson) napenda kusema kwamba, huu ni mwezi mtukufu wa ramadhani, na tarehe 3 Novemba 2014 nilisimama hapa kuongelea ucheleweshaji wa kesi na niligusia sana kesi ya masheikh wa uamsho Zanzibar.

Nilisema wakati huo kesi ikiwa na miaka minne, leo nataka kusema imefikia mwaka wa nane una kwenda wa tisa, kesi ile imechelewa sana,” alisema Khatib.

Khatib alisema “kila mshtakiwa anakwenda mahakamani anachosubiri hukumu ya makosa yake, haki ya mtuhumi ni kuhukumiwa sio kukaa gerezani kipindi kirefu, kunyongwa ni hukumu,kifungo cha maisha ni haki ya mshtakiwa kulingana na makosa yake. Unamponyima hukumu mshtakiwa tayari unamnyima haki yake ya msingi.”

Kwa sasa Masheikh hao wanakabiliwa na Kesi ya Jinai Na. 121/2021, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Awali walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 25 ya makosa ya ugaidi, lakini Aprili mwaka huu, mahakama hiyo iliwafutia mashtaka 14, na kubaki mashataka 11.

Kwa mujibu wa Mwansheria Kiongozi wa Jopo la Mawakili wanaowatetea masheikh hao, Juma Nasoro, mashtaka yaliyofutwa na mahakama hayo, ni yale wanayodaiwa kutenda Zanzibar, na yaliyobaki, wanadaiwa kuyatenda Tanzania Bara.

Masheikh hao wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 walijihusisha na makosa ya ugaidi, kinyume na kifungu cha 27 (c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.

error: Content is protected !!